< Esta 4 >

1 Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini, akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu.
Modeka aliposikia kilichokuwa kimepangwa dhidi yao, alirarua mavazi yake na kuvaa maguni na majivu. Akaenda katikati mwa mji na kulia kwa sauti na uchungu mwingi.
2 Alikwenda akasimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa nguo za magunia.
Akaenda hadi langoni mwa mfalme; kwa sababu hakuna aliye ruhusiwa kuingia akiwa amevaa magunia.
3 Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya nguo za magunia na majivu.
Amri hii ilipofika katika kila jimbo, kulikuwa na kilio kikubwa kwa Wayahudi, na kufunga, kulia na maombolezo. Wengi wao walilala katika magunia na majivu.
4 Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai hakuzikubali.
Malkia Esta alipopata habari kutoka kwa wahudumu wake, alipatwa na majonzi. Akatuma watu wampelekee nguo Modekai ili avue magunia na kuvaa nguo nzuri, lakini Modekai hakukubali.
5 Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmojawapo wa matowashi wa mfalme ambaye alikuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta ni nini kilikuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini.
kisha Esta akamwita Hathaki, mmoja wa wasimamizi wa mfalme, ambaye alikuwa amepewa wajibu wa kumuhudumia. Akamwagiza kwenda kwa Modekai ili afahamu kwa nini Modekai ameamua kufanya hivyo.
6 Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme.
Hivyo Hathaki akaenda kwa Modekai katika mji mbele ya lango la mfalme.
7 Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi.
Modekai akamweleza Hathaki mambo yote kuhusu maangamizi ya Wayahudi yaliyo pangwa na kiasi cha fedha ambacho Hamani ameahidi kuwapa wahazini wa mfalme, ili kuwaua Wayahudi.
8 Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonyesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake.
Na kisha akampa nakala ya mbiu ambayo ilitolewa Shushani kwa uangamivu wa Wayahudi. Alifanya hiivyo ili kwamba Hathaki amwambie Esta achukue jukumu la kwenda na kumuomba mfalme na kumsihi kwa niaba ya Wayahudi.
9 Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai.
Hivyo, Hathaki akaenda na kumweleza Esta kile alicho ambiwa na Modekai.
10 Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai,
Esta akaongea na Hathaki na akamwambia arudi kwa Modekai.
11 “Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.”
Esta akamwambia Hathaki, “Watumishi wote wa mfalme na watu wote katika majimbo yote wanafahamu kuwa mtu yeyote aingiae kwa mfalme bila kibali anapaswa kufa isipokuwa yule ambaye mfalme atamunyoshea fimbo yake ya dhahabu. Ni siku thelathini sasa sijaenda mbele ya mfalme.
12 Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta,
Hathaki akamwambia Modekai maneno aliyoambiwa na Esta.
13 Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona.
Modekai akarudisha ujumbe: “usifikiri kwamba wewe utasalimika kuliko Wayahudi wote.
14 Kwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?”
Kama ukikaa kimya kwa wakati huu, Mungu ataleta wokovu kwa njia nyingine, lakini wewe na nyumba ya baba yako mtaangamia. Ni nani ajuaye umekuja katika nafasi hii kwa wakati muafaka kama huu.
15 Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai:
Kisha Esta akatuma ujumbe kwa Modekai,
16 “Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”
“Nenda, uwakusanyea Wayahudi wote wanaoishi katika mji wa Shushani, na wafunge kwa ajili yangu. Wasile wala kunywa kwa muda wa siku tatu. Mimi na watumishi watumishi wangu wa kike tutafunga kwa siku hizo. Na kisha nitaenda mbele ya mfalme kinyume cha sheria. Na kama nitakufa na nife.
17 Kwa hiyo Mordekai alikwenda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.
Modekai akaenda na akafanya yote ambayo Esta aliyo mwagiza kufanya.

< Esta 4 >