< Torati 32 >

1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema; sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.
Tega sikio, enyi mbingu, na niruhusu kuzungumza.
2 Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua, na maneno yangu na yashuke kama umande, kama manyunyu juu ya majani mabichi, kama mvua tele juu ya mimea myororo.
Acha dunia isikie maneno ya kinywa changu. Acha mafundisho yangu yamwagike chini kama mvua, acha usemi wangu udondoke kama umande, kama mvua tulivu juu ya majani laini, na kama mvua za manyunyu juu ya mimea.
3 Nitalitangaza jina la Bwana. Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!
Kwa maana nitatangaza jina la Yahwe, na kumpatia ukuu Mungu wetu.
4 Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni haki. Mungu mwaminifu ambaye hakosei, yeye ni mnyofu na mwenye haki.
Mwamba, kazi yake ni kamili; kwa maana njia zake ni za haki. Yeye ni Mungu mwaminifu, hana udhalimu. Yeye ni wa haki na mwadilifu.
5 Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake; kwa aibu yao, wao si watoto wake tena, lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.
Wamefanya yaliyo maovu dhidi yake. Wao sio watoto wake. Ni aibu kwao. Wao ni kizazi kiovu na kilichopindika.
6 Je, hii ndiyo njia ya kumlipa Bwana, enyi watu wajinga na wasio na busara? Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu, aliyewafanya ninyi na kuwaumba?
Je! Unamzawadia Yahwe kwa njia hii, enyi watu wapumbavu na msiojitambua? Je! yeye si baba yenu, yule ambaye aliwaumba? Aliwaumba na kuwaimarisha.
7 Kumbuka siku za kale; tafakari vizazi vya zamani vilivyopita. Uliza baba yako, naye atakuambia, wazee wako, nao watakueleza.
Kumbukeni siku zile za zamani, tafakari juu ya miaka mingi ya nyuma. Muulize baba yako naye atakuonyesha, wazee wako nao watakuambia.
8 Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao, alipogawanya wanadamu wote, aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.
Pale ambapo Aliye Juu alipowapatia mataifa urithi wao – alipowagawa wanadamu wote, na kuweka mipaka ya watu, na alipoimarisha idadi ya miungu yao.
9 Kwa kuwa fungu la Bwana ni watu wake, Yakobo kura yake ya urithi.
Kwa maana fungu la Yahwe ni watu wake; Yakobo ni mgao wa urithi wake.
10 Katika nchi ya jangwa alimkuta, katika nyika tupu ivumayo upepo. Alimhifadhi na kumtunza; akamlinda kama mboni ya jicho lake,
Alimpata katika nchi ya jangwa, na katika jangwa kame na livumalo upepo; alimkinga na kumtunza, alimlinda kama mboni ya jicho lake.
11 kama tai avurugaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka, na huwachukua kwenye mabawa yake.
Kama tai akichungaye kiota chake na kupiga piga mabawa juu ya makinda yake, Yahwe alitandaza mabawa yake na kuwachukua, na kuwabeba kwenye mapapatio yake.
12 Bwana peke yake alimwongoza; hakuwepo mungu mgeni pamoja naye.
Yahwe pekee alimuongoza, hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.
13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi, akamlisha kwa mavuno ya mashamba. Akamlea kwa asali toka mwambani, na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu,
Alimfanya aendeshe katika maeneo ya juu ya nchi, na alimlisha matunda ya mbugani; alimrutubisha kwa asali kutoka kwenye jiwe, na mafuta kutoka kwenye mwamba mgumu sana.
14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe na kutoka makundi ya mbuzi, kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi, kwa kondoo dume wazuri wa Bashani, na kwa ngano nzuri. Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.
Alikula siagi kutoka katika kundi na kunywa maziwa kutoka katika kundi la mifugo, pamoja na mafuta ya wanakondoo, kondoo dume wa Bashani na mbuzi, pamoja na ngano safi kabisa – nawe ulikunywa divai itokayo povu iliyotengenezwa kwa juisi ya mizabibu.
15 Yeshuruni alinenepa na kupiga teke; alikuwa na chakula tele, akawa mzito na akapendeza sana. Akamwacha Mungu aliyemuumba, na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.
Lakini Yeshuruni akakua kwa unene na kupiga mateke – ulikua kwa unene, ulikua mnene sana, na ulikuwa umekula ujazo wako – alimuacha Mungu aliyemuumba, na kukataa Mwamba wa wokovu wake.
