< Ezekieli 37 >

1 Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa Bwana na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele.
Mkono wa Yahwe ulikuwa juu yangu, na akanitoa kwa Roho wa Bwana Yahwe na kuniweka chini katikati ya bonde; lilikuwa limejaa mifupa.
2 Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana.
Kisha akanifanya kupita kati yao kuizunguka pande zote. Tazama! Mingi yao mikubwa ilikuwa katika bonde! Ilikuwa mikavu sana.
3 Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?” Nikajibu, “Ee Bwana Mwenyezi, wewe peke yako wajua.”
Akanambia, “Mwanadamu, Je! Hii mifupa inaweza kuishi kinyume?” Hivyo nikasema, “Bwana Yahwe, wajua wewe pekee.”
4 Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la Bwana!
Kisha akanambia, “Tabiri juu ya hii mifupa na iambie, 'Mifupa mikavu. Lisikilizeni neno la Yahwe.
5 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa hii mifupa: Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
Bwana Yahwe asema hivi kwenye hii mifupa: Tazama! nakaribia kuweka pumzi juu yenu, nanyi mtaishi.
6 Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’”
Nitaweka mishipa juu yenu na kuleta nyama juu yenu. Nitawafunika kwa ngozi na kuweka pumzi ndani yenu hivyo mtaishi. Kisha mtajua kwamba mimi ni Yahwe.”'
7 Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Wakati nilipokuwa ninatabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
Hivyo nimetoa unabii kama nilivyokuwa nimeamriwa: nimetabiri, tazama, sauti ikaja, iliyokuwa ya mtetememo. Kisha mifupa ikasogeleana pamoja-mfupa juu ya mfupa.
8 Nikatazama, mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini hapakuwepo pumzi ndani yake.
Nikatazama na, kumbe, mishipa ilikuwa juu sasa, na nyama ikatoka juu na ngozi ikazifunika. Lakini hapakuwa na pumzi juu yao.
9 Ndipo aliponiambia, “Utabirie upepo, tabiri, mwanadamu na uuambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Njoo kutoka pande nne, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’”
Kisha Yahwe akanambia, “Itabirie pumzi, tabiri, mwanadamu, na iambie pumzi, 'Bwana Yahwe asema hivi: Pumzi, hutoka pepo nne, na pumzi juu ya hawa walioawa, hivyo wanaweza kuishi.”'
10 Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
Hivyo nimetabiri kama nilivyokuwa nimeamriwa; pumzi ikawajilia na wakaishi. Kisha wakasimama kwa miguu yao, jeshi moja kubwa sana.
11 Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’
Kisha Yahwe akanambia, “Mwanadamu, mifupa hii yote ni ya nyumba ya Israeli. Tazama! Wanasema, 'Mifupa yetu imekauka, na tumaini letu limepotea. Tumekatwa.'
12 Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli.
Kwa hiyo tabiri na waambie, 'Bwana Yahwe asema hivi: Tazama! Nitayafunua makabiri yenu na kuwapandisha kutoka kwayo, watu wangu. Nitakurudisha hata katika nchi ya Israeli.
13 Ndipo ninyi watu wangu, mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo.
Kisha mtajua kwamba mimi ni Yahwe, nitakapo yafunua makaburi yenu na kuwatoa kutoka kwao, watu wangu.
14 Nitatia Roho yangu ndani yenu nanyi mtaishi, nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtakapojua kwamba Mimi Bwana nimenena, nami nitalitenda, asema Bwana!’”
Nitaweka Roho wangu ndani yenu hivyo mtaishi, na nitawafanya kupumzika katika nchi yenu mtakapojua yakwamba mimi ni Yahwe. Nasema na nitayafanya hayo-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”'
15 Neno la Bwana likanijia kusema:
Kisha neno la Yahwe likanijia, likisema,
16 “Mwanadamu, chukua fimbo na uandike juu yake, ‘Hii ni kwa ajili ya Yuda na Waisraeli waliofungamana naye.’ Kisha chukua fimbo nyingine, uandike juu yake, ‘Fimbo ya Efraimu, ni kwa ajili ya Yosefu na nyumba yote ya Israeli wanaofungamana naye.’
“Sasa wewe, mwanadamu, chukua fimbo moja kwa ajili yako na andika juu yake, 'Kwa ajili Yuda na kwa ajili ya watu wa Israeli, wenzake,' Kisha fimbo nyingine andika juu yake, 'Kwa kuwa Yusufu, tawi la Efraimu, na kwa ajili ya watu wa Israeli, wenzake.
