< Mhubiri 9 >
1 Kwa hiyo niliyatafakari yote haya nikafikia uamuzi kwamba waadilifu na wenye hekima na yale wanayoyafanya yako mikononi mwa Mungu, lakini hakuna mtu ajuaye kama anangojewa na upendo au chuki.
2 Wote wanayo hatima inayofanana, mwadilifu na mwovu, mwema na mbaya, aliye safi na aliye najisi, wale wanaotoa dhabihu na wale wasiotoa. Kama ilivyo kwa mtu mwema, ndivyo ilivyo kwa mtu mwenye dhambi; kama ilivyo kwa wale wanaoapa, ndivyo ilivyo kwa wale wasioapa.
3 Huu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa.
4 Yeyote aliye miongoni mwa walio hai analo tumaini, hata mbwa hai ni bora kuliko simba aliyekufa!
5 Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa, lakini wafu hawajui chochote, hawana tuzo zaidi, hata kumbukumbu yao imesahaulika.
6 Upendo wao, chuki yao na wivu wao vimetoweka tangu kitambo, kamwe hawatakuwa tena na sehemu katika lolote linalotendeka chini ya jua.
7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya.
8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta.
9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua.
10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima. (Sheol )
11 Nimeona kitu kingine tena chini ya jua: Si wenye mbio washindao mashindano au wenye nguvu washindao vita, wala si wenye hekima wapatao chakula au wenye akili nyingi wapatao mali, wala wenye elimu wapatao upendeleo, lakini fursa huwapata wote.
12 Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja: Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili, au ndege wanaswavyo kwenye mtego, vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya zinazowaangukia bila kutazamia.
13 Pia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana:
14 Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzunguka akaweka jeshi kubwa dhidi yake.
15 Katika mji huo kulikuwepo mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini.
16 Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake.
17 Maneno ya utulivu ya mwenye hekima husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu.
18 Hekima ni bora kuliko silaha za vita, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mema mengi.