< Kutoka 18 >
1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Mose na watu wake wa Israeli, pia jinsi Bwana alivyowatoa Israeli Misri.
2 Baada ya Mose kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea
3 pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Mose alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
4 Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”
5 Yethro, baba mkwe wa Mose, pamoja na wana wawili wa Mose na mkewe, wakamjia Mose huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu.
6 Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Mose, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”
7 Kwa hiyo Mose akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani.
8 Mose akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Bwana alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsi Bwana alivyowaokoa.
9 Yethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuri Bwana aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri.
10 Yethro akasema, “Sifa na ziwe kwa Bwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri.
11 Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.”
12 Kisha Yethro, baba mkwe wa Mose, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Aroni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Mose mbele za Mungu.
13 Siku iliyofuata, Mose akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni.
14 Baba mkwe wake alipoona yote Mose anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”
15 Mose akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu.
16 Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.”
17 Baba mkwe wa Mose akamjibu, “Unachofanya sio kizuri.
18 Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe.
19 Sasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake.
20 Uwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya.
21 Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.
22 Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe.
23 Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”
24 Mose akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema.
25 Mose akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.
26 Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Mose, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.
27 Kisha Mose akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.