16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo.
Walimfanya Yahwe apatwe wivu kwa miungu yao ya ajabu; kwa maudhi yao walimkasirisha.
17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
Walitoa dhabihu kwa mapepo, ambayo sio Mungu – miungu ambayo hawajaijua, miungu ambayo imejitokeza hivi karibuni, miungu ambayo mababu zenu hawakuogopa.
18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa.
Umetelekeza Mwamba, ambao ulikuwa baba yako, na ukasahau Mungu aliyekuzaa.
19 Bwana akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe na binti zake.
Yahwe aliliona hili na kuwakataa, kwa sababu watoto wake wa kiume na mabinti zake walimchokoza.
20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu.
“Nitaficha uso wangu kwao”, alisema, “nami nitaona mwisho wao utakuaje; maana wao ni kazazi kaidi, watoto ambao sio waaminifu.
21 Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao zisizokuwa na thamani. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu.
Wamenifanya kuwa na wivu kwa kile ambacho sio mungu na kunikasirisha kwa mambo yao yasiyo na maana. Nitawafanya waone wivu kwa wale ambao sio taifa; nitawakasirisha kwa taifa pumbavu.
22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima. (Sheol h7585)
Kwa maana moto kuwashwa kwa hasira yangu na inawaka hadi chini mwa Sheoli; inameza ulimwengu na mavuno yake; inawasha moto misingi ya milima. (Sheol h7585)
23 “Nitalundika majanga juu yao na kutumia mishale yangu dhidi yao.
Nitarundia maafa juu yao; nitafyatua mishale yangu yote kwao;
24 Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya, yateketezayo na tauni ya kufisha; nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu, na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini.
Watapotea kwa njaa na kumezwa kwa joto liwakalo na uharibifu mchungu; nitatuma kwao meno ya wanyama wa mwituni, pamoja na sumu ya vitu vitambaao mavumbini.
25 Barabarani upanga utawakosesha watoto; nyumbani mwao hofu itatawala. Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia, pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
Nje panga litawatwaa, na ndani ya vyumba hofu kuu itafanya hivyo. Wote mwanamume kijana na bikra nitawaangamiza, mchanga anyonyaye, na mwanamume mwenye mvi.
26 Nilisema ningewatawanya na kufuta kumbukumbu lao katika mwanadamu.
Nilisema nitawasambaza mbali, kwamba nitafanya kumbukumbu yao kukoma miongoni mwa wanadamu.
27 Lakini nilihofia dhihaka za adui, adui asije akashindwa kuelewa, na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda; Bwana hakufanya yote haya.’”
Isingekuwa kwamba naogopa uchokozi wa adui, na kwamba adui zake wangehukumu kimakosa, na kwamba wangesema, “Mkono wetu umeinuliwa,” ningefanya haya yote.
28 Wao ni taifa lisilo na akili, hakuna busara ndani yao.
Kwa maana Israeli ni taifa linalopungukiwa na hekima, na hakuna ufahamu ndani mwao.
29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili, na kutambua mwisho wao utakuwa aje!
Ah laiti wangekuwa na hekima, wangeelewa hili, na kuzingatia ujio wa hatima yao!
30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja, au wawili kufukuza elfu kumi, kama si kwamba Mwamba wao amewauza, kama si kwamba Bwana amewaacha?
Inawezekanaje mmoja kufukuza maelfu, na wawili kuweka makumi elfu mbioni, isipokuwa Mwamba wao hajawauza, na Yahwe hajawaachilia kwao?
31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu, sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
Kwa maana mwamba wa maadui zetu si kama Mwamba wetu, kama vile maadui zetu wanavyokiri.
32 Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma, na kutoka kwenye mashamba ya Gomora. Zabibu zake zimejaa sumu, na vishada vyake vimejaa uchungu.
Kwa maana mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma, na kwenye mashamba ya Gomorra; na zabibu zake ni zabibu za sumu; vishada vyao ni vichungu.
33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka, sumu yenye kufisha ya swila.
Mvinyo yao ni sumu ya nyoka na sumu katili ya nyoka.
34 “Je, hili sikuliweka akiba na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
Huu mpango haujafichwa kwangu kwa siri, na kufungwa kabisa katika hazina zangu?
35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza. Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza; siku yao ya maafa ni karibu, na maangamizo yao yanawajia haraka.”
