< Esta 5 >
1 Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa akiketi katika kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni.
Baada ya siku tatu, Esta akajivika mavazi yake ya kimalkia na akasimama sehemu ya ndani ya ua wa ikulu ya mfalme, mbele ya nyumba ya mfalme. mfalme alikuwa ameketi katika kiti chake cha enzi na akitazama mlango wa kuingilia.
2 Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu ile iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme.
Mfalme alipomwona malkia Esta alipata kibali kwa mfalme. Alimpa fimbo ya dhahabu mikononi mwa Esta. Hivyo Esta akamsogelea mfalme na kuishika fimbo ya utawala.
3 Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.”
Kisha mfalme akamwambia Malkia Esta, “Unahitaji upewe nini? Ombi lako ni lipi? Hata nusu ya ufalme wangu utapewa.”
4 Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu ambayo nimeiandaa kwa ajili yake.”
Malkia Esta akamwambia mfalme, kama nimepata kibali machoni pako, naomba wewe na Hamani muhudhurie leo katika karamu niliyoiandaa kwa ajili yake.”
5 Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.” Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta.
Mfalme akasema, “Mleteni haraka Hamani sawa sawa na matakwa ya Malkia Esta.” Mfalme pamoja na Hamani wakahuduria katika karamu aliyoandaa malkia Esta.
6 Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”
Mvinyo ulipohudumiwa katika karamu, mfalme akamuuliza Malkia Esta hitaji lako ni nini? Na ombi lako ni lipi? Utapewa hata nusu ya ufalme.”
7 Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili:
Esta akajibu mfalme, “Hitaji na ombi langu ni hili,
8 Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake na kama ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”
kama ikikupendeza mfalme, kwa kunipa haja yangu na kuheshimu ombi langu, wewe na Hamani muhudhurie tena katika karamu nitakayoiandaa kesho na hapo ndipo nitakapo kuambia haja yangu.
9 Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonyesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai.
Hamani akaenda nyumbani kwakwe huku akiwa amejawa na furaha moyoni mwake. Lakini alipomwona Modekai katika lango la mfalme, modekai hasimami wala kutetemeka mbele zake, alijawa na ghadhabu kwa ajili ya Modekai.
10 Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani. Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe.
Lakini akajizuia na akaenda nyumbani kwake. Akawaarika marafiki zake wakakusanyika pamoja na Zereshi, mkewe.
11 Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine.
Hamani akawaeleza juu ya utukufu wa mali na idadi ya watoto aliokuwa nao, na vile alivyo juu kuliko wasimamizi na watumishi wote wa mfalme.
12 Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho.
Hamani akawambia, “Hata jana Malkia Esta aliandaa karamu kwa ajili ya mfalme na ni mimi tu na mfalme tulio hudhuria katika karamu aliyoiandaa Malkia Esta. Na hata kesho tuna mwaliko mwingine pamoja na mfalme.
13 Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.”
Lakini haya yote sio kitu kama Modekai ataendelea kukaa katika lango la mfalme.
14 Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini, kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.
Kisha Zereshi, mkewe Hamani akamwambia Mmewe na rafiki zake wote, “Andaeni mti wenye urefu wa futi hamsini. Na wakati wa ahsubuhi ongea na mfalme ili Modekai atundikwe katika mti huo. Kisha nenda kwa furaha na mfalme katika karamu aliyoiandaa Malkia.