< Ezekieli 20 >
1 Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa Bwana, wakaketi mbele yangu.
2 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema:
3 “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema Bwana Mwenyezi.’
4 “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao
5 na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
6 Siku ile niliwaapia wao kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote.
7 Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
8 “‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri.
9 Lakini kwa ajili ya Jina langu nilifanya kile ambacho kingelifanya lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa waliyoishi miongoni mwao na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli kwa kuwatoa katika nchi ya Misri.
10 Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani.
11 Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo.
12 Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi Bwana niliwafanya kuwa watakatifu.
13 “‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani.
14 Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli.
15 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyokuwa nimewapa, yaani, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote,
16 kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao.
17 Lakini niliwahurumia wala sikuwaangamiza wala hakuwafuta kabisa jangwani.
18 Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao.
19 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, fuateni amri zangu tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu.
20 Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
21 “‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani.
22 Lakini nikauzuia mkono wangu na kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kingelifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli.
23 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba ningewatawanya miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali,
24 kwa sababu hawakutii sheria zangu lakini walikuwa wamekataa amri zangu na kuzinajisi Sabato zangu, nayo macho yao yakatamani sanamu za baba zao.
25 Pia niliwaacha wafuate amri ambazo hazikuwa nzuri na sheria ambazo mtu hawezi kuishi kwa hizo sheria.
26 Nikawaacha wanajisiwe kwa matoleo yao, kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu, yaani, kule kuwapitisha wazaliwa wao wa kwanza kwenye moto, nipate kuwajaza na hofu ili wajue kwamba Mimi ndimi Bwana.’
27 “Kwa hiyo, mwanadamu, sema na watu wa Israeli na uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika hili pia, baba zenu walinikufuru kwa kuniacha mimi:
28 Nilipowaleta katika nchi ile ambayo nilikuwa nimeapa kuwapa na kuona kilima chochote kirefu au mti wowote wenye majani mengi, huko walitoa dhabihu zao, wakatoa sadaka ambazo zilichochea hasira yangu, wakafukiza uvumba wenye harufu nzuri na kumimina sadaka zao za kinywaji.
29 Ndipo nikawaambia: Ni nini maana yake hapa mahali pa juu pa kuabudia miungu mnapopaendea?’” (Basi jina la mahali pale panaitwa Bama hata hivi leo.)
30 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Je, mtajinajisi kama vile baba zenu walivyofanya na kutamani vinyago vyao vya machukizo?
31 Mnapotoa matoleo yenu, yaani, wana wenu kafara katika moto, mnaendelea kujinajisi na sanamu zenu zote hadi siku hii ya leo. Je, niulizwe neno na ninyi, ee nyumba ya Israeli? Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, mimi sitaulizwa neno na ninyi.
32 “‘Lile lililoko mioyoni mwenu kamwe halitatokea, mnaposema, “Tunataka tuwe kama mataifa mengine, kama watu wengine wa dunia, wanaotumikia miti na mawe.”
33 Hakika kama niishivyo asema Bwana Mwenyezi, nitatawala juu yenu kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa.
34 Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa.
35 Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso.
36 Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema Bwana Mwenyezi.
37 Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa Agano.
38 Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.
39 “‘Kwa habari zenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu.
40 Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema Bwana Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote.
41 Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa.
42 Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu.
43 Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda.
44 Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi Bwana, nitakaposhughulika nanyi kwa ajili ya Jina langu na wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema Bwana Mwenyezi.’”
45 Neno la Bwana likanijia kusema:
46 “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri juu ya upande wa kusini na utoe unabii juu ya msitu wa Negebu.
47 Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la Bwana. Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo.
48 Kila mmoja ataona kuwa mimi Bwana ndiye niliyeuwasha huo moto, nao hautazimwa.’”
49 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mwenyezi! Wao hunisema, ‘Huyu si huzungumza mafumbo tu?’”