< Ezekieli 19 >

1 “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli
“Tena wewe, chukua maombolezo juu ya viongozi wa Israeli
2 na useme: “‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike miongoni mwa simba! Alilala katikati ya wana simba na kulisha watoto wake.
na sema, 'Mama yako alikuwa nani? Simba jike mmoja, aliishi na mtoto wa simba dume; katikati ya simba wadogo, aliwalisha watoto wake.
3 Alimlea mmoja wa watoto wake, naye akawa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu.
Alimlea mmoja wa wale watoto kurarua wanyama wengine, na kisha alijifunza jinsi ya kuwinda watu na kuwala.
4 Mataifa wakasikia habari zake, naye akanaswa katika shimo lao. Wakamwongoza kwa ndoana mpaka nchi ya Misri.
Kisha mataifa wakasikia kuhusu yeye. Akakamatwa kwenye mtego wao, na wakamleta kwa kulabu hata nchi ya Misri.
5 “‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki, nayo matarajio yake yametoweka, akamchukua mwanawe mwingine na kumfanya simba mwenye nguvu.
Kisha alipoona kwamba ingawa alikuwa akimsubiri arudi, matumaini yake sasa yalienda, hivyo alimchukua mtoto wake wengine katika watoto wake na kumlea hata kuwa mwana simba.
6 Alizungukazunguka miongoni mwa simba, kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu.
Huyu mwana simba alitembea huku na huku katikati ya simba. Akawa mwana simba na kujifunza kuwinda mawindo; akala watu.
7 Akabomoa ngome zao na kuiharibu miji yao. Nchi na wote waliokuwa ndani yake wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake.
Akawakamata wajane na kuiharibu miji. Nchi na viijazavyo vilitelekezwa kwa sababu ya sauti ya kunguruma kwake.
8 Kisha mataifa wakaja dhidi yake kutoka sehemu zilizomzunguka. Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake, naye akanaswa katika shimo lao.
Lakini mataifa yakaja juu yake kutoka mikoa yote; wakatengeneza nyavu juu yake. Akakamatwa kwenye mtego wao.
9 Kwa kutumia ndoana wakamvutia kwenye tundu na kumleta mpaka kwa mfalme wa Babeli. Wakamtia gerezani, hivyo kunguruma kwake hakukusikika tena katika milima ya Israeli.
Kwa kulabu wakamuweka kwenye tundu na kisha wakamleta hata kwa mfalme wa Babeli. Wakamleta hata kwenye ngome imara ili kwamba sauti yake isiweze kusikika juu ya milima ya Israeli.
10 “‘Mama yako alikuwa kama mzabibu katika shamba lako la mizabibu uliopandwa kando ya maji, ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi kwa sababu ya wingi wa maji.
Mama yako alikuwa kama mzabibu uliopandwa kwenye damu yako karibu na maji. ulizaa matunda na kujaa matawi kwa sababu ya wingi wa maji.
11 Matawi yake yalikuwa na nguvu, yaliyofaa kuwa fimbo ya enzi ya mtawala. Ulikuwa mrefu kupita miti mingine katikati ya matawi manene; ulionekana kwa urahisi kwa ajili ya urefu wake na wingi wa matawi yake.
Ulikuwa na matawi imara yaliyokuwa yakitumika kwa ajili ya fimbo ya utawala, na kipimo chake kiliinuka juu ya matawi, na kina wake ulionekana kwa ukubwa wa majani yake.
12 Lakini ulingʼolewa kwa hasira kali na kutupwa chini. Upepo wa mashariki uliufanya usinyae, matunda yake yakapukutika, matawi yake yenye nguvu yakanyauka na moto ukayateketeza.
Lakini mzabibu uling'olewa kwa ghadhabu na kutupwa chini hata aridhini, na upepo wa mashariki uliuvunja na kunyauka na moto ukavila.
13 Sasa umepandwa jangwani katika nchi kame na ya kiu.
Hivyo sasa, umepandwa jangwani, kwenye nchi ya ukame na kavu.
14 Moto ulienea kuanzia katika mmojawapo ya matawi yake makubwa na kuteketeza matunda yake. Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake lifaalo kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.’ Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”
Kwa kuwa moto ulitoka kwenye matawi makubwa na kuyala matunda yake. Hakuna tawi imara juu yake, hakuna fimbo ya kifalme kutawala.' Haya ni maombolezo na yataimbwa kama maombolezo.”

< Ezekieli 19 >