< Kutoka 26 >
1 “Tengeneza maskani kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi atatarizi makerubi kwenye mapazia hayo.
2 Mapazia yote yatatoshana kwa ukubwa: kila moja litakuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne
3 Unganisha mapazia matano pamoja; fanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.
4 Tengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, na ufanye vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho.
5 Fanya vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, nazo vitanzi vyote vielekeane.
6 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili vitumike kufunga na kuunganisha mapazia pamoja kufanya Hema liwe kitu kimoja.
7 “Tengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika maskani.
8 Mapazia hayo kumi na moja yatakuwa na kipimo kimoja, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne.
9 Unganisha hayo mapazia matano yawe fungu moja, na hayo mengine sita yawe fungu lingine. Kunja hilo pazia la sita mara mbili mbele ya maskani.
10 Tengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine.
11 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya shaba, uviingize katika vile vitanzi ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.
12 Kuhusu kile kipande cha ziada cha pazia la Hema, nusu ya hilo pazia lililobaki litaningʼinizwa upande wa nyuma wa Hema.
13 Mapazia ya hema yatakuwa na urefu wa dhiraa moja zaidi pande zote, sehemu itakayobaki itaningʼinia pande zote za Hema ili kuifunika.
14 Tengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
15 “Tengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani.
16 Kila mhimili uwe na urefu wa dhiraa kumi na upana wa dhiraa moja na nusu,
17 zikiwa na ndimi mbili zilizo sambamba kila mmoja na mwingine. Tengeneza mihimili yote ya maskani jinsi hii.
18 Tengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa maskani,
19 kisha tengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.
20 Kuhusu upande wa kaskazini wa maskani, tengeneza mihimili ishirini
21 na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
22 Kisha tengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa maskani,
23 na pia utengeneze mihimili miwili ya pembe za upande ulio mbali.
24 Katika pembe hizi mbili ni lazima mihimili yake iwe miwili kuanzia chini mpaka juu, na iingizwe kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili itafanana.
25 Kwa hiyo itakuwepo mihimili minane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
26 “Pia tengeneza mataruma ya mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa maskani,
27 matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili ya mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa maskani.
28 Taruma la katikati litapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine.
29 Funika hiyo mihimili kwa dhahabu, kisha tengeneza pete za dhahabu ambazo zitashikilia hayo mataruma. Pia funika hayo mataruma kwa dhahabu.
30 “Simamisha Hema sawasawa na mfano ulioonyeshwa kule mlimani.
31 “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atirizi makerubi kwenye hilo pazia.
32 Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha.
33 Ningʼiniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Mahali Patakatifu kutoka Patakatifu pa Patakatifu.
34 Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Patakatifu pa Patakatifu.
35 Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa Hema, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa Hema.
36 “Kwa ajili ya ingilio la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi.
37 Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia, na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha mimina vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.