< Ezekieli 26 >

1 Mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema:
Hivyo ilikuwa katika mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, lile neno la Yahwe likanijia, kusema,
2 “Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema kuhusu Yerusalemu, ‘Aha! Lango la kwenda kwa mataifa limevunjika, nayo milango yake iko wazi mbele yangu, sasa kwa kuwa amekuwa magofu nitastawi.’
“Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemuu, 'Aha! Malango ya watu waliovunjika! Amenigeukia; Nitajazwa kwa sababu ameharibika.'
3 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na wewe, ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi dhidi yako, kama bahari inayovurumisha mawimbi yake.
Kwa hiyo Bwana Yahwe asema hivi, 'Tazama! Niko juu yako, Tiro, na nitayainua mataifa mengi juu yako kama bahari iiunuavyo mawimbi yake.
4 Watavunja kuta za Tiro na kuibomoa minara yake, nitakwangua udongo wake na kuufanya mwamba mtupu.
Wataziharibu kuta za Tiro na kuiangusha chini minara yao. Nitafagia mavumbi yake mbali na kumfanya kama jiwe tupu.
5 Itakuwa huko katikati ya bahari patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki, kwa maana nimenena, asema Bwana Mwenyezi. Atakuwa nyara kwa mataifa,
Atakuwa sehemu ya kuwekea nyavu kati ya bahari, kwa kuwa nimesema hilo-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-na atakuwa mateka kwa ajili ya mataifa.
6 nayo makao yake huko bara yataangamizwa kwa upanga. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.
Binti zake walioko mashambani watachinjwa kwa panga, na watajua kwamba mimi ni Yahwe.'
7 “Kwa maana hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kutoka kaskazini nitamleta dhidi ya Tiro Mfalme Nebukadneza wa Babeli, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi na magari ya vita, wapanda farasi na jeshi kubwa.
Kwa kuwa hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo: Tazama, kutoka kaskazini namleta Nebukadreza mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, dhidi ya Tiro, pamoja na farasi na magari ya farasi, na pamoja na waendesha farasi na watu wengi.
8 Atayaharibu makao yako huko bara kwa upanga, ataweka jeshi kukuzingira, atakuzingira mpaka kwenye kuta za ngome zako na kuinua ngao zake dhidi yako.
Atawaua binti zako katika shamba. Ataweka kazi ya boma na kujenga ulaghai dhidi ya kuta zako na kuziinua ngao dhidi yao.
9 Ataelekeza mapigo ya vyombo vyake vya kubomolea dhidi ya kuta zako na kubomoa minara yako kwa silaha zake.
Ataweka vyombo vya kubomolea dhidi ya kuta zako, na vyombo vyake vitaanguka chini ya minara yako.
10 Farasi zake zitakuwa nyingi sana kiasi kwamba utafunikwa na mavumbi watakayotimua. Kuta zako zitatikisika kwa mshindo wa farasi wa vita, magari makubwa na magari ya vita wakati aingiapo malango yako kama watu waingiao mji ambao kuta zake zimebomolewa kote.
Farasi zake zitakuwa nyingi kwamba mavumbi yao yatawafunika. Kuta zako zitatikisika kwa mlio wa waendesha farasi, magurudumu, na magari ya farasi. Wakati atakapoingia malango yako, ataingia kama watu waingiavyo kwenye mji ambao kuta zimebomolewa.
11 “Kwato za farasi zake zitakanyaga barabara zako zote, atawaua watu wako kwa upanga na nguzo zako zilizo imara zitaanguka chini.
Kwato za farasi zake zitaikanyaga mitaa yako yote. Atawaua watu wako kwa upanga na nguzo za uweza wako zitaanguka chini.
12 Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako.
Watauteka nyara utajiri wako na bidhaa iliyoporwa. Watabomoa kuta zako na kuziharibu nyumba zako za kifahari. Mawe yako, mbao zako, na kokoto watazitupa kwenye maji.