17 Ziunganishe pamoja kuwa fimbo moja ili kwamba ziwe fimbo moja katika mkono wako.
Walete wote pamoja kwenye fimbo moja, ili wawe kitu kimoja katika mkono wako.
18 “Watu wako watakapokuuliza, ‘Je, hutatuambia ni nini maana ya jambo hili?’
Wakati watu wako watakapokwambia na kusema, 'Je! hutatuambia haya mambo yako yana maana gani?'
19 Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaichukua fimbo ya Yosefu, iliyoko mikononi mwa Efraimu na ya makabila ya Israeli yanayofungamana naye na kuiunganisha na fimbo ya Yuda, nikizifanya kuwa fimbo moja, nao watakuwa wamoja katika mkono wangu.’
kisha waambie, 'Bwana Yahwe asema hivi: Tazama! Nalichukua tawi la Yusufu ambalo lipo kwenye mkono wa Efraimu na kabila za Israeli wenzake na kuungana nalo hata kwenye tawi la Yuda, ili kwamba wawe tawi moja, na watakuwa kitu kimoja katika mikono yangu.'
20 Inua mbele ya macho yao zile fimbo ulizoziandika
Shika kwenye mkono wako na matawi uliyoandika mbele ya macho yao.
21 kisha waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawatoa Waisraeli katika mataifa walikokuwa wamekwenda. Nitawakusanya popote walipo na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe.
Waambie, 'Bwana Yahwe asema hivi: Tazama! nakaribia kuwachukua watu wa Israeli kutoka miongoni mwa mataifa walipoenda. Nitawakusanya kutoka nchi zilizozunguka na nitawaleta kwenye nchi yao.
22 Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, katika milima ya Israeli. Patakuwa na mfalme mmoja juu yao wote na kamwe hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili au kugawanyika katika falme mbili.
Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, juu ya milima ya Israeli, na kutakuwa na mfalme mmoja kama mfalme juu yao wote, na hawatakuwa mataifa mawili tena. Hawatagawanyika kwenye falme mbili tena.
23 Hawatajitia tena unajisi kwa sanamu zao na vinyago vyao visivyo na maana wala kwa makosa yao yoyote, kwa maana nitawaokoa kutoka dhambi zao zote zilizowarudisha nyuma, nami nitawatakasa. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
Kisha hawatajitia unajisi tena kwa sanamu zao, mambo yao yachukizao, au dhambi zao nyingine. Kwa kuwa nitawaokoa kutoka matendo yao ya uongo ambayo wamefanya dhambi, na nitawatakasa, hivyo watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao.
24 “‘Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja. Watafuata sheria zangu na kuzishika amri zangu kwa uangalifu.
Daudi mtumishi wangu atakuwa mfalme juu yao. Hivyo kutakuwa na mchungaji mmoja juu yao wote, na wataishi kulingana na sheria zangu na watazitunza amri zangu na kuzitii.
25 Wataishi katika nchi niliyompa mtumishi wangu Yakobo, nchi ambamo baba zenu waliishi. Wao na watoto wao na watoto wa watoto wao wataishi humo milele, naye Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele.
Wataishi katika nchi niliwapatia watumishi wangu Yakobo, ambapo baba zenu walipoishi. Wataishi humo milele-wao, watoto wao, na wajukuu zao, kwa Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele.
26 Nitafanya nao Agano la amani, litakuwa Agano la milele. Nitawafanya imara na kuongeza idadi yao, nami nitaweka mahali patakatifu pangu miongoni mwao milele.
Nitaweka agano la amani pamoja nao. Litakuwa agano la milele pamoja nao. Nitawaweka na kuwazidisha na kupaweka mahali patakatifu pangu katikati yao milele.
27 Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
Maskani yangu yatakuwa pamoja nao; Nitakuwa Mungu wao, na watakuwa watu wangu.
28 Ndipo mataifa watakapojua kwamba Mimi Bwana ndiye ninayeifanya Israeli kuwa takatifu, wakati mahali patakatifu pangu patakapokuwa miongoni mwao milele.’”
Kisha mataifa watajua yakwamba mimi ni Yahwe niliyewatenga Israeli, wakati mahali pangu patakatifu patakapokuwa katikati yao milele.”

< Ezekieli 37 >