< Kutoka 8 >

1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
Kisha Yahweh akazungumza na Musa, “Nenda kwa Farao na umwambie, 'Yahweh anasema hivi: Acha watu wangu waende hili wakaniabudu.
2 Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura.
Ukikataa kuwaruhusu waende, nitaidhuru nchi yako yote kwa vyura.
3 Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga.
Mito itajawa na vyura. Watatoka na kuingia nyumbani kwako, chumbani kwako, na kitandani kwako. Wataenda nyumbani mwa watumishi wako. Wataenda kwa watu wako, kwenye majiko yako, na vyombo vya kukandia mkate.
4 Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’”
Vyura watakushambulia wewe, watu wako, na watumishi wako wote."”'
5 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’”
Yahweh akamwambia Musa, “Mwambie Aruni, 'Nyoosha mkono wako na gongo lako kwenye mito, mifereji, na kwenye mabwawa, na uwatoe vyura juu ya nchi ya Misri.”'
6 Ndipo Aroni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi.
Aruni akanyoosha mkono juu ya maji ya Misri, na vyura wakatoka na kujaza nchi ya Misri.
7 Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.
Lakini wachawi walifanya vivyo hivyo na uchawi wao: waliwatoa vyura juu ya nchi ya Misri.
8 Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kusema, “Mwombeni Bwana awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Bwana dhabihu.”
Kisha Farao akawaita Musa na Aruni na kuwaambia, “Muombeni Yahweh iliawaondoe vyura kwangu na kwa watu wangu. Kisha nitawaacha watu waende, iliwamtolee dhabihu.”
9 Mose akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako na watu wako ili kwamba vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu. Isipokuwa wale walio katika Mto Naili.”
Musa akamwambia Farao, “Unaweza chukuwa fursa ya kuniambia lini nikuombee wewe, watumishi wako, na watu wako, ili vyura waondolewe kwako na nyumbani kwako na wabaki tu kwenye mito.”
10 Farao akasema, “Kesho.” Mose akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama Bwana Mungu wetu.
Farao akasema, “Kesho.” Musa akasema, “Acha iwe kama ulivyo sema, ili kwamba ujue hakuna Mungu mwengine kama Yahweh, Mungu wetu.
11 Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.”
Vyura wataondoka kutoka kwako, nyumbani mwako, kwa watumishi wako, na kwa watu wako. Watabaki tu kwenye mito.”
12 Baada ya Mose na Aroni kuondoka kwa Farao, Mose akamlilia Bwana kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao.
Musa na Aruni wakaondoka kwa Farao. Kisha Musa akamlilia Yahweh kuhusu hao vyura alio waleta kwa Farao.
13 Naye Bwana akafanya lile Mose alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani.
Yahweh akafanya kama Musa alivyo omba: Vyura wakafa kwenye nyumba, nyuani, na mashambani.
14 Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka.
Watu wakawakusanya kwa mafungu, na nchi ikanuka.
15 Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.
Lakini Farao alipoona kuna afadhali, aliufanya moyo wake kuwa mgumu na hakumsikiliza Musa na Aruni, kama Yahweh alivyo sema.
16 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.”
Yahweh akamwambia Musa, “Mwambie Aruni, 'Nyoosha gongo lako na upige udongo chini, iliuwe chawa kati nchi yote ya Misri.”'
17 Wakafanya hivyo, Aroni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto.
Wakanya hivyo: Aruni akanyoosha mkono wake na gongo lake. Akaupiga udongo wa ardhi. Chawa wakaja juu ya watu na wanyama. Udongo wote kwenye ardhi ukawa chawa katika nchi ya Misri.
18 Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.
Wachawi walijaribu kufanya chawa kwa uganga wao lakini hawakuweza. Palikuwa na chawa kwa watu na kwa wanyama.
19 Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Bwana alivyosema.
Kisha wachawi wakamwambia Farao, “Hichi ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ulikuwa Mgumu, hivyo akakataa kuwasikiliza. Ilikuwa kama Yahweh alivyo sema Farao atafanya.
20 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
Yahweh akamwambia Musa, “Inuka asubui mapema na usimame mbele ya Farao anapoenda mtoni. Umwambie, 'Yahweh anasema hivi: “Acha watu wangu waende wakaniabudu mimi.
21 Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri.
Lakini usipo acha watu wangu waende nitatuma kundi la nzi kwako, watumishi wako, na watu wako, na kwenye nyumba zenu. Nyumba za wa Misri zitajawa na makundi ya nzi, na ata ardhi wanayo simama itajawa na nzi.
22 “‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Bwana, niko katika nchi hii.
Lakini katika siku hiyo nitaitendea nchi ya Gosheni tofauti, nchi ambayo watu wangu wanaishi, ilikwamba kusiwe na makundi ya nzi huko. Hili litatokea ili kwamba mjue mimi ni Yahweh katika hii nchi.
23 Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’”
Nitaweka utofauti kati ya watu wangu na watu wako. Hii ishara ya nguvu zangu itatokea kesho"”'
24 Naye Bwana akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi.
Yahweh akafanya hivyo, na kundi kubwa la nzi likaja nyumbani mwa Farao na nyumbani mwa watumishi wake. Katika nchi yote ya Misri, nchi iliharibiwa na makundi ya nzi.
25 Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”
Farao akawaita Musa na Aruni na kuwaambia, “Nendeni, mtolee Mungu wenu dhabihu kwenye nchi yetu.”
26 Lakini Mose akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea Bwana Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Kama tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe?
Musa akasema, “Sio vyema sisi kufanya hivyo, kwa kuwa dhabihu tunazo mtolea Yahweh Mungu wetu zinachukiza kwa Wamisri. Kama tutatoa dhabihu mbele ya macho yao zilizo chukizo kwa Wamisri, hawata tupiga mawe?
27 Ni lazima twende mwendo wa siku tatu mpaka tufike jangwani ili tumtolee Bwana Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.”
Hapana, ni safari ya siku tatu kwenda nyikani ambayo lazima tuende, ili kiutoa dhabihu kwa Yahweh Mungu wetu, kama anavyo tuamuru.”
28 Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea Bwana Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”
Farao akasema, “Nitakuruhusu kwenda kumtolea dhabihu Yahweh Mungu wenu nyikani. Ila usiende mbali sana. Niombee.”
29 Mose akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba Bwana na kesho mainzi yataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake. Hakikisha tu kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea Bwana dhabihu.”
Musa akasema, “Wakati tu nitakapoenda kutoka kwako, nitamuomba Yahweh ili makundi ya nzi yatoke kwako, wewe Farao, na watumishi wako na watu kesho. Lakini usifanye udhalimu tena kwa kutowaacha watu wetu waende kumtolea dhabihu Yahweh.”
30 Ndipo Mose akamwacha Farao na kumwomba Bwana,
Musa akaenda nje kutoka kwa Farao na kumuomba Yahweh.
31 naye Bwana akafanya lile Mose alilomwomba. Mainzi yakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia.
Yahweh akafanya kama Musa alivyo muomba: alitoa makundi ya nzi kutoka kwa Farao, watumishi wake, na watu wake. Hakuna ata mmoja aliye baki.
32 Lakini wakati huu pia Farao akaushupaza moyo wake, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.
Lakini Farao aliufanya moyo wake mgumu tena, na hakuwaacha watu waende.

< Kutoka 8 >