< Torati 34 >

1 Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani,
Musa aliondoka kutoka nyanda za Moabu mpaka mlima wa Nebo, hadi kilele cha Pisga, kilicho mkabala na Yericho. Huko Yahwe alimwonyesha nchi yote ya Gileadi kutoka umbali wa Dani,
2 Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,
na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi,
3 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari.
na Negevi, na uwanda wa bonde la Yericho, mji wa mitende, mpaka umbali wa Soari.
4 Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
Yahwe alimwambia, “Hii ni nchi niliyoapa kwa Abrahamu, kwa Isaka, na kwa Yakobo, na kusema, “Nitawapatia uzao wako.” Nimekuruhusu uitazame kwa macho yako, lakini hautakwenda kule.”
5 Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema.
Basi Musa mtumishi wa Yahwe, alikufa pale katika nchi ya Moabu, kama neno la Yahwe lilivyoahidi.
6 Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo.
Yahwe alimzika katika bonde katika nchi ya Moabu mkabala na Beth-peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo hadi leo hii.
7 Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika.
Musa alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipokufa; macho yake hayakufifia, wala nguvu asili zake hazikupungua.
8 Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
Watu wa Israeli walimuomboleza Musa katika nyanda za Moabu kwa siku thelathini, hapo ndipo siku za maombolezo ya Musa zilipotimia.
9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.
Yoshua mwana wa Nuni alikuwa amejawa na roho ya hekima, kwa maana Musa alimwekea mkono juu yake. Watu wa Israeli walimsikiliza na kufanya yale ambayo Yahwe alimuamuru Musa.
10 Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso,
Tangu hapo hakujatokea nabii katika Israeli kama Musa, ambaye Yahwe alimjua uso kwa uso.
11 aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote.
Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa ishara na miujiza ambayo Yahwe alimtuma kufanya katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake, na kwa nchi yake yote.
12 Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.
Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa mambo yote makubwa, ya kutisha ambayo Musa aliyafanya machoni pa Israeli yote.

< Torati 34 >