< Torati 33 >
1 Hii ndiyo baraka Mose mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake.
2 Alisema: “Bwana alikuja kutoka Mlima Sinai, akachomoza kama jua juu yao kutoka Mlima Seiri, akaangaza kutoka Mlima Parani. Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu kutoka kusini, kutoka materemko ya mlima wake.
3 Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu, watakatifu wako wote wamo mkononi mwako. Miguuni pako wote wanasujudu na kutoka kwako wanapokea mafundisho,
4 sheria ile Mose aliyotupa sisi, tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.
5 Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni wakati viongozi wa watu walipokusanyika, pamoja na makabila ya Israeli.
6 “Reubeni na aishi, asife, wala watu wake wasiwe wachache.”
7 Akasema hili kuhusu Yuda: “Ee Bwana, sikia kilio cha Yuda, mlete kwa watu wake. Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea. Naam, uwe msaada wake dhidi ya adui zake!”
8 Kuhusu Lawi alisema: “Thumimu yako na Urimu yako ulimpa, mtu yule uliyemfadhili. Ulimjaribu huko Masa na kushindana naye kwenye maji ya Meriba.
9 Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake, ‘Mimi siwahitaji kamwe.’ Akawasahau jamaa zake, asiwatambue hata watoto wake, lakini akaliangalia neno lako na kulilinda Agano lako.
10 Humfundisha Yakobo mausia yako na Israeli sheria yako. Hufukiza uvumba mbele zako na sadaka nzima za kuteketezwa juu ya madhabahu yako.
11 Ee Bwana, bariki ustadi wake wote, nawe upendezwe na kazi ya mikono yake. Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake; wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
12 Kuhusu Benyamini akasema: “Mwache mpenzi wa Bwana apumzike salama kwake, kwa maana humkinga mchana kutwa, na yule Bwana ampendaye hupumzika kati ya mabega yake.”
13 Kuhusu Yosefu akasema: “Bwana na aibariki nchi yake kwa umande wa thamani kutoka mbinguni juu, na vilindi vya maji vilivyotulia chini;
14 pamoja na vitu vilivyo bora sana viletwavyo na jua, na vitu vizuri sana vinavyoweza kutolewa na mwezi;
15 pamoja na zawadi bora sana za milima ya zamani na kwa wingi wa baraka za vilima vya milele;
16 pamoja na baraka nzuri mno za ardhi na ukamilifu wake, na upendeleo wake yeye aliyeishi kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu, juu ya paji la uso la aliye mkuu miongoni mwa ndugu zake.
17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza; pembe zake ni pembe za nyati, na kwa pembe hizo atapiga mataifa, hata yaliyo miisho ya dunia. Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu; hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”
18 Kuhusu Zabuloni akasema: “Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje, nawe Isakari, katika mahema yako.
19 Watawaita mataifa kwenye mlima, na huko mtatoa dhabihu za haki; watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari, kwa hazina zilizofichwa mchangani.”
20 Kuhusu Gadi akasema: “Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi! Gadi huishi huko kama simba, akirarua kwenye mkono au kichwa.
21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote kwa ajili yake mwenyewe; fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa kwa ajili yake. Viongozi wa watu walipokusanyika, alitimiza haki ya mapenzi ya Bwana, na hukumu zake kuhusu Israeli.”
22 Kuhusu Dani akasema: “Dani ni mwana simba, akiruka kutoka Bashani.”
23 Kuhusu Naftali akasema: “Naftali amejaa tele upendeleo wa Bwana, naye amejaa baraka yake; atarithi magharibi na kusini.”
24 Kuhusu Asheri akasema: “Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri; yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake, yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba, nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni, ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie, na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27 Mungu wa milele ni kimbilio lako, na chini kuna mikono ya milele. Atamfukuza adui yako mbele yako, akisema, ‘Mwangamize yeye!’
28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake. Mzao wa Yakobo ni salama katika nchi ya nafaka na divai mpya, mahali ambapo mbingu hudondosha umande.
29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa! Ni nani kama wewe, taifa lililookolewa na Bwana? Yeye ni ngao yako na msaada wako, na upanga wako uliotukuka. Adui zako watatetemeka mbele yako, nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.”