< Ezekieli 23 >
1 Neno la Bwana likanijia kusema:
Neno la Yahwe likanijia, kusema,
2 “Mwanadamu, walikuwepo wanawake wawili, binti wa mama mmoja.
“Mwanadamu, Kulikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja.
3 Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa huko na wakapoteza ubikira wao.
Walifanya ukahaba katika Misri katika kipindi cha ujana wao. Walitenda kama makahaba huko. Maziwa yao yalikuwa yamebana na ubikira wa chuchu zao zilipapaswa huko.
4 Mkubwa aliitwa Ohola na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa wavulana na msichana. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu.
Majina yao yalikuwa Ohola-dada mkubwa-na Oholiba-dada yake mdogo. Kisha wakawa wangu na kuzaa wana na binti. Majina yao yalikuwa yakimaanasha hivi: Ohola maana yake Samaria, na Oholiba maana yake Yerusalemu.
5 “Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru,
Lakini Ohola alifanya kama kahaba hata alipokuwa wangu; aliwatamani wapenzi wake, kwa kuwa Waashuri na nguvu,
6 waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi.
liwali aliyekuwa amevaa urijuana, na kwa ajili ya maafisa wake, waliokuwa hodari na wanaume wa kuvutia, wote walikuwa waendesha farasi.
7 Akafanya ukahaba na wasomi wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani.
Hivyo akajitoa yeye mwenyewe kama kahaba kwao, kwa watu bora wa Ashuru, na alijitia mwenyewe uchafu pamoja na kila mmoja aliyekuwa amemtamani-pamoja na sanamu zake zote.
8 Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati ambapo tangu ujana wake wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake.
Kwa kuwa hakuacha tabia zake za kihaba nyuma katika Misri, wakati walipolala naye wakati alipokuwa msichana mdogo, wakati walipoanza kwanza kupapasa ubikira wa maziwa yake, wakati walipoanza kummwagia tabia ya uzinzi wao juu yake.
9 “Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani.
Kwa hiyo nilimtia kwenye mkono wa wapenzi wake, kwenye mkono wa Waashuru kwa kuwa aliwatamani.
10 Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe na binti zake, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake na adhabu ikatolewa dhidi yake.
Wakamfunua uchi wake. Wakawachukua wana wake na binti, na wakamuua kwa upanga, na akawa aibu kwa wanawake wengine, hivyo wakapitisha hukumu juu yake.
11 “Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola dada yake.
Dada yake Oholiba akaliona hili, lakini aliyatamani zaidi na kufanya kama kahaba hata zaidi kuliko dada yake.
12 Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia.
Aliwatamanai Waashuru, mabosi na watawala waliokuwa wamevaa ngua za ushawishi, walikuwa watu waendesha farasi. Wote walikuwa hodari, wote vijana wa kuvutia.
13 Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja.
Nikaona kwamba alikuwa amefanya uchafu mwenyewe. Ilikuwa kama kwa wadada wote.
14 “Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo waliovalia nguo nyekundu,
Kisha akaongeza ukahaba wake tena zaidi. Aliona watu waume waliokuwa wamechorwa juu ya kuta, michoro ya Wakaldayo iliyochorwa kwa rangi nyekundu,
15 wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo.
waliovaa mikanda kuzunguka viuno vyao, na vilemba virefu juu ya vichwa vyao. Wote walikuwa na mwonekano wa maafisa wa jeshi la waendesha farasi, mfano wa wana wa Wababeli, ambao asili ya nchi ni Ukaldayo.
16 Mara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo.
Na mara macho yake yalipowaona, aliwatamani, hivyo akawatuma wajumbe wake kwao katika Ukaldayo.
17 Ndipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia.
Kisha Wababeli wakaja katika kitanda chake cha tamaa, na walimfanya unajisi kwa uzinzi wao. Kwa kile alichokuwa amekifanya alifanya unajisi, basi akageuka mwenyewe kutoka kwao katika karaha.
18 Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonyesha hadharani uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake.
