< Kutoka 27 >
1 “Jenga madhabahu ya mbao za mti wa mshita, kimo chake kiwe dhiraa tatu; itakuwa mraba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano.
2 Tengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu ziwe zimeungana, na ufunike madhabahu kwa shaba.
3 Tengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama, na vyombo vya kuchukulia moto.
4 Kisha tengenezea hayo madhabahu wavu wa shaba, na utengeneze pete za shaba kwenye kila moja ya hizo pembe nne za huo wavu.
5 Weka wavu huo chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu.
6 Tengeneza mipiko ya mti wa mshita kwa ajili ya madhabahu, na uifunike kwa shaba.
7 Hiyo mipiko itaingizwa kwenye zile pete ili iwe pande mbili za madhabahu inapobebwa.
8 Tengeneza madhabahu yawe na uvungu ndani yake ukitumia mbao. Utaitengeneza sawasawa na vile ulivyoonyeshwa mlimani.
9 “Tengeneza ua kwa ajili ya Hema la Kukutania. Upande wa kusini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja, na utakuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri,
10 pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
11 Upande wa kaskazini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja, nao utakuwa na mapazia, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
12 “Upande wa magharibi wa ua utakuwa na upana wa dhiraa hamsini, nao utakuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi.
13 Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, ua pia utakuwa na upana wa dhiraa hamsini.
14 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yatakuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
15 Kutakuwepo tena na mapazia ya dhiraa kumi na tano kwa upande mwingine wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
16 “Kuhusu ingilio la ua, weka pazia lenye urefu wa dhiraa ishirini la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo litashikiliwa na nguzo nne na vitako vinne.
17 Nguzo zote zinazozunguka ua zitakuwa na tepe na kulabu za fedha, na vitako vya shaba.
18 Ua wa kukutania utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini, ukiwa na mapazia ya kitani yaliyosokotwa vizuri yenye urefu wa dhiraa tano kwenda juu na vitako vya shaba.
19 Vyombo vingine vyote vinavyotumika katika maskani kwa shughuli yoyote, pamoja na vigingi vyote na hata vile vya ua, vitakuwa vya shaba.
20 “Utawaamuru Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili zile taa ziwake mfululizo.
21 Katika Hema la Kukutania, nje ya pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, Aroni na wanawe watahakikisha kuwa taa hizo zinawaka kuanzia jioni mpaka asubuhi mbele za Bwana. Hili litakuwa agizo la milele miongoni mwa Waisraeli kwa vizazi vyote vijavyo.