< Waefeso 2 >

1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu,
Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu.
2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. (aiōn g165)
Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu. (aiōn g165)
3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote.
Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.
4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema,
Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,
5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema.
hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa.
6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu,
Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.
7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. (aiōn g165)
Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu. (aiōn g165)
8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu,
Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.
9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.
Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.
10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.
11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu),
Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine—mnaoitwa, “wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) —kumbukeni mlivyokuwa zamani.
12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi mkiwa hamna tumaini wala Mungu duniani.
Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani.
13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.
Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.
14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu,
Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui.
15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani,
Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.
16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao.
Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu.
17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu.
Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.
18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja.
19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu.
Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu.
20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.
Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi.
21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana.
Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana.
22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.
Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

< Waefeso 2 >