Alionyesha matendo yake ya ukahaba na alionyesha uchi wake, hivyo roho yangu ikagauka kutoka kwake, kama roho yangu ilivyogeuka kutoka kwa dada yake.
19 Lakini akazidisha zaidi ukahaba wake alipozikumbuka siku zake za ujana, alipokuwa kahaba huko Misri.
Kisha alifanya matendo mengi zaidi ya ukahaba, akakumbuka na kutafakari siku za ujana wake, wakati alipotenda kama kahaba katika nchi ya Misri.
20 Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi.
Basi akawatamani wapenzi wake, ambao sehemu zao za siri zilikuwa kama zile za punda, na kile kizaliwacho hutoka kilikuwa kama wale farasi.
21 Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na walipokutomasa kwa sababu ya matiti yako machanga.
Hivi ndivyo ulivyofanya matendo ya aibu ya ujana wako, wakati Wamisri walipopapasa chuchu zako kuyaminya maziwa ya ujana wako.
22 “Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande:
Kwa hiyo, Oholiba, Bwana Yahwe asema hivi, 'Tazama! Nitawarudisha wapenzi wako dhidi yako. Wale ambao uliowarudisha, nitawaleta juu yako kutoka kila upande.
23 Wababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi.
Wababeli na Wakaldayo wote, Pekodi, Shoa, na Koa, na Waashuru wote pamoja nao, hodari, vijana wa kutamanika, magavana na maamiri jeshi, wote ni maafisa na watu wote wenye sifa, wote wenye kuendesha farasi.
24 Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kofia za chuma. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao.
Watakuja juu yako kwa silaha, na kwa magari ya farasi na mikokoteni, na kundi kubwa la watu. Watapanga ngao kubwa, ngao ndogo, na kofia za chuma juu yako pande zote. Nitawapatia nafasi kukuadhibu, na watakuadhibu kwa matendo yao.
25 Nitaelekeza wivu wa hasira yangu dhidi yako, nao watakushughulikia kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako na binti zako, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto.
Kwa kuwa nitaweka hasira yangu ya wivu juu yako, na watashughulika na wewe kwa hasira. Watakukatilia mbali pua zako na masikio yako, na masalia yako wataanguka kwa upanga. Watawachukua wana wako na binti zako, na masalia yako watateketea kwa moto.
26 Watakuvua pia nguo zako na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu.
Watakuvua nguo zako na kuchukua mapambo yako ya vito.
27 Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani tena, wala kukumbuka Misri tena.
Hivyo nitaiondoa tabia yako ya aibu kutoka kwako na matendo yako ya kikahaba kutoka nchi ya Misri. Hutainua macho yako kuwaelekea kwa sahauku, na hutaikumbuka Misri tena.'
28 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia.
Kwa kuwa Bwana Yahwe asema hivi, 'Tazama! Nitakutia katika mkono wa wale uwachukiao, kukurudisha kwenye mkono wa wale ambao uliokuwa umewarudisha.
29 Watakushughulikia kwa chuki na kukunyangʼanya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako
Watashughulika pamoja nawe kwa chuki; watachukua milki zako zote na kukutelekeza uchi na kukuweka wazi. Uchi wa aibu ya ukahaba wako utafunuliwa, tabia yako ya aibu na uzinzi wako.
30 umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao.
Haya mambo yatafanyika kwako kwa kuwa umetenda kama kahaba, tamaa za mataifa kwazo umetiwa unajisi kwa sanamu zao.
31 Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako.
Umetembea katika njia za dada yako, hivyo nitaweka kikombe chake cha adhabu kwenye mkono wako.'
32 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako, kikombe kikubwa na chenye kina kirefu; nitaletea juu yako dharau na dhihaka, kwa kuwa kimejaa sana.
Bwana Yahwe asema hivi, 'Utakinywea kikombe cha dada yako ambacho ni kirefu na kikubwa. Utakuwa dhihaka na kutawaliwa na dharau-hiki kikombe kimejaa kiasi kikubwa.