13 Nitakomesha kelele za nyimbo zako, na uimbaji wako wa kinubi kamwe hautasikika tena.
Nitaikomesha sauti ya nyimbo zako. Sauti ya vinubi haitasikika tena.
14 Nitakufanya mwamba mtupu, nawe utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za kuvulia samaki. Kamwe hutajengwa tena, kwa maana Mimi Bwana nimenena, asema Bwana Mwenyezi.
Nitakufanya jiwe tupu, utakuwa mahali ambapo nyavu zitasambazwa kuzikausha. Hutajengwa tena, kwa kuwa mimi, Bwana Yahwe nimesema-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
15 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa Tiro: ‘Je, nchi za pwani hazitatetemeka kwa kishindo cha anguko lako, wakati majeruhi wanapolia kwa maumivu makali na wakati mauaji yanaendelea ndani yako?
Bwana Yahwe amwambia hivi Tiro, 'Je visiwa havitatetemeka kwa mlio wa kuanguka kwako, na pamoja na watakaogumia kwa jeraha wakati machinjio mabaya yatakapokuwa kati yako?
16 Ndipo wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka kutoka kwenye viti vyao vya enzi na kuweka kando majoho yao na kuvua nguo zao zilizotariziwa. Wakiwa wamevikwa hofu kuu, wataketi chini ardhini, wakiwa wanatetemeka kila dakika na wakikustajabia.
Kisha wakuu wote wa bahari watakaposhuka kutoka kwenye viti vyao vya enzi na kuvua mavazi yao rasmi na kutupa mavazi yaliyonakshiwa. Watavaa wenyewe kwa kutetemeka, wataketi chini na kutetemeka kila wakati, na wataogopa kwa sababu yako.
17 Ndipo wao watakuombolezea na kukuambia: “‘Tazama jinsi ulivyoharibiwa, ee mji uliokuwa na sifa, wewe uliyekaliwa na mabaharia! Ulikuwa na nguvu kwenye bahari, wewe na watu wako; wote walioishi huko, uliwatia hofu kuu.
Watainua maombolezo juu yako na kukwambia, umekuwaje, uliyekuwa umekaliwa na manahodha wa meli, umeharibika. Mji mashuhuri ulikuwa imara sana-sasa umetoka kwenye bahari. Wale wanaoishi ndani yake wanaotia hofu kuhusu wenyewe juu ya kila mmoja aliyeishi karibu nao.
18 Sasa nchi za pwani zinatetemeka katika siku ya anguko lako; visiwa vilivyomo baharini vinaogopa kwa kuporomoka kwako.’
Sasa fukwe zitatetemeka katika siku ya kuanguka kwako. Visiwa katika bahari vimeogofya, kwa sababu umekufa.'
19 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitakapokufanya uwe mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa tena na watu, nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako na maji yake makuu yatakapokufunika,
Kwa kuwa Bwana Yahwe asema hivi: wakati nitakapokufanya wewe mji kuwa ukiwa, kama miji mingine ambayo haikaliwi, wakati nitakapoviinua vilindi dhidi yako, na wakati maji makuu yatakapokufunika,
20 ndipo nitakapokushusha chini pamoja na wale washukao shimoni, kwa watu wa kale, nami nitakufanya uishi katika pande za chini za nchi kama katika magofu ya kale, pamoja na wale washukao shimoni, nawe hutarudi au kurejea kwenye makao yako katika nchi ya walio hai.
kisha nitakushusha chini kwenda kwa watu wa nyakati za zamani, kama wengingine walioenda chini kwenye shimo; kwa kuwa nitakufanya uishi katika falme za chini za dunia kama uharibifu wa nyakati za zamani. Kwa sababu hii hutarudi na kusimama katika nchi ya walio hai.
21 Nitakufikisha mwisho wa kutisha wala hutakuwepo tena. Watu watakutafuta, lakini kamwe hutaonekana tena, asema Bwana Mwenyezi.”
Nitaweka janga juu yako, na hutakuwepo tena milele. Kisha utatafutwa, lakini hutapatikana milele tena-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”

< Ezekieli 26 >