< Mhubiri 2 >

1 Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili.
Nikasema moyoni, “Njoo, na nitakujaribu kwa kwa furaha. Kwa hiyo furahia.” Lakini tazama, huu nao ulikuwa ni upepo wa muda.
2 Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?”
Nikasema juu ya kicheko, “Ni wazimu,” na kuhusu furaha, “Yafaa nini?”
3 Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu.
Nikajipeleleza moyoni mwangu katika jinsi ya kutimiza hamu yangu kwa mvinyo. Nikaruhusu akili yangu iongozwe na hekima ingawa bado nilikuwa nikishikilia ujinga. Nilitaka kutafuta jambo lililo jema kwa wanadamu kufanya chini ya mbingu wakati wa siku za maisha yao.
4 Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu.
Nilitimiza mambo makubwa. Nilijenga nyumba kwa ajili yangu na kupanda miti ya mizabibu.
5 Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda.
Nilitengeneza bustani na viwanja; nikapanda aina zote za matunda ndani yake.
6 Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri.
Nikatengeneza mabwawa ya maji ili kumwagilia msitu mahali miti ilikuwa imepandwa.
7 Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu.
Nilinunua watumwa wa kiume na wa kiume; nilikuwa na watumwa waliozaliwa katika ikulu yangu. Pia nikawa na makundi makubwa na wanyama wa kufugwa, zaidi ya mfalme yeyote aliyetawala kabla yangu katika Yerusalemu.
8 Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia.
Pia nilijikusanyia fedha na dhahabu, hazina ya wafalme na majimbo. Nikapata waimbaji wanaume na wanawake kwa ajili yangu, na kufurahia kutoka kwa wana wa wanadamu, masulia na wanawake.
9 Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima.
Hivyo nikawa mkuu na tajiri kuliko wote waliokuwa Yerusalemu kabla yangu, na hekima yangu ilikuwa ndani yangu.
10 Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote.
Lolote ambalo macho yangu yalikitamani sikuyazuia. Sikuuzuia moyo wangu katika furaha yeyote, kwa sababu moyo wangu ulifurahi katika katka kazi yangu zote na furaha ilikuwa ni tunu kwa kazi zangu zote.
11 Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.
Kisha nikatazama matendo yote ambayo mikono yangu iliyokwisha kuyatimiliza na juu ya kazi niliyokuwa nimeifanya, lakini tena, kila kitu kilikuwa ni mvuke na kujaribu kuuchunga upepo. Hakukuwa na faida chini ya jua.
12 Kisha nikageuza mawazo yangu kufikiria hekima, wazimu na upumbavu. Ni nini zaidi mtu anayetawala baada ya mfalme anachoweza kufanya ambacho hakijafanywa?
Kisha nikageuka kuipambanua hekima, na upumbavu na ujinga. Kwa maana ni kitu gani mfalme anayekuja baada yangu afanye, ambacho hakijafanyika?
13 Nikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu, kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza.
Kisha nikaanza kuelewa kwamba hekima ina faida kuliko upumbavu, kama nuru ilivyo bora kuliko giza.
14 Mtu mwenye hekima ana macho katika kichwa chake, lakini mpumbavu anatembea gizani; lakini nikaja kuona kwamba wote wawili hatima yao inafanana.
Mwenye hekima hutumia macho yake katika kichwa chake kuona mahali anakoenda, lakini mpumbavu hutembea katika giza, ingawa ninafahamu kuwa mwisho wa aina moja umetunzwa kwa kila mmoja.
15 Kisha nikafikiri moyoni mwangu, “Hatima ya mpumbavu itanipata mimi pia. Nitafaidi nini basi kwa kuwa na hekima?” Nikasema moyoni mwangu, “Hili nalo ni ubatili.”
Kisha nikasema moyoni mwangu, “Kinachotokea kwa mpumbavu, ndicho kitachotokea na kwangu. Hivyo kuna utofauti gani kama mimi ni mwenye hekima sana?” Nikahitimisha moyoni mwangu, “Huu pia ni mvuke tu.”
16 Kwa maana kwa mtu mwenye hekima, kama ilivyo kwa mpumbavu, hatakumbukwa kwa muda mrefu, katika siku zijazo wote watasahaulika. Kama vile ilivyo kwa mpumbavu, mtu mwenye hekima pia lazima atakufa!
Kwa kuwa mwenye hekima, kama mpumbavu, hakumbukwi kwa muda mrefu. Katika siku zijazo, kila kitu kitakuwa kimesahauliwa. Mwenye hekima hufa kama navyokufa mpumbavu.
17 Kwa hiyo nikachukia maisha, kwa sababu kazi inayofanyika chini ya jua ilikuwa masikitiko kwangu. Yote hayo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Hivyo nikauchukia uhai kwa sababu kazi zote zilizofanyika chini ya jua zilikuwa mbaya kwangu. Hii ni kwa sababu kila kitu ni mvuke na kujaribu kuuchunga upepo.
18 Nikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu.
Nikachukia yote niliyoyatimiza, ambayo nilikuwa nimekwisha yafanya chini ya jua kwa sababu ni lazima niyaache kwa mtu anaye kuja baada yangu.
19 Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili.
Na ni nani ajuaye kama atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Ila atakuwa msimamizi juu ya kila kitu chini ya jua ambayo kazi yangu na hekima yangu imeyajenga. Huu pia ni mvuke.
20 Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua.
Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi zote nilizozifanya chini ya jua.
21 Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa.
Kwa kuwa kunaweza kuwa na mtu anayefanya kazi kwa hekima, ufahamu, na umahili, lakini ataacha kila kitu alichonacho kwa mtu ambaye hajafanya chochote. Huu nao ni mvuke na hatari kubwa.
22 Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua?
Kwa maana ni faida gani mtu hupata ambaye hufanya kazi kwa juhudi na kujaribu moyoni mwake kutimiza kazi zake chini ya jua?
23 Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.
Kila siku kazi yake ni maumivu na masikitiko, hivyo wakati wa usiku roho yake haipumziki. Huu pia ni mvuke.
24 Hakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu,
Hakuna jambo jema kwa mtu yeyote zaidi ya kula na kunywa na kuridhika na kile kilichochema katika kazi yake. Nikaona kwamba ukweli huu unatoka kutoka mkononi mwa Mungu.
25 kwa sababu pasipo yeye, ni nani awezaye kula na kufurahi?
Kwa kuwa ni nani anaweza kula au anaweza kupata furaha yoyote tofauti na Mungu?
26 Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Kwa kuwa kwa kila anayemfurahisha yeye, Mungu humpa hekimana ufahamu ba furaha. Ingawa, kwa mwenye dhambi humpa kazi ya kukusanya na kutunza ili kwamba ampe mtu anayempendeza Mungu. Huu pia ni sawa na mvuke na kujaribu kuuchunga upepo.

< Mhubiri 2 >