< Kutoka 14 >
1 Ndipo Bwana akamwambia Mose,
2 “Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni.
3 Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’
4 Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Bwana.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.
5 Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!”
6 Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake.
7 Akachukua magari bora mia sita, pamoja na magari mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote.
8 Bwana akaufanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri.
9 Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.
10 Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Bwana.
11 Wakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuwako makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri?
12 Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”
13 Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena.
14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”
15 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
16 Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini.
17 Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake.
18 Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Bwana nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”
19 Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma,
20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.
21 Ndipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Bwana akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika,
22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
23 Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi.
24 Karibia mapambazuko, Bwana akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha.
25 Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Bwana anawapigania dhidi ya Misri.”
26 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.”
27 Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Bwana akawasukumia ndani ya bahari.
28 Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.
29 Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
30 Siku ile Bwana akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa.
31 Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa Bwana aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa Bwana na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Mose mtumishi wake.