< Esta 2 >
1 Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya na alilokuwa ameamuru juu yake.
2 Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Na ufanyike utafiti kwa ajili ya wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme.
3 Mfalme na ateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya utunzaji wa Hegai, towashi wa mfalme, msimamizi wa wanawake; na wapewe matunzo yote ya urembo.
4 Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata.
5 Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila ya Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi,
6 ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda.
7 Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.
8 Wakati agizo na amri ya mfalme lilitangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake.
9 Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya uzuri na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake.
10 Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wala kabila lake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza.
11 Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.
12 Kabla zamu ya msichana haijafika ya kwenda kwa Mfalme Ahasuero, ilimbidi atimize miezi kumi na miwili ya matunzo ya urembo kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa miezi sita walikuwa wajipake mafuta ya manemane, na miezi sita kujipaka manukato na vipodozi.
13 Basi hivi ndivyo ambavyo msichana angeingia kwa mfalme: Kila kitu alichohitaji aliruhusiwa kuchukua kutoka nyumba ya wanawake na kwenda navyo katika jumba la mfalme.
14 Jioni angekwenda pale na asubuhi kurudi sehemu nyingine ya nyumba ya wanawake katika utunzaji wa Shaashgazi, towashi wa mfalme ambaye alikuwa mkuu wa masuria. Hangeweza kurudi kwa mfalme mpaka apendezwe naye na kuagiza aitwe kwa jina lake.
15 Zamu ya Esta ilipofika kwenda kwa mfalme (msichana ambaye Mordekai alikuwa amemlea, binti wa Abihaili mjomba wake), Esta hakutaka vitu zaidi ya vile ambavyo Hegai, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake alivyokuwa amemshauri. Naye Esta alipata kibali kwa kila mtu aliyemwona.
16 Esta alipelekwa kwa Mfalme Ahasuero katika makao ya mfalme mwezi wa kumi, yaani mwezi wa Tebethi, katika mwaka wake wa saba wa kutawala.
17 Basi ikawa mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti.
18 Mfalme akafanya karamu kubwa, karamu ya Esta, kwa wakuu wake wote na maafisa. Mfalme alitangaza mapumziko katika majimbo yake yote na kugawa zawadi kwa ukarimu wa kifalme.
19 Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme.
20 Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya kabila lake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea.
21 Wakati Mordekai alikuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero.
22 Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai.
23 Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.