< Kutoka 40 >
1 Kisha Bwana akamwambia Mose:
2 “Simika Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.
3 Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake.
4 Kisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake.
5 Weka madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la Maskani ya Mungu.
6 “Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania;
7 weka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake.
8 Fanyiza ua kuzunguka maskani na uweke pazia penye ingilio la ua.
9 “Chukua mafuta ya upako, ipake Maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani mwake, nayo itakuwa takatifu.
10 Kisha yapake mafuta hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo yatakuwa takatifu sana.
11 Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.
12 “Mlete Aroni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji.
13 Kisha mvike Aroni yale mavazi matakatifu, umtie mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia katikati ya ukuhani.
14 Walete wanawe na uwavike makoti.
15 Kisha watie mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kutiwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.”
16 Mose akafanya kila kitu sawa kama vile Bwana alivyomwagiza.
17 Kwa hiyo Maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili.
18 Mose alipoweka wakfu Maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo.
19 Kisha akalitandaza hema juu ya Maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama Bwana alivyomwagiza.
20 Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake.
21 Kisha Mose akalileta Sanduku ndani ya Maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Bwana alivyomwagiza.
22 Mose akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini ya Maskani ya Mungu nje ya pazia
23 na kupanga mikate juu yake mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwagiza.
24 Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa Maskani ya Mungu
25 na kuziweka taa mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwagiza.
26 Mose akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia
27 na kufukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama Bwana alivyomwagiza.
28 Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la Maskani ya Mungu.
29 Mose akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama Bwana alivyomwagiza.
30 Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia,
31 Naye Mose, Aroni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao.
32 Wakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu kama Bwana alivyomwagiza Mose.
33 Kisha Mose akafanya ua kuizunguka Maskani ya Mungu na madhabahu, pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Mose akaikamilisha kazi.
34 Ndipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu wa Bwana ukaijaza Maskani ya Mungu.
35 Mose hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu wa Bwana ukaijaza Maskani ya Mungu.
36 Katika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya Maskani ya Mungu, wangeondoka;
37 lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, mpaka siku lilipoinuka.
38 Kwa hiyo wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.