< Kutoka 30 >
1 “Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba.
Nawe fanya madhabahu ya kufukizia uvumba; utaifanyiza kwa mti wa mshita.
2 Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo.
Urefu wake utakuwa dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; itakuwa mraba; na kwenda juu kwake dhiraa mbili; pembe zake zitakuwa za kitu kimoja nayo.
3 Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka.
Nawe utaifunikiza dhahabu safi juu yake - na mbavu zake kando kando, na pembe zake. Nawe utaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka.
4 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu.
Kisha utaifanyia pete mbili za dhahabu, chini ya ukingo wake katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili utazifanya; nazo zitakuwa mahali pa kuitia miti ya kuichukulia madhabahu.
5 Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu.
Na ile miti utaifanya kwa mti wa mshita, na kuifunikiza dhahabu safi.
6 Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya Sanduku la Ushuhuda, mahali ambapo nitakutana nawe.
Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe.
7 “Itampasa Aroni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa.
Na Aruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi. Atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza,
8 Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Bwana kwa vizazi vijavyo.
na Aruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Yahweh katika vizazi vyenu vyote.
9 Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake.
Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji.
10 Mara moja kwa mwaka Aroni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Bwana.”
Naye Aruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka. Kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote. Ni takatifu sana kwa Yahweh.”
11 Naye Bwana akamwambia Mose,
BWANA akanena na Musa,
12 “Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Bwana fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu.
“Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa BWANA kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.
13 Kila mmoja anayekwenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini. Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Bwana.
Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini). Nusu shekeli kwa sadaka ya Yahweh.
14 Wote wale wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Bwana.
Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka kwangu.
15 Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Bwana kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu.
Watu watakapo leta hii sadaka kwangu kufanya upatananisho, matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua katika hiyo nusu shekeli.
16 Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Bwana kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”
Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania. Ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele yangu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.
17 Kisha Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akamwambia Musa,
18 “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake.
“Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.
19 Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia.
Na Aruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo.
20 Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto,
Hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania au waendepo karibu na madhabahu kunitumikia kwa kuchoma sadaka, watajiosha majini, ili wasife.
21 watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”
Basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.
22 Kisha Bwana akamwambia Mose,
Kisha Yahweh akasema na Musa,
23 “Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500 za manemane ya maji, shekeli 250 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri,
“Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri 250, na kane shekeli 250
24 shekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni.
na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano.
25 Vitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako.
Nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa.
26 Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda,
Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda,
27 meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba,
na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake,
28 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake.
na madhabahu ya kufukizia uvumba, na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake.
29 Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.
30 “Mtie Aroni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani.
Nawe utawatia mafuta Aruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
31 Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo.
Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.
32 Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu.
Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu.
33 Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’”
Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.'”
34 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa,
Yahweh akamwambia Musa, “Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja.
35 pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu.
Nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu.
36 Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu.
Nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana.
37 Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Bwana.
Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili yangu.
38 Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”
Mtu ye yote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.