< Torati 32 >
1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema; sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.
2 Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua, na maneno yangu na yashuke kama umande, kama manyunyu juu ya majani mabichi, kama mvua tele juu ya mimea myororo.
3 Nitalitangaza jina la Bwana. Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!
4 Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni haki. Mungu mwaminifu ambaye hakosei, yeye ni mnyofu na mwenye haki.
5 Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake; kwa aibu yao, wao si watoto wake tena, lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.
6 Je, hii ndiyo njia ya kumlipa Bwana, enyi watu wajinga na wasio na busara? Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu, aliyewafanya ninyi na kuwaumba?
7 Kumbuka siku za kale; tafakari vizazi vya zamani vilivyopita. Uliza baba yako, naye atakuambia, wazee wako, nao watakueleza.
8 Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao, alipogawanya wanadamu wote, aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.
9 Kwa kuwa fungu la Bwana ni watu wake, Yakobo kura yake ya urithi.
10 Katika nchi ya jangwa alimkuta, katika nyika tupu ivumayo upepo. Alimhifadhi na kumtunza; akamlinda kama mboni ya jicho lake,
11 kama tai avurugaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka, na huwachukua kwenye mabawa yake.
12 Bwana peke yake alimwongoza; hakuwepo mungu mgeni pamoja naye.
13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi, akamlisha kwa mavuno ya mashamba. Akamlea kwa asali toka mwambani, na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu,
14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe na kutoka makundi ya mbuzi, kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi, kwa kondoo dume wazuri wa Bashani, na kwa ngano nzuri. Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.
15 Yeshuruni alinenepa na kupiga teke; alikuwa na chakula tele, akawa mzito na akapendeza sana. Akamwacha Mungu aliyemuumba, na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.
16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo.
17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa.
19 Bwana akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe na binti zake.
20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu.
21 Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao zisizokuwa na thamani. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu.
22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima. (Sheol )
23 “Nitalundika majanga juu yao na kutumia mishale yangu dhidi yao.
24 Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya, yateketezayo na tauni ya kufisha; nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu, na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini.
25 Barabarani upanga utawakosesha watoto; nyumbani mwao hofu itatawala. Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia, pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
26 Nilisema ningewatawanya na kufuta kumbukumbu lao katika mwanadamu.
27 Lakini nilihofia dhihaka za adui, adui asije akashindwa kuelewa, na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda; Bwana hakufanya yote haya.’”
28 Wao ni taifa lisilo na akili, hakuna busara ndani yao.
29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili, na kutambua mwisho wao utakuwa aje!
30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja, au wawili kufukuza elfu kumi, