< Kutoka 32 >
1 Watu walipoona kuwa Mose amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimkusanyikia Aroni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui jambo lililompata.”
Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Aruni, wakamwambia, “Njoo, katufanyizie sanamu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.”
2 Aroni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu na binti zenu wamevaa, mkaniletee.”
Hivyo Aruni akawaambia, “Zitoeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.”
3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Aroni.
Watu wote wakavua pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, na wakamletea Aruni.
4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akavifanyiza kwa kusubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
Akapoke mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha. Nao wakasema, “Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.”
5 Aroni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Bwana.”
Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Aruni akatangaza akasema,
6 Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.
“Kesho itakuwa sikukuu kwa Yahweh.” Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze.
7 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka.
Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Shuka upesi, kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao.
8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kuyeyusha yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’”
Wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu. Wakasema, 'Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.
9 Bwana akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu.
Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu.
10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”
Basi sasa usinizuie. Ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize. Nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.”
11 Lakini Mose akamsihi Bwana Mungu wake, akasema, “Ee Bwana, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu?
Musa akamsihi sana Yahweh Mungu wake, na kusema,”Yahweh, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?
12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako.
Kwa nini Wamisri kusema, 'Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi?' Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako.
13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’”
Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, 'Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.'”
14 Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
Na Yahweh akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.
15 Mose akageuka, akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma.
Kisha Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake. Mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa.
16 Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.
Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.
17 Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Mose, “Kuna sauti ya vita kambini.”
Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna kelele ya vita kambini.
18 Mose akajibu: “Si sauti ya ushindi, wala si sauti ya kushindwa; ni sauti ya kuimba ninayosikia.”
“Lakini Musa akasema, “Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.”
19 Mose alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima.
Hata alipoyakaribia kambini akaiona ile ndama, na watu wakicheza. Hasira ya Musa ikawaka. Akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima.
20 Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.
Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji. Akawanywesha wana wa Israeli.
21 Mose akamwambia Aroni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”
Musa akamwambia Aruni, “Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao?
22 Aroni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu.
Aruni akasema, “Hasira yako isiwake, bwana wangu. Wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya.
23 Wao waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatufahamu yaliyompata.’
Maana waliniambia, 'Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu. Kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.'
24 Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”
Nikawaambia, 'Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivue; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.”
25 Mose akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Aroni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao.
Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi (maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao)
26 Kwa hiyo Mose akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Bwana, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
Ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, “Mtu awaye yote aliye upande wa Yahweh na aje kwangu.” Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia.
27 Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’”
Akawaambia, Yahweh, Mungu wa Israeli, asema hivi, 'Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake.'”
28 Walawi wakafanya kama Mose alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao 3,000.
Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu.
29 Kisha Mose akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Bwana, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”
Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa Yahweh leo, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili Yahweh awape baraka leo.”
30 Siku iliyofuata Mose akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Bwana, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kuu. Sasa nitakwenda juu kwa Yahweh. Labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
31 Hivyo Mose akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu.
Musa akarejea kwa Yahweh akasema,” Oh! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu.
32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kwenye kitabu ulichoandika.”
Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.”
33 Bwana akamjibu Mose, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kwenye kitabu changu.
Yahweh akamwambia Musa, “Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.
34 Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”
Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Lakini pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.”
35 Ndipo Bwana akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya kwa ndama yule ambaye alitengenezwa na Aroni.
Kisha Yahweh akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Aruni aliifanya.