< Ezekieli 18 >
1 Neno la Bwana likanijia kusema:
2 “Je, ninyi watu mna maana gani kutumia mithali hii inayohusu nchi ya Israeli: “‘Baba wamekula zabibu zenye chachu, nayo meno ya watoto yametiwa ganzi’?
3 “Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hamtatumia tena mithali hii katika Israeli.
4 Kwa kuwa kila roho ni mali yangu, kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.
5 “Mtu aweza kuwa ni mwenye haki atendaye yaliyo haki na sawa.
6 Hakula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima wala hakuziinulia macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakukutana kimwili na mwanamke wakati wa siku zake za hedhi.
7 Hamwonei mtu yeyote, bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
8 Hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huuzuia mkono wake usifanye mabaya, naye huhukumu kwa haki kati ya mtu na mtu.
9 Huzifuata amri zangu na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu. Huyo mtu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mwenyezi.
10 “Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya
11 (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya): “Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima. Humtia unajisi mke wa jirani yake.
12 Huwaonea maskini na wahitaji. Hunyangʼanyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo.
13 Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
14 “Lakini yawezekana mwana huyo ana mwana aonaye dhambi hizi zote anazofanya baba yake, naye ingawa anaziona, yeye hafanyi mabaya kama haya:
15 “Hakula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima, wala hainulii macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake.
16 Hakumwonea mtu yeyote wala hakutaka rehani kwa ajili ya mkopo. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
17 Huuzuia mkono wake usitende dhambi, hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huzishika amri zangu na kuzifuata sheria zangu. Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi.
18 Lakini baba yake atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe, kwa sababu alitoza bei isiyo halali kwa nguvu, akamnyangʼanya ndugu yake na kufanya yaliyo mabaya miongoni mwa watu wake.
19 “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mwana asiadhibiwe kwa uovu wa baba yake?’ Kwa vile mwana ametenda yaliyo haki na sawa na amekuwa mwangalifu kuzishika amri zangu zote, hakika ataishi.
20 Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Mwana hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya baba yake, wala baba hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya mwanawe. Haki ya mtu mwenye haki itahesabiwa juu yake na uovu wa mtu mwovu utalipizwa juu yake.
21 “Lakini mtu mwovu akiacha dhambi zake zote alizozitenda na kushika amri zangu zote na kufanya lililo haki na sawa, hakika ataishi, hatakufa.
22 Hakuna kosa lolote alilotenda litakalokumbukwa juu yake. Kwa ajili ya mambo ya haki aliyoyatenda, ataishi.
23 Je, mimi ninafurahia kifo cha mtu mwovu? Asema Bwana Mwenyezi. Je, si mimi ninafurahi wanapogeuka kutoka njia zao mbaya na kuishi?
24 “Lakini kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi na kufanya mambo ya machukizo ambayo mtu mwovu hufanya, Je, ataishi? Hakuna hata mojawapo ya matendo ya haki aliyotenda litakalokumbukwa. Kwa sababu ya kukosa uaminifu kwake anayo hatia na kwa sababu ya dhambi alizozitenda, atakufa.
25 “Lakini mnasema, ‘Njia ya Bwana si ya haki.’ Sikia, ee nyumba ya Israeli: Njia yangu siyo iliyo ya haki? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?
26 Kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, kwa sababu ya dhambi alizotenda, atakufa.
27 Lakini mtu mwovu akigeuka kutoka maovu aliyoyatenda na kufanya yaliyo haki na sawa, ataokoa maisha yake.
28 Kwa kuwa anayafikiria na kugeuka kutoka makosa yake yote aliyoyatenda na kuyaacha, hakika ataishi, hatakufa.
29 Lakini nyumba ya Israeli inasema, ‘Njia za Bwana si haki.’ Je, njia zangu si za haki, ee nyumba ya Israeli? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?”
30 “Kwa hiyo, ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu, kila mmoja sawasawa na njia zake, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni! Geukeni kutoka makosa yenu yote, ndipo dhambi haitakuwa anguko lenu.
31 Tupilieni mbali makosa yenu yote mliyoyatenda, nanyi mpate moyo mpya na roho mpya. Kwa nini mfe, ee nyumba ya Israeli?
32 Kwa maana sifurahii kifo cha mtu awaye yote afaye katika uovu, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni basi, mkaishi!