< Kutoka 29 >

1 “Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari.
Sasa Hivi ndivyo wapaswa kufanya kuwatenga ili wanitumikie kama makuhani. Chukuwa mtoto wa ng'ombe dume na kondoo bila lawama,
2 Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate midogo myembamba.
mkate bila hamira, na keki bila hamira iliyo changanywa na mafuta. Pia chukuwa maandazi bila hamira yalio pakwa mafuta. Fanya maandazi kwa unga mzuri wa ngano.
3 Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili.
Lazima uweke kwenye ndoo moja, leta kwenye ndoo, na kuleta pamoja na ng'ombe dume na wana kondoo wawili.
4 Kisha mlete Aroni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji.
Lazima nawe umlete Aruni na wana wake wawili katika lango la kuingilia hema la kukutania. Lazima uwasafishe Aruni na wana wake kwenye maji.
5 Chukua yale mavazi na umvike Aroni koti, joho la kisibau na kisibau chenyewe pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kisibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliosukwa kwa ustadi.
Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
6 Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu ishikamane na hicho kilemba.
Nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba.
7 Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake.
Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta.
8 Walete wanawe na uwavike makoti,
Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu.
9 pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Aroni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Aroni na wanawe.
Nawe uwakaze mishipi, Aruni na wanawe, na kuwavika kofia. Nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele. Nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.
10 “Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
Kisha utamleta huyo ng’ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng’ombe.
11 Mchinje huyo fahali mbele za Bwana kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
Kisha utamchinja huyo ng’ombe mbele ya Yahweh pa hema ya kukutania. BWANA,
12 Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu.
Kisha twaa baadhi ya damu ya ng’ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu.
13 Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, yale yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu.
Kisha chukuwa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu.
14 Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi.
Lakini nyama yake huyo ng’ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi.
15 “Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Aruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume.
16 Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu.
Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando.
17 Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine.
Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake,
18 Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu. Ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yaYahweh; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa Yahweh kwa njia ya moto.
19 “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake.
Kisha mtwae huyo kondoo mwingine; na Aruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo.
20 Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Aroni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu.
Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Aruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando.
21 Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Aroni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu.
Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Aruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
22 “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani yale yanayofunika ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.)
Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu.
23 Kutoka kwenye kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Bwana, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta na mkate mdogo mwembamba.
Utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya Yahweh.
24 Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Aroni na wanawe na uviinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
Nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Aruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Yahweh.
25 Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Bwana, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele yangu; ni sadaka iliyotengenezwa kwangu kwa njia ya moto.
26 Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Aroni, kiinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako.
Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Yahwe nacho kitakuwa ni sehemu yako.
27 “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Aroni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa.
Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Aruni na wanawe.
28 Siku zote hili litakuwa fungu la kawaida kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Aroni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Bwana kutoka sadaka zao za amani.
Navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya Yahweh.
29 “Mavazi matakatifu ya Aroni yatakuwa ya wazao wake ili kwamba waweze kutiwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa.
Na hayo mavazi matakatifu ya Aruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu.
30 Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba.
Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu.
31 “Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu.
Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu.
32 Aroni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania.
Na Aruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania.
33 Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu.
Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu.
34 Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki mpaka asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu.
Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu
35 “Hivyo utamfanyia Aroni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu.
Ni hivyo utakavyowatendea Aruni na wanawe kama nilivyo kuagiza. Utawaweka kwa kazi takatifu siku saba.
36 Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uitie mafuta na kuiweka wakfu.
Kila siku utamtoa ng’ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa.
37 Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu.
38 “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja.
Lazima utoe kwenye madhabahu wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku
39 Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni.
daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni
40 Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji.
Pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji.
41 Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni. Nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji. Hii itatoa harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwangu kwa njia ya moto.
42 “Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi,
Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Yahweh, hapo nitakapokutana nanyi, ili niseme na wewe hapo.
43 Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu.
Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo; na hiyo hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu.
44 “Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Aroni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani.
Pia Aruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
45 Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao.
Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.
46 Nao watajua kuwa Mimi Ndimi Bwana Mungu wao, aliyewatoa Misri ili nipate kufanya makao miongoni mwao. Mimi Ndimi Bwana Mungu wao.
Nao watanijua kuwa mimi ndimi Yahweh, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao. Ni mimi Yahweh, Mungu wao.

< Kutoka 29 >