< Kutoka 14 >

1 Ndipo Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akasema na Musa na kumwambia,
2 “Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni.
“Waambie Waisraeli wageuke na kueka kambi mbele ya Pi Hahirothi, katikati ya Migdoli na bahari, mbele ya Baali Zefoni. Wapaswa kueka kambi pembenni ya Pi Hahirothi.
3 Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’
Farao atasema kuhusu Waisraeli, 'Wanaangaika kwenye nchi. Nyikani imewafunika.'
4 Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Bwana.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.
Nitaufanya moyo wa Farao mgumu, na yeye ata wakimbiza. Nitapata utukufu kwasababu ya Farao na jeshi lake lote. Wamisri watajua mimi ni Yahweh.” Kisha Waisraeli wakaeka kambi kama walivyo elekezwa.
5 Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!”
Mfalme wa Misri alipo ambiwa Waisraeli wametoroka, nia ya Farao na watumishi wake ikageuka dhidi ya watu. Wakasema, “Tumefanya nini kwa kuwaacha Waisraeli waende huru na wasitutumikie?”
6 Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake.
Kisha Farao akachukuwa magari yake ya farasi na jeshi lake.
7 Akachukua magari bora mia sita, pamoja na magari mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote.
Alichukuwa magari ya farasi mia sita imara na magari yote ya farasi ya Misri, pamoja na maafisa wa hayo magari.
8 Bwana akaufanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri.
Yahweh akafanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, na mfalme akawafukuzia Waisraeli. Sasa Waisraeli waliondoka kwa shangwe.
9 Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.
Lakini Wamisri wali wafukuzia, pamoja na farasi na magari ya farasi, wapanda farasi, na jeshi lake. Walikuta Waisraeli wameeka kambi pembezoni mwa bahari kati ya Pi Hahirothi na Baali Zefoni.
10 Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Bwana.
Farao alipo karibia, Waisraeli walitaza juu na kushangaa. Wamisri walikuwa wakija kwao, na waliogopa. Waisraeli walimlilia Yahweh.
11 Wakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuwako makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri?
Walimwambia Musa, “Ni kwasababu hakukuwa na makaburi Misri, hadi umetuleta tufe huku nyikani? Kwanini umetutendea hivi, kwa kututoa Misri?
12 Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”
Hili si ndilo tulilo kwambia Misri? Tulikwambia, 'Utuache, ili tuwafanyie Wamisri kazi.' Ingekuwa bora kwetu sisi kuwafanyia kazi kuliko kufa nyikani.”
13 Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena.
Musa akawaambia watu, “Msiogope. Simameni imara na muone wokovu Yahweh atakao uleta kwenu leo. Kwa maana hamtawaona tena Wamisri mnao waona leo.
14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”
Yahweh ata wapigania, na ninyi mtasima imara.”
15 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Kwanini wewe, Musa, unaendelea kuniita mimi? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
16 Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini.
Nyanyua gongo lako juu, nyoosha mkono wako kuelekea baharini na uigawanye sehemu mbili, ili watu wa Israeli wapite baharini kwenye nchi kavu.
17 Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake.
Jitahadharishe kuwa nitafanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu ili wawafuate. Nitapata utukufu kwasababu ya Farao na jeshi lake lote, magari yake ya farasi, na wapanda farasi.
18 Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Bwana nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”
Kisha Wamisri watajua kuwa mimi ni Yahweh nitakapo pata utukufu kwasababu ya Farao, magari yake ya farasi, na wapanda farasi wake.”
19 Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma,
Malaika wa Mungu, aliyeenda mbele ya Waisraeli, aliama na kwenda nyuma yao. Nguzo ya wingu ili sogea mbele yao na kwenda kusimama nyumba yao.
20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.
Wingu lilikuja katikati ya kambi ya Misri na kambi ya Israeli. Lilikuwa wingu jeusi kwa Wamisri, lakini liliangaza usiku kwa ajili ya Waisraeli, hivyo upande mmoja haukuweza kuja karibu ya mwingine usiku wote.
21 Ndipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Bwana akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika,
Musa akanyoosha mkono wake kuelekea bahari. Yahweh akasogeza bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku huo wote na kufanya bahari nchi kavu. Kwa namna hii maji yaligawanyika.
22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
Waisraeli walienda katikati ya bahari kwa nchi kavu. Maji yaliunda ukuta mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto.
23 Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi.
Wamisri waka wafukuzia. Wali wafuata hadi katikati ya bahari - farasi wote wa Farao, magari ya farasi, na wapanda farasi.
24 Karibia mapambazuko, Bwana akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha.
Lakini masaa ya mapema ya asubui, Yahweh alitazama chini jeshi la Wamisri kupitia nguzo ya moto na wingu. Alisababisha hofu miongoni mwa Wamisri.
25 Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Bwana anawapigania dhidi ya Misri.”
Magari yao ya farasi yalikuwa yana kwama matairi, na wapanda farasi waliendesha kwa ugumu. Hivyo Wamisri walisema, “Acha tuwakimbie Waisraeli, kwa kuwa Yahweh anawapigania dhidi yetu.”
26 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.”
Yahweh akamwambia Musa, “Nyoosha mkono kuelekea bahari ili maji yawarudie Wamisri, magari yao ya farasi, na wapanda farasi wao.”
27 Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Bwana akawasukumia ndani ya bahari.
Hivyo Musa akanyoosha mkono wake kuelekea bahari, na ikarudi kwenye hali yake ya kawaida palipo pambazuka. Wamisri walikimbilia ndani ya bahari, na Yahweh akawaingiza Wamisri katikati ndani yake.
28 Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.
Maji yakarudi na kufunika magari ya farasi ya Farao, wapanda farasi, na jeshi lake lote lililo fuata magari ya farasi kwenye bahari. Hakuna aliyepona.
29 Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
Walakini, Waisraeli walitembea kwenye nchi kavu katikati ya bahari. Maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kulia na mkono wa kushoto.
30 Siku ile Bwana akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa.
Hivyo Yahweh akaokoa Israeli hiyo siku kutoka mkono wa Wamisri, na Israeli ikaona maiti za Wamisri ufukweni.
31 Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa Bwana aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa Bwana na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Mose mtumishi wake.
Israeli ilipoona nguvu kubwa Yahweh aliyo itumia dhidi ya Wamisri, watu walimsifu Yahweh, na kumwamini Yahweh na mtumishi wake Musa.

< Kutoka 14 >