< Kutoka 25 >
1 Bwana akamwambia Mose,
2 “Waambie Waisraeli waniletee sadaka. Utapokea sadaka kwa niaba yangu kutoka kwa kila mtu ambaye moyo wake wapenda kutoa.
3 Hizi ndizo sadaka utakazozipokea kutoka kwao: dhahabu, fedha na shaba;
4 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu, pamoja na kitani safi; singa za mbuzi;
5 ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita;
6 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri;
7 na vito vya shohamu na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani.
8 “Kisha uwaamuru wanitengenezee mahali patakatifu, nami nitakaa miongoni mwao.
9 Tengeneza hema hili na vyombo vyake vyote sawasawa na kielelezo nitakachokuonyesha.
10 “Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, upana wa dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
11 Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka.
12 Utalisubu kwa pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine.
13 Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.
14 Utaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba.
15 Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa.
16 Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.
17 “Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu.
18 Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko.
19 Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.
20 Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko.
21 Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku.
22 Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.
23 “Tengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
24 Ifunike kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
25 Kisha tengeneza upapi wenye upana wa nyanda nne, na ufanyie ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote.
26 Tengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na uzifungie kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne.
27 Pete hizo zitakuwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko itakayotumika kuibebea hiyo meza.
28 Tengeneza mipiko hiyo kwa mbao za mshita, uifunike na dhahabu, uitumie kubeba hiyo meza.
29 Tengeneza sahani zake na masinia yake kwa dhahabu safi, pamoja na bilauri na bakuli zake kwa ajili ya kumiminia sadaka.
30 Utaweka mikate ya Wonyesho juu ya meza hii iwe mbele yangu daima.
31 “Tengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vinavyofanana na ua, matovu yake na maua yake viwe kitu kimoja.
32 Matawi sita yatatokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.
33 Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vitakuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yanayotokeza kwenye kile kinara cha taa.
34 Juu ya kinara chenyewe vitakuwepo vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi yakiwa na matovu yake na maua yake.
35 Tovu moja litakuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla.
36 Matovu na matawi yote yatakuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakifuliwa kwa dhahabu safi.
37 “Kisha tengeneza taa zake saba na uziweke juu ya kinara hicho ili ziangaze mbele yake.
38 Mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote zitakuwa za dhahabu safi.
39 Utatumia talanta moja ya dhahabu safi kutengeneza hicho kinara na vifaa vyake vyote.
40 Hakikisha kuwa umevitengeneza sawasawa na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani.