< Kutoka 26 >

1 “Tengeneza maskani kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi atatarizi makerubi kwenye mapazia hayo.
Lazima ufanye hiyo maskani iwe na mapazia kumi ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, pamoja na makerubi. Kazi ya fundi stadi.
2 Mapazia yote yatatoshana kwa ukubwa: kila moja litakuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne
Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne. Mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja.
3 Unganisha mapazia matano pamoja; fanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.
Mapazia matano yataungwa pamoja, na mapazia matano mengine yataungwa pamoja.
4 Tengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, na ufanye vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho.
Lazima ufanye tanzi za rangi ya samawati upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake. Vivyo hivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili.
5 Fanya vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, nazo vitanzi vyote vielekeane.
Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili.
6 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili vitumike kufunga na kuunganisha mapazia pamoja kufanya Hema liwe kitu kimoja.
Fanya hivi ili hizo tanzi zielekeana. Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganisha hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo na hiyo maskani itakuwa ni moja.
7 “Tengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika maskani.
Lazima ufanye mapazia ya nywele za mbuzi yawe hema juu ya maskani. Lazima ufanye mapazia kumi na moja.
8 Mapazia hayo kumi na moja yatakuwa na kipimo kimoja, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne.
Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne. Hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja.
9 Unganisha hayo mapazia matano yawe fungu moja, na hayo mengine sita yawe fungu lingine. Kunja hilo pazia la sita mara mbili mbele ya maskani.
Lazima utaunganisha mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalikunja hapo upande wa mbele wa ile hema.
10 Tengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine.
Ufanye tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja.
11 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya shaba, uviingize katika vile vitanzi ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.
Kisha ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja.
12 Kuhusu kile kipande cha ziada cha pazia la Hema, nusu ya hilo pazia lililobaki litaningʼinizwa upande wa nyuma wa Hema.
Kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani.
13 Mapazia ya hema yatakuwa na urefu wa dhiraa moja zaidi pande zote, sehemu itakayobaki itaningʼinia pande zote za Hema ili kuifunika.
Lazima kuwe na dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili - ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika.
14 Tengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
15 “Tengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani.
Nawe lazima ufanye hizo fremu za maskani za mti wa mjohoro.
16 Kila mhimili uwe na urefu wa dhiraa kumi na upana wa dhiraa moja na nusu,
Kila fremu utakuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wake kila ubao utakuwa dhiraa moja na nusu.
17 zikiwa na ndimi mbili zilizo sambamba kila mmoja na mwingine. Tengeneza mihimili yote ya maskani jinsi hii.
Kila fremu itakuwa na ndimi mbili, zenye kuunganishwa huu na huu. Ndivyo utakavyozifanya mbao zote za maskani.
18 Tengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa maskani,
Kisha ufanye zile mbao za maskani, mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini.
19 kisha tengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.
Lazima nawe ufanye vitako arubaini vya fedha chini ya zile fremu ishirini. Vitako viwili chini ya fremu moja, kupokea zile ndimi zake mbili, na vitako viwili chini ya fremu nyingine kupokea zile ndimi zake mbili.
20 Kuhusu upande wa kaskazini wa maskani, tengeneza mihimili ishirini
Kwa upande wa pili wa maskani, upande wa kaskazini, mbao ishirini
21 na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
na vitako vyake vya fedha arubaini. Lazima kuwe na vitako viwili chini ya fremu moja, na vitako viwili chini ya fremu nyingine.
22 Kisha tengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa maskani,
Ufanye fremu sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi.
23 na pia utengeneze mihimili miwili ya pembe za upande ulio mbali.
Tena ufanye fremu mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma.
24 Katika pembe hizi mbili ni lazima mihimili yake iwe miwili kuanzia chini mpaka juu, na iingizwe kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili itafanana.
Hizi fremu zitakuwa zimetengana upande wa chini, lakini zimeshinkana kwa juu ya duara moja.
25 Kwa hiyo itakuwepo mihimili minane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
Fremu zitakuwa ni nane, na vitako vyake vya fedha. Vitako kumi na sita, vitako viwili chini ya fremu moja, na vitako viwili chini ya ubao wa pili.
26 “Pia tengeneza mataruma ya mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa maskani,
Lazima ufanye mataruma ya mti wa mshita- mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani,
27 matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili ya mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa maskani.
na mataruma matano kwa ajili ya fremu za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya fremu za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi.
28 Taruma la katikati litapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine.
Na hilo taruma la katikati lililo katikati ya zile fremu, litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu.
29 Funika hiyo mihimili kwa dhahabu, kisha tengeneza pete za dhahabu ambazo zitashikilia hayo mataruma. Pia funika hayo mataruma kwa dhahabu.
lazima uzifunuke hizo fremu kwa dhahabu. Nawe lazima ufanye maduara yake ya za dhahabu, kuwa kama vishikizo, na hayo mataruma utayafunika dhahabu.
30 “Simamisha Hema sawasawa na mfano ulioonyeshwa kule mlimani.
Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake uliooneshwa mlimani.
31 “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atirizi makerubi kwenye hilo pazia.
Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi.
32 Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha.
Kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika vitako vya fedha vinne.
33 Ningʼiniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Mahali Patakatifu kutoka Patakatifu pa Patakatifu.
Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda. Lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana.
34 Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Patakatifu pa Patakatifu.
Nawe lazima utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. Na ile meza utaiweka nje ya pazia.
35 Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa Hema, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa Hema.
Lazima uweke kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini. Lile meza utaiweka upande wa kaskazini.
36 “Kwa ajili ya ingilio la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi.
Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa hema, cha nyuzi za rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshonaji wa taraza.
37 Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia, na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha mimina vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.
Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu. Nawe utasubu vitako vya shaba vitano kwa ajili yake.

< Kutoka 26 >