< Waefeso 6 >

1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema.
Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema.
2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi,
“Waheshimu Baba na mama yako,” hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani,
3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”
“Upate fanaka na miaka mingi duniani.”
4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.
Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.
5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo.
Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo.
6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo.
Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo.
7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu.
Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu.
8 Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.
Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana.
9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.
Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu.
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.
11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi.
Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.
12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. (aiōn g165)
Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. (aiōn g165)
13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.
Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti.
14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani,
Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,
15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani.
na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu.
16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.
17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu.
Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.
18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.
Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu.
19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri,
Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti.
20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.
Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo.
21 Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya sasa.
Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya.
22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.
Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo.
23 Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo.
Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
24 Neema iwe na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo wa dhati. Amen.
Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.

< Waefeso 6 >