< Kutoka 31 >

1 Ndipo Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akasema na Musa,
2 “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda,
“Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda
3 nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi,
Nami nimemjaza Bezaleli na roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,
4 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba,
ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,
5 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi.
na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.
6 Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe:
Tena, nimemchagua, awe pamoja naye Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. Nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza. Hii ni,
7 Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema,
hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;
8 meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba,
na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote,
9 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake,
na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake.
10 pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani,
Pia mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
11 pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.”
Pia mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
12 Kisha Bwana akamwambia Mose,
akasema na Musa,
13 “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi Bwana, niwafanyaye ninyi watakatifu.
“Waambie wana wa Israeli, 'Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.
14 “‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akafie mbali na watu wake.
Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
15 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, takatifu kwa Bwana. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe.
Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa.
16 Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa Agano la milele.
Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato. Kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.
17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Bwana aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’”
Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Yahweh alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.
18 Bwana alipomaliza kusema na Mose juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.
Hapo Mungu alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa mkono wake.

< Kutoka 31 >