< Ezekieli 12 >
1 Neno la Bwana likanijia kusema:
2 “Mwanadamu, unaishi miongoni mwa watu waasi. Wana macho ya kuona, lakini hawaoni na masikio ya kusikia lakini hawasikii, kwa kuwa ni watu waasi.
3 “Kwa hiyo, mwanadamu, funga mizigo yako kwa kwenda uhamishoni tena wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toka nje na uende mahali pengine kutoka hapo ulipo. Labda wataelewa, ingawa wao ni nyumba ya kuasi.
4 Wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toa nje mizigo yako iliyofungwa kwa ajili ya kwenda uhamishoni. Kisha wakati wa jioni, wakiwa wanakutazama toka nje kama wale waendao uhamishoni.
5 Wakiwa wanakutazama, toboa ukuta utolee mizigo yako hapo.
6 Beba mizigo hiyo begani mwako wakikuangalia uichukue nje wakati wa giza la jioni. Funika uso wako ili usione nchi, kwa maana nimekufanya ishara kwa nyumba ya Israeli.”
7 Basi nikafanya kama nilivyoamriwa. Wakati wa mchana nilitoa vitu vyangu nje vilivyofungwa tayari kwa uhamishoni. Kisha wakati wa jioni nikatoboa ukuta kwa mikono yangu. Nikachukua mizigo yangu nje wakati wa giza la jioni, nikiwa nimeibeba mabegani mwangu huku wakinitazama.
8 Asubuhi neno la Bwana likanijia kusema:
9 “Mwanadamu, je, nyumba ile ya kuasi ya Israeli haikukuuliza, ‘Unafanya nini?’
10 “Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Neno hili linamhusu mkuu aliye katika Yerusalemu na nyumba yote ya Israeli ambao wako huko.’
11 Waambie, ‘Mimi ndiye ishara kwenu.’ “Kama vile nilivyotenda, basi litatendeka vivyo hivyo kwao. Watakwenda uhamishoni kama mateka.
12 “Naye mkuu aliye miongoni mwao atabeba mizigo yake begani mwake kwenye giza la jioni na kuondoka na tundu litatobolewa ukutani kwa ajili yake ili kupitia hapo. Atafunika uso wake ili kwamba asiweze kuiona nchi.
13 Nitatandaza wavu wangu kwa ajili yake, naye atanaswa kwenye mtego wangu, nitamleta mpaka Babeli, nchi ya Wakaldayo, lakini hataiona, naye atafia huko.
14 Wote wanaomzunguka nitawatawanya pande zote, watumishi wake na majeshi yake yote, nami nitawafuatilia kwa upanga uliofutwa.
15 “Wao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana, nitakapowatawanya miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi zote.
16 Lakini nitawaacha wachache wao waokoke na upanga, njaa na tauni, ili kwamba katika mataifa watakakokwenda waweze kutambua matendo ya machukizo waliotenda. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana.”
17 Neno la Bwana likanijia kusema:
18 “Mwanadamu, tetemeka wakati ulapo chakula chako, tetemeka kwa hofu wakati unywapo maji yako.
19 Waambie watu wa nchi: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kuhusu hao wanaoishi Yerusalemu na katika nchi ya Israeli: Watakula chakula chao kwa wasiwasi na kunywa maji yao kwa kufadhaika, kwa kuwa nchi yao itanyangʼanywa kila kitu chake kwa sababu ya udhalimu wa wote wanaoishi humo.
20 Miji inayokaliwa na watu itaharibiwa na nchi itakuwa ukiwa. Ndipo mtakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.’”
21 Neno la Bwana likanijia kusema:
22 “Mwanadamu, ni nini hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia?’
23 Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia wakati kila maono yatakapotimizwa.
24 Kwa maana hapatakuwepo tena na maono ya uongo wala ubashiri wa udanganyifu miongoni mwa watu wa Israeli.
25 Lakini Mimi Bwana nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa maana katika siku zako, wewe nyumba ya kuasi, nitatimiza kila nisemalo, asema Bwana Mwenyezi.’”
26 Neno la Bwana likanijia kusema:
27 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli inasema, ‘Maono yale anayoyaona ni kwa ajili ya miaka mingi ijayo, naye hutabiri kuhusu siku zijazo zilizo mbali.’
28 “Kwa hiyo, waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakuna maneno yangu yatakayocheleweshwa tena zaidi, lolote nisemalo litatimizwa, asema Bwana Mwenyezi.’”