33 Utalewa ulevi na kujawa huzuni, kikombe cha maangamizo na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria.
Utajazwa kwa ulevi na huzuni, kikombe cha ushangao na uharibifu; kikombe cha dada yako Samaria.
34 Utakinywa chote na kukimaliza; utakivunja vipande vipande na kuyararua matiti yako. Nimenena haya, asema Bwana Mwenyezi.
Utakinywea na kubakia kitupu; kisha utakivunja vunja na kuyararua maziwa yako kuwa vipande vipande. Kwa kuwa nimesema hivyo-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.'
35 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”
Kwa hiyo, Bwana Yahwe asema hivi, 'Kwa sababu umenisahau na kunitupa mbali nyumba ya mgongo wako, basi pia utachukua matokeo ya tabia zako za aibu na matendo ya uasherati.”'
36 Bwana akaniambia, “Mwanadamu, Je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo,
Yahwe akanambia, “Mwanadamu, Je! utamhukumu Ohola na Oholiba? Basi waambie matendo yao ya machukizo,
37 kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata wamewatoa watoto wao walionizalia kuwa kafara, kuwa chakula kwao.
kwa kuwa wamefanya uzinzi, na kwa kuwa kuna damu juu ya vichwa vyao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, na wamewaweka hata wana wao kwenye moto, kama chakula cha sanamu zao.
38 Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu.
Kisha waliendelea kufanya hivi kwa ajili yangu: Wamepafanya patakatifu pangu unajisi, na katika siku hiyo hiyo wakainajisi Sabato zangu.
39 Siku ile ile walitoa watoto wao kuwa kafara kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupatia unajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu.
Kwa kuwa walipokuwa wamewachinjia watoto wao kwa ajili ya sanamu zao, kisha wakaja hata patakatifu pangu siku hiyo hiyo kupanajisi! Hivyo tazama! Hivi ndivyo walivyofanya kati ya nyumba yangu.
40 “Walituma hata wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako rangi na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu.
Mmewatuma watu kutoka mbali, ambao wajumbe waliwatuma-sasa tazama. Wakaja kweli, ambao uliojiosha kwa ajili yao, uliweka rangi macho yako, na kujipamba kwa mapambo ya vito.
41 Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu.
Huko ulikaa kwenye kitanda kizuri na kwenye meza iliyokuwa imepangwa mbele yake ulikuwa umeweka ubani na mafuta yangu.
42 “Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao.
Hivyo sauti za watu zilikuwa zimemzunguka; pamoja na watu wa kila aina, hata walevi waliletwa kutoka jangwani, na wakawavalisha vikuku mikononi mwao na mataji mazuri juu ya vichwa vyao.
43 Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’
Kisha nikasema juu yake aliyekuwa ameonywa kwa uzinzi, 'Sasa watazini pamoja naye, na yeye pamoja nao.'
44 Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba.
Wakamwingilia na kulala naye kama watu wamwingiliavyo kahaba. Katika njia hii walilala Ohola na Oholiba, waliokuwa wanawake wazinzi.
45 Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.
Lakini watu wenye haki watapitisha hukumu na kuwaadhibu kama wazinzi, na watawaadhibu kwa hukumu kwa wale wamwagao damu, kwa sababu wao ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.
46 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo, Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara.
Hivyo Bwana Yahwe asema hivi: Nitainua kundi la watu juu yao na kuwatoa kuwa kitisho na kuteka nyara.
47 Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao na binti zao na kuzichoma nyumba zao.
Kisha hilo kundi la watu litawapiga kwa mawe na kuwakatilia chini kwa panga zao. Watawaua wana wao na binti na kuzichoma nyumba zao.
48 “Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya.
Kwa kuwa nitaondoa tabia ya aibu kutoka kwenye nchi na nidhamu wanawake wote hivyo hawatatenda kama makahaba.
49 Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.”
Hivyo wataweka tabia yenu ya aibu juu yenu. Mtachukua hatia ya dhambi zenu pamoja na sanamu zenu, na kwa njia hii mtajua yakuwa mimi ni Bwana Yahwe.”