< Kutoka 10 >
1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili kwamba nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao
2 ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi Bwana.”
3 Kwa hiyo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
4 Kama ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako.
5 Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekane. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu.
6 Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii mpaka leo hii.’” Ndipo Mose akageuka na kumwacha Farao.
7 Maafisa wa Farao wakamwambia, “Mpaka lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu Bwana Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?”
8 Ndipo Mose na Aroni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu Bwana Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaokwenda?”
9 Mose akajibu, “Tutakwenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na kondoo zetu, ngʼombe, mbuzi, farasi na punda kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa Bwana.”
10 Farao akasema, “Bwana awe pamoja nanyi, kama nikiwaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya.
11 La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu Bwana, kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Mose na Aroni wakaondolewa mbele ya Farao.
12 Basi Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya Misri ili kundi la nzige liweze kuingia juu ya nchi na kutafuna kila kitu kiotacho katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.”
13 Kwa hiyo Mose akanyoosha fimbo yake juu ya Misri, Bwana akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige.
14 Wakaivamia Misri yote na kukaa kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe hapajapata kuwepo pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwepo tena.
15 Wakafunika ardhi yote mpaka ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kile chote kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe, kila kitu kiotacho mashambani pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu chochote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri.
16 Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wenu na dhidi yenu pia.
17 Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe Bwana Mungu wako aondoe pigo hili baya kwangu.”
18 Kisha Mose akaondoka kwa Farao akamwomba Bwana.
19 Naye Bwana akaugeuza upepo ukavuma kutoka magharibi, wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki popote katika nchi ya Misri.
20 Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.
21 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.”
22 Kwa hiyo Mose akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu.
23 Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.
24 Ndipo Farao akamwita Mose na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Bwana. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.”
25 Lakini Mose akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Bwana Mungu wetu.
26 Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Bwana Mungu wetu, kwa kuwa mpaka tutakapofika huko hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Bwana.”
27 Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.
28 Farao akamwambia Mose, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”
29 Mose akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”