Kisasi ni changu kutoa, na fidia, katika muda mguu wao utakapotereza; kwa maana siku ya maafa kwao ipo karibu, na vitu vitakavyokuja juu yao vitaharakisha kutendeka.
36 Bwana atawahukumu watu wake, na kuwahurumia watumishi wake atakapoona nguvu zao zimekwisha wala hakuna yeyote aliyebaki, mtumwa au aliye huru.
Kwa maana Yahwe atatoa haki kwa watu wake, na atawahurumia watumishi wake. Atahakikisha kuwa nguvu yao imetoweka, na hakuna atakayesalia, iwe watumwa au watu huru.
37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao, mwamba walioukimbilia,
Kisha atasema, “wako wapi miungu yao, mwamba ambao wamekimbilia? –
38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji? Wainuke basi, wawasaidie! Wawapeni basi ulinzi!
miungu iliyokula sadaka zao nene na kunywa mvinyo wa sadaka zao za kinywaji? Na wainuke na kukusaidia; na wawe ulinzi kwako.
39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye! Hakuna mungu mwingine ila Mimi. Mimi ninaua na Mimi ninafufua, Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya, wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
Tazama sasa mimi, hata mimi, ni Mungu, na kwamba hakuna mungu tofauti yangu; ninaua, na ninaleta uhai; ninajeruhi, na ninaponya, na hakuna mtu atakayekuokoa kutoka kwa uwezo wangu.
40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema: Hakika kama niishivyo milele,
Kwa maana ninainua mikono yangu mbinguni na kusema, “Niishivyo milele, nitatenda.
41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu, nitalipiza kisasi juu ya adui zangu na kuwalipiza wale wanaonichukia.
Nitakapong’oa panga langu lingaaro, na mkono wangu utakapoanza kuleta haki, nitalipiza kisasi juu ya maadui zangu, na kuwalipa wale wote wanichukiao.
42 Nitailevya mishale yangu kwa damu, wakati upanga wangu ukitafuna nyama: damu ya waliochinjwa pamoja na mateka, vichwa vya viongozi wa adui.”
Nitafanya mishale yangu kulewa na damu, na panga langu litameza nyama kwa damu ya waliouawa na mateka, na kutoka kwa vichwa vya viongozi wa adui.”
43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake, kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake, atalipiza kisasi juu ya adui zake na kufanya upatanisho kwa ajili ya nchi na watu wake.
Furahi, enyi mataifa, na watu wa Mungu, kwa maana atalipiza kisasi damu ya watumishi wake; atalipiza kisasi juu ya maadui zake, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nchi yake, kwa watu wake.
44 Mose na Yoshua mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.
Musa alikuja na kunena maneno yote ya wimbo huu masikioni mwa watu, yeye na Yoshua mwana wa Nuni.
45 Mose alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote,
Kisha Musa alimaliza kunena maneno haya yote kwa Israeli yote.
46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili kwamba mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii.
Aliwaambia, “Imarisheni akili yenu kwa haya maneno ambayo nimewashuhudia kwenu leo, ili kwamba muwaamuru watoto wenu kuyashika, maneno yote ya sheria hii.
47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
Kwa maana hili si jambo dogo kwako, kwa sababu ni uzima wako, na kupitia jambo hili utarefusha siku zako katika nchi ambayo unakwenda juu ya Yordani kumiliki.”
48 Siku hiyo hiyo Bwana akamwambia Mose,
Yahwe alizungumza na Musa katika siku hiyo hiyo na kusema,
49 “Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe.
“Nenda katika usawa huu wa milima wa Abarimu, juu ya mlima wa Nebo, ambao upo katika nchi ya Moabu, mkabala na Yeriko. Utatazama nchi ya Kanani, ambayo ninawapatia watu wa Israeli kama miliki yao.
50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake.
Utakufa katika mlima utakaopanda, na utakusanywa kwa watu wako, kama Haruni Muisraeli mwenzako alivyokufa juu ya mlima wa Hori na kukusanywa kwa watu wake. Hii
51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli.
itatendeka kwa sababu haukuwa mwaminifu kwangu miongoni mwa watu wa Israeli katika maji ya Meriba kule Kadeshi, katika jangwa la Zini; kwa sababu haukunitendea utukufu na heshima miongoni mwa watu wa Israeli.
52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”
Kwa maana utaona nchi mbele yako, lakini hautakwenda kule, katika nchi ninayowapatia watu wa Israeli.”

< Torati 32 >