< Mhubiri 11 >
1 Tupa mkate wako juu ya maji, kwa maana baada ya siku nyingi utaupata tena.
Peleka mkate wako juu ya maji, kwa kuwa utaupata tena baada ya siku nyingi.
2 Wape sehemu watu saba, naam hata wanane, kwa maana hujui ni baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
Shiriki mkate na watu saba, hata wanane kwa kuwa haujui ni majanga gani yanayo kuja juu ya nchi.
3 Kama mawingu yamejaa maji, hunyesha mvua juu ya nchi. Kama mti ukianguka kuelekea kusini au kuelekea kaskazini, mahali ulipoangukia, hapo ndipo utakapolala.
Kama mawingu yamejaa mvua, yanajivua yenyewe chini ya nchi. Na kama mti ukianguka kuelekea kusini au kuelekea kaskazini, popote mti unapoangukia papo hapo utabakia.
4 Yeyote atazamaye upepo hatapanda, yeyote aangaliaye mawingu hatavuna.
Yeyote autazamaye upepo yawezekana asipande, na yeyote atazamaye mawingu yawezekana asivune.
5 Kama vile usivyofahamu njia ya upepo, au jinsi mwili uumbwavyo ndani ya tumbo la mama, vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu, Muumba wa vitu vyote.
Kama usivyo jua njia ya upepo, wala vile ambavyo mtoto akuavyo tumboni, vivyo hivyo huwezi kuielewa kazi ya Mungu, aliye umba kila kitu.
6 Panda mbegu yako asubuhi, nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee, kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa, kwamba ni hii au ni ile, au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.
Asubuhi panda mbegu yako; hadi jioni, fanya kazi kwa mikono yako kama inavyo hitajika kwa kuwa haujui ni ipi itafanikiwa, jioni au asubuhi, au hii au ile au zote zitakuwa nzuri.
7 Nuru ni tamu, tena inafurahisha macho kuona jua.
Kweli nuru ni tamu, na ni kitu cha kufurahisha kwa ajili ya macho kuona jua.
8 Hata kama mtu ataishi miaka mingi kiasi gani, na aifurahie yote. Lakini na akumbuke siku za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.
Kama mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote, lakina na afikiri juu ya siku zijazo za giza, kwa kuwa zitakuwa nyingi. Kila kitu kijacho ni mvuke unaoteketea.
9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana, moyo wako na ukupe furaha katika siku za ujana wako. Fuata njia za moyo wako na chochote macho yako yaonayo, lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote Mungu atakuleta hukumuni.
Furahia kijana, katika ujana wako, na moyo wako ufurahie siku za ujana wako. fuatilia yale mema ya moyo wako, chochote kilicho mbele ya macho yako. Ingawa, fahamu kwamba MUngu atakuleta hukumuni kwa ajili ya vitu hivi vyote.
10 Kwa hiyo basi, ondoa wasiwasi moyoni mwako na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako, kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.
Ondoa hasira kutoka moyoni mwako, na usijali maumivu yoyote katika mwili wako, kwa sababu ujana na nguvu zake ni mvuke.