< Ezekieli 16 >

1 Neno la Bwana likanijia kusema:
Kisha neno la Yahwe likanijia, kusema,
2 “Mwanadamu, ijulishe Yerusalemu kuhusu mwenendo wake wa machukizo
“Mwanadamu, mwambie Yerusalemu kuhusu machukizo yake,
3 na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Wewe asili yako na kuzaliwa kwako ni katika nchi ya Kanaani, baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti.
na useme, 'Bwana Yahwe asema hivi kwa Yerusalemu: Mwanzo wako na kuzaliwa kwako kulichukua nafasi katika nchi ya Kanaani; baba yako alikuwa Mwamori, na mama yako alikuwa Mhiti.
4 Siku uliyozaliwa kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo.
Katika siku ya kuzaliwa kwako, mama yako hakukata kitovu chako, wala hakukuosha kwenye maji usafishwe au kukuchua kwa chumvi, wala kukusitiri nguo.
5 Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa.
Hakuna jicho lililokuhurumia kufanya haya mambo kwa ajili yako, kukuhurumia wewe. Katika siku uliyozaliwa, kwa kuchukiwa uhai wako, ulitupwa nje uwandani.
6 “‘Ndipo nilipopita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!”
Lakini nilipita karibu nawe, nalikuona ukijinyonga kwa damu yako mwenyewe, “kubaki hai!”
7 Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote.
Nimekufanya ukue kama mmea katika shamba. Umeongezeka na kuwa mkubwa, na umekuwa mzuri wa wazuri. Maziwa yako yakawa thabiti, na nywele zako zikawa nyingi, ingawa ulikuwa uchi huna nguo.
8 “‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, nililitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye Agano na wewe, asema Bwana Mwenyezi, nawe ukawa wangu.
Nilipita karibu nawe tena, na nalikuona. Tazama! wakati wa upendo umefika kwako, hivyo nikatandika joho langu juu yako na kufunika uchi wako. Kisha nikaapa kwako na kukuleta kwenye agano-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-na ukawa wangu.
9 “‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta.
Basi nilikuosha kwa maji na kukufuta damu yako, na kukupaka mafuta.
10 Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya kamba vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa.
Nilikuvalisha nguo ya taraza na kukuwekea makuzi ya ngozi kwenye miguu yako. Nilikufungia kwa kitani kizuri na kukufunika kwa hariri.
11 Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako,
Kisha nalikupamba kwa vito, na kukuvalisha vikuku kwenye mikono yako, na mkufu kwenye shingo yako.
12 nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako.
Nalitia hazama katika pua yako na hereni katika masikio yako, na taji nzuri juu ya kichwa chako.
13 Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha, nguo zako zilikuwa za kitani safi, hariri na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana ukainuka kuwa malkia.
Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha, na ulivaa kitani safi, hariri, na ngu za taraza; ulikula unga mzuri, asali, na mafuta, na ulikuwa mzuri sana, na ukawa malkia.
14 Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mwenyezi.
Umaarufu wako ukaenda miongoni mwa mataifa kwa sababu ya uzuri wako, kwa kuwa ulikuwa mkamili katika ukuu niliokuwa nimekupa-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
15 “‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uzinzi kwa kila mtu aliyepita, uzuri wako ukawa kwa ajili yake.
Lakini ulitumaini uzuri wako, na ukafanya kama kahaba kwa sababu ya umaarufu wako; umeyamwaga matendo yako ya kikahaba kwa kila aliyepita karibu, ili kwamba uzuri wako uwe wake.
16 Ulichukua baadhi ya mavazi yako ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia miungu, mahali ambapo ulifanyia ukahaba wako. Mambo ya namna hiyo hayastahili kutendeka wala kamwe kutokea.
Kisha ulichukua nguo zako na pamoja nao umepatengeneza mahali pa juu kwa ajili yako palipambwa kwa rangi tofauti tofauti, na hapo ulifanya kama kahaba. Hii haitatokea. Wala haitatokea.
17 Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo.
Umevichukua vito vizuri vya dhahabu na fedha nilizowapatia, na umejitengenezea sanamu za wanaume, na umefanya pamoja nao ukahaba afanyao.
18 Ukayachukua mavazi yako niliyokupa yaliyotariziwa na ukazivalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu.
Ulichukua nguo zako za tarizi na kuwafunika, na kuwawekea mafuta yangu na manukato mbele yao.
19 Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mwenyezi.
Mkate wangu niliokupatia-ulitengenezwa kwa unga mzuri, mafuta, na asali-umeviweka mbele yao kwa ajili ya kunukia harufu nzuri, kwa kuwa hivi ndivyo ilivyotokea-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
20 “‘Nawe uliwachukua wanao na binti zako ulionizalia mimi na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha?
Kisha uliwachukua watoto wako ulionizalia, na kuwatoa sadaka kwa picha ili waliwe kama chakula. Je! matendo yako ya kikahaba ni kitu kidogo?
21 Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu.
Umewachinja watoto wangu na kuwatupia kwenye moto.
22 Katika matendo yako yote ya machukizo, pamoja na ukahaba wako hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako.
Katika machukizo yako yote na matendo yako ya kikahaba hukutafakari kuhusu siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi na bila nguo kama kama umepigwa katika damu.
23 “‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine,
Ole! Ole wako! -hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-kwahiyo, zaidi ya hapo kwa haya maovu yote,
24 Ukajijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za miungu kwenye kila uwanja wa mikutano.
umejijengea chumba cha chini kwa chini katika kila sehemu ya watu wengi.
25 Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za miungu na kuaibisha uzuri wako, ukiutoa mwili wako kwa kuzidisha uzinzi kwa kila apitaye.
Umepajenga mahali pako palipoinuka kwenye kichwa cha kila njia na kuunajisi uzuri wako, kwa kuwa umeutoa mwili wako kwa kila mtu apitaye karibu na umefanya matendo mengi zaidi ya ukahaba.
26 Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, jirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako.
Umetenda kama kahaba pamoja na Wamisri, tamaa ya jirani zako, na umetenda matendo mengi zaidi ya kikahaba, ili kuchochea hasira yangu.
27 Hivyo nilinyoosha mkono wangu dhidi yako na kuipunguza nchi yako, nikakutia kwenye ulafi wa adui zako, binti za Wafilisti, walioshtushwa na tabia yako ya uasherati.
Tazama! Nitakunyooshea mkono wangu na kupunguza chakula chako. Nitauchukua uhai wako juu ya adui zako, binti za Wafilisti, ambao walikuwa na haya ya tabia yako ya uchafu.
28 Ulifanya ukahaba na Waashuru pia, kwa kuwa hukuridhika, hata baada ya hayo, ukawa bado hukutosheleka.
Umetenda kama kahaba pamoja na Waashuru kwa sababu hukuweza kuridhika. Umetenda kama kahaba na bado hukuridhika.
29 Ndipo ukaongeza uzinzi wako kwa Wakaldayo nchi ya wafanyabiashara, hata katika hili hukutosheka.
Umefanya matendo mengi zaidi ya kikahaba katika nchi ya jamii ya wana maji wa Ukaldayo, na wala hukuridhika kwa hayo.
30 “‘Tazama jinsi ulivyo na dhamiri dhaifu, asema Bwana Mwenyezi, unapofanya mambo haya yote, ukifanya kama kahaba asiyekuwa na aibu!
Jinsi moyo wako ulivyo dhaifu-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-kwamba utaweza kuyafanya haya mambo yote, matendo ya aibu ya kikahaba?
31 Unapojenga jukwaa lako kila mwanzo wa barabara na kufanyiza mahali pa fahari pa ibada za miungu katika kila kiwanja cha wazi, lakini hukuwa kama kahaba, kwa sababu ulidharau malipo.
Mmepajenga mahali penu pa juu kwenye kichwa cha kila mtaa na kufanya chumba cha chini kwa chini katika kila sehemu ya watu wengi. Bado hukuwa kama kahaba kwa sababu ulikataa kulipwa ujira.
32 “‘Wewe mke mzinzi! Unapenda wageni, kuliko mume wako mwenyewe.
Wewe mwanamke mzinifu, wewe upokeaye wageni badala ya mume wako.
33 Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako.
Watu hulipa kwa kila kahaba, lakini wewe huwapa mshara wako wapenzi wako wote na kuwapa rushwa ili waje kwako pande zote kwa matendo yako ya kikahaba.
34 Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako, hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, wewe ndiye uliyelipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe. Wewe ulikuwa tofauti.
Hivyo kuna tofauti kati yako na hao wanawake wengine, kwa kuwa hakuna hata mmoja ajaye kwako kukuuliza kulala pamoja nao. Badala yake, unawalipa. Hakuna akulipaye.
35 “‘Kwa hiyo, wewe kahaba, sikia neno la Bwana!
Kwa hiyo, wewe kahaba, lisikilize neno la Yahwe.
36 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umemwaga tamaa zako na kuonyesha uchi wako katika uzinzi wako kwa wapenzi wako na kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo na kwa sababu uliwapa damu ya watoto wako,
Bwana Yahwe asema hivi: Kwa sababu umemwaga tamaa yako na kuonyesha sehemu zako za siri kupitia matendo yako ya ukahaba pamoja na wapenzi wako wote pamoja na sanamu zako za chukizo, na kwa sababu ya damu ya watoto wako uliyowapatia sanamu zako,
37 kwa hiyo nitawakusanya wapenzi wako wote, wale ambao ulijifurahisha nao, wale uliowapenda na wale uliowachukia pia. Nitawakusanya wote dhidi yako kutoka pande zote na nitakuvua nguo mbele yao, nao wataona uchi wako wote.
kwa hiyo, tazama! Nitawakusanya wapenzi wako wote uliokutana nao, wote ambao uliowapenda na wote uliowachukia, na nitawakusanya juu yako kila upande. Nitawaonyesha wazi sehemu zako za siri hivyo wanaweza kuona uchi wako wote.
38 Nitakuhukumia adhabu wanayopewa wanawake wafanyao uasherati na hao wamwagao damu, nitaleta juu yenu kisasi cha damu cha ghadhabu yangu na wivu wa hasira yangu.
Kwa kuwa nitakuadhibu kwa uasherati na kumwaga damu, na nitaleta juu yako damu ya hasira yangu na hasira kali.
39 Kisha nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa majukwaa yako na kuharibu mahali pako pa fahari pa ibada ya miungu. Watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vya thamani na kukuacha uchi na bila kitu.
Nitakutia kwenye mikono yao hivyo watakutupa chini kwenye chumba cha chini kwa chini na kupavunja mahali pako pa juu na watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vyote. watakuacha uchi bila nguo.
40 Wataleta kundi la watu dhidi yako, watakaokupiga kwa mawe na kukukatakata vipande vipande kwa panga zao.
Kisha wataleta kundi la watu juu yako na kukupiga kwa mawe, na kukukata kwa panga zao.
41 Watachoma nyumba zako na kutekeleza adhabu juu yako machoni pa wanawake wengi. Nitakomesha ukahaba wako, nawe hutawalipa tena wapenzi wako.
Watachoma nyumba zako na kufanya matendo mengi ya adhabu juu yako kwenye uso wa wanawake wengi, kwa kuwa nitakusimamisha ukahaba wako, na hutawalipa tena wapenzi wako.
42 Ndipo ghadhabu yangu dhidi yako itakapopungua na wivu wa hasira yangu utaondoka kwako. Nitatulia wala sitakasirika tena.
Kisha nitatuliza ghadhabu yangu juu yako; hasira yangu itakuacha, kwa kuwa nitaridhika, na sitakuwa na hasira tena.
43 “‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinikasirisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema Bwana Mwenyezi. Je hukuongeza uasherati juu ya matendo yako yote ya kuchukiza?
Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako na kunifanya nitetemeke kwa hasira kwa sababu ya haya mambo yote, kwa hiyo, tazama! Mimi mwenyewe nitashusha kwa kichwa chako mwenyewe adhabu kwa kile ulichokifanya-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo. Hutaongeza ukahaba kwa matendo yako yote ya machukizo?
44 “‘Kila mtu atumiaye maneno ya mithali hii, atayatumia juu yako: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.”
Tazama! Kila mtu azungumzaye Mithali kuhusu wewe atasema, “Kama alivyo, hivyo pia ni binti yake.”
45 Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimchukia kabisa mume wake na watoto wake, tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowachukia kabisa waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori.
Wewe ni binti wa mama yako, amchukiaye mume wake na mtoto wake, na wewe ni dada wa dada zako aliyewachukia waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako alikuwa Mwamori.
46 Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake, pamoja na dada yake, naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini yako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma.
Dada yako mkubwa alikuwa Samaria na binti zake walikuwa wale waliokuwa wakiishi kaskazini, wakati dada yako mdogo alikuwa ni yule aliyekuwa akiishi kusini mwako, ambaye ni, Sodoma na binti zake.
47 Hukuziendea njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali kwa muda mfupi katika njia zako zote uliharibika tabia zaidi kuliko wao.
Hukuenenda katika njia zao na kuchukua tabia zao na matendo yao, lakini katika njia zako zote ulikuwa mbaya zaidi kuliko walivyokuwa wao.
48 Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.
Kama niishivyo- hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-dada yako Sodoma na binti zake, hawajafanya uovu mwingi kama wewe ulivyofanya na binti zako walivyofanya.
49 “‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji.
Tazama! Hii ilikuwa dhambi ya dada yako Sodoma: Alikuwa na kiburi katika mafanikio yake, uzembe na kutojali kuhusu chochote. Hakuitia nguvu mikono ya maskini na watu wahitaji.
50 Walijivuna na kufanya mambo ya machukizo sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.
Alikuwa na kiburi na kufanya machukizo mbele yangu, hivyo niliwatoa kama nilivyoona.
51 Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko wao, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya.
Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi zako; badala yake, umefanya machukizo mengi kuliko walivyofanya, na umewonyesha hayo dada zako walikuwa bora kuliko wewe kwa sababu ya machukizo yako uyafanyayo!
52 Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya zaidi kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi kuliko wewe. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki.
Hasa wewe, umeonyesha aibu yako mwenyewe; kwa njia hii umewaonyesha dada zako walikuwa bora kuliko wewe, kwa sababu ya dhambi ulizozifanya katika hayo machukizo yako yote. Dada zako sasa wanaonekana bora kuliko wewe. Hasa wewe, umeonyesha aibu yako mwenyewe, kwa njia hii umewaonyesha kwamba dada zako walikuwa bora kuliko wewe.
53 “‘Lakini nitarudisha baraka za Sodoma na binti zake na za Samaria na binti zake, nami nitarudisha baraka zako pamoja na zao,
Kwa kuwa nitarudisha masalia wao-masalia ya Sodoma na binti zake, na masalia ya Samaria na binti zake; lakini masalia yako yatakuwa miongoni mwao.
54 ili upate kuchukua aibu yako na kufedheheka kwa ajili ya yote uliyotenda ambayo yamekuwa faraja kwao wakijilinganisha na wewe.
Kwa kufikiria haya mambo utaonyesha aibu yako; utakuwa mnyenyekevu kwa sababu ya kila kitu ulichokifanya, na kwa njia hii utakuwa faraja kwao.
55 Nao dada zako, Sodoma na binti zake na Samaria na binti zake, watarudishwa kama vile walivyokuwa mwanzoni, nawe pamoja na binti zako mtarudishwa kama mlivyokuwa hapo awali.
Hivyo dada yako Sodoma na binti zake watarudishwa kwenye hali yao ya zamani, na Samaria na binti zake watarudishwa kwenye mashamba yao ya zamani. Kisha wewe na binti zako watarudishwa kwenye hali yako ya kawaida.
56 Hukuweza hata kumtaja dada yako Sodoma kwa sababu ya dharau yako katika siku za kiburi chako,
Sodoma dada yako hakutajwa hata kwa kinywa chako katika siku ulipojiinua,
57 kabla uovu wako haujafunuliwa. Hata hivyo, sasa unadhihakiwa na binti za Edomu na jirani zake wote, na binti za Wafilisti, wale wote wanaokuzunguka wanakudharau.
kabla uovu wako haujafunuliwa. Lakini sasa wewe ni kitu cha dharau kwa binti za Edomu na binti wote wa Wafilisti waliomzunguka. Watu wote wanakudharau wewe.
58 Utachukua matokeo ya uasherati wako na matendo yako ya kuchukiza, asema Bwana.
Utaonyesha aibu yako na matendo yako ya machukizo! -hivi ndivyo Yahwe asemavyo!
59 “‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitakushughulikia kama unavyostahili, kwa kuwa umedharau kiapo changu kwa kuvunja Agano.
Bwana Yahwe asema hivi: Nitashughulika na wewe kama unavyostahili, wewe uliyedharau kiapo chako kwa kulivunja agano.
60 Lakini nitakumbuka Agano nililolifanya nawe wakati wa ujana wako, nami nitaweka nawe Agano imara la milele.
Lakini mimi mwenyewe nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe katika siku za ujana wako, nitaliimarisha agano la milele pamoja na wewe.
61 Ndipo utakapozikumbuka njia zako na kuona aibu utakapowapokea dada zako, wale walio wakubwa wako na wadogo wako. Nitakupa hao wawe binti zako, lakini si katika msingi wa Agano langu na wewe.
Kisha utazikumbuka njia zako na kuona aibu utakapo wapokea dada zako wakubwa na dada zako wadogo. Nitakupatia wao kama binti zako, lakini kwa sababu ya agano lako.
62 Hivyo nitalifanya imara Agano langu na wewe, nawe utajua kuwa Mimi ndimi Bwana.
Mimi nitaweka imara agano lango pamoja nawe, nawe utajua yakwamba mimi ni Yahwe.
63 Basi, nitakapofanya upatanisho kwa ajili yako, kwa yale yote uliyoyatenda, utakumbuka na kuaibika, nawe kamwe hutafumbua tena kinywa chako kwa sababu ya aibu yako, asema Bwana Mwenyezi.’”
Kwa sababu ya haya mambo, utakumbuka kila kitu na kuona aibu, hutafungua mdomo wako tena kuongea kwa sababu ya aibu yako, wakati nitakapokusamehe kwa yale yote uliyoyafanya-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”'

< Ezekieli 16 >