< Ezekieli 25 >

1 Neno la Bwana likanijia kusema:
Kisha neno la Yahwe likanijia, kusema,
2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao.
“Mwanadamu, weka uso wako juu ya watu wa Amoni na tabiri juu yao.
3 Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipokwenda uhamishoni,
Waambie watu wa Amoni, 'Sikiliza neno la Bwana Yahwe. Hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo: Kwa sababu umesema, “Aha!” juu ya patakatifu pangu wakati palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli wakati ilipokuwa ukiwa, na juu ya nyumba ya Yuda wakati walipoenda utumwani,
4 kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao katikati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu.
kwa hiyo, tazama, nitakupatia kwa watu katika mashariki kama milki yao. Watafanya kambi juu yako na kuweka mahema miongoni mwako. Watakula matunda yako na watakunywa maziwa yako.
5 Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.
Nitamfanya Raba malisho ya ngamia na watu wa Amoni shamba la mifugo. Kisha utajua yakwamba mimi ni Yahwe.
6 Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umepiga makofi yako na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli,
Kwa kuwa Bwana Yahwe asema hivi: Umepigia makofi mikono yako na kupiga chapa miguu yako, na kufurahi pamoja na dharau ndani yako dhidi ya nchi ya Israeli.
7 hivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yako na kukutoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka kwenye mataifa na kukungʼoa katika nchi. Nitakuangamiza, nawe utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana.’”
Kwa hiyo, tazama! Nitanyoosha mkono wangu na kukupatia kama mateka kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka watu na kukuangamiza kutoka miongoni mwa nchi! Nitakuharibu, na utajua yakwamba mimi ni Yahwe.'
8 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,”
Bwana Yahwe asema hivi, 'Kwa sababu Moabu na Seiri husema “Tazama! Nyumba ya Yuda ni kama kila taifa jingine.”
9 kwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyoko mipakani, yaani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo.
Kwa hiyo, tazama! ntafungua miteremko ya Moabu, kuanzia kwenye miji yake juu ya mpaka-uzuri wa Beth Yeshimothi, Baal Meoni, na Kiriathaimu-
10 Nitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili kwamba Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa,
kwa watu wa mashariki waliokuwa juu ya watu wa Amoni. Nitawapatia kama milki ili kwamba watu wa Amoni hawatakumbukwa miongoni mwa mataifa.
11 nami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’”
Hivyo nitafanya hukumu juu ya Moabu, na watajua yakwamba mimi ni Yahwe.'
12 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Edomu ulilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda na kukosa sana kwa kufanya hivyo,
Bwana Yahwe asema hivi, Edomu amelipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda na amefanya makosa katika kufanya hivyo.
13 kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaunyoosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga.
Kwa hiyo, Bwana Yahwe asema hivi: Nitaunyoosha mkono wangu juu ya Edomu na kumharibu kila mtu na wanyama huko. Nitawaharibu, sehemu ya ukiwa, kutoka Temani hata Dedani. Wataanguka kwa upanga.
14 Nitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana Mwenyezi.’”
Nitaweka kisasi changu juu ya Edomu kwa mkono wa watu wangu Israeli, na watafanya kwa Edomu kulingana na hasira yangu na ghadhabu yangu, na wakitajua kisasi changu-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.'
15 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda,
Bwana Yahwe asema hivi, 'Wafilisti wamelipiza kisasi pamoja na uovu na kutoka ndani yao wamejaribu kuiharibu Yuda tena na tena.
16 kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ninakaribia kuunyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani.
Basi hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo: Tazam! Nitanyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, na nitakalia mbali Wakerethi na kuwaharibu mabaki yaliyobaki karibu na pwani.
17 Nitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapolipiza kisasi juu yao.’”
Kwa kuwa nitalipiza kisasi kikubwa dhidi yao pamoja na matendo ya ghadhabu kubwa ya adhabu, hivyo watajua yakwamba mimi ni Yahwe, nitakapolipiza kisasi juu yao.”'

< Ezekieli 25 >