< Kutoka 1 >

1 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli ambao walikwenda Misri na Yakobo, kila mmoja akiwa pamoja na jamaa yake:
Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokuja Misri pamoja na Yakobo kila moja na familia yake:
2 Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda;
Rubeni, Simioni, Lawi, na Yuda,
3 Isakari, Zabuloni na Benyamini;
Isakari, Zebuluni, na Benjamini,
4 Dani na Naftali, Gadi na Asheri.
Dani, Naftali, Gadi, na Asheri.
5 Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yosefu alikuwa tayari yuko Misri.
Jumla ya watu wa ukoo wa Yakobo walikuwa sabini. Yusufu alikuwa Misri tayari.
6 Basi Yosefu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa,
Ndipo Yusufu, pamoja na kaka zake wote, na kizazi chote wakafa.
7 lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, kwa hiyo wakaijaza nchi.
Waisraeli walifanikiwa sana, wakaongezeka sana idadi yao, na wakawa na nguvu maana nchi ilijazwa na wao.
8 Kisha mfalme mpya ambaye hakufahamu habari za Yosefu akatawala Misri.
Wakati huu sasa mfalme mpya asiyemjua Yusufu aliinuka katika Misri.
9 Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kutuliko sisi.
Akawaambia watu wake, “Tazama, hawa Waisraeli ni wengi na wenye nguvu kuliko sisi.
10 Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana dhidi yetu na kuondoka katika nchi hii.”
Njooni na tukae nao kwa akili, ama sivyo wataendelea kuongezeka na kama vita ikiibuka, wataungana na adui zetu, watapigana nasi, na kisha wataondoka.”
11 Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao.
Hivyo wakawekea walinzi ambao waliwatesa kwa kuwatumikisha kazi ngumu. Waisraeli walijenga maghala ya miji kwa ajili ya Farao: Pishoni na Ramsei.
12 Lakini walivyozidi kuteswa ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi; Wamisri wakawaogopa Waisraeli,
Lakini kadiri Wamisri walivyowatesa, ndivyo Waisraeli waliendelea kuongezeka na kusambaa. Hivyo Wamisri wakaanza kuwaogopa Waisraeli.
13 kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili.
Wamisri waliwafanya Waisraeli wafanye kazi kwa nguvu nyingi.
14 Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.
Waliyafanya maisha yao kuwa machungu kwa kuwafanyisha kazi ngumu kwa vinu na matofali na kwa kila aina ya kazi za shambani. Kazi zao zote zilikuwa ngumu.
15 Mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Kimisri waliowazalisha wanawake wa Kiebrania, ambao majina yao ni Shifra na Pua,
Kisha mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Kiebrania; mmoja wao aliitwa jina lake Shifra, na mwingine aliitwa Puha.
16 “Mtakapowazalisha wanawake wa Kiebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni, lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.”
Akasema, “Wakati mnapowasaidia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, chunguzeni wanapozaa. Ikiwa ni mtoto wa kiume, basi muueni; bali ikiwa ni mtoto wa kike, basi mwacheni aishi.”
17 Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi.
Lakini wale Wakunga walimwogopa Mungu na hawakufanya kama mfalme wa Misri alivyowaagiza; badala yake waliwaacha watoto wa kiume waishi.
18 Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”
Mfalme wa Misri akawaita Wakunga na kuwaambia, “Kwanini mmefanya haya, na kuwaacha watoto wa kiume wakaishi?”
19 Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania ni tofauti na wanawake wa Kimisri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”
Wale Wakunga wakamjibu Farao, “Hawa wanawake wa Kiebrania siyo kama wanawake wa Kimisri. Hawa wana nguvu na jasiri sana maana wao humaliza kuzaa kabla hata mkunga hajafika.”
20 Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi.
Mungu aliwalinda hawa Wakunga. Watu waliongezeka kwa idadi na kuwa na nguvu sana.
21 Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.
Kwa sababu wale Wakunga walimwogopa Mungu, aliwapa familia.
22 Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”
Farao akawaagiza watu wote, “Lazima mmutupe kila mtoto wa kiume anayezaliwa katika mto, lakini kila mtoto wa kike wamwache aishi.”

< Kutoka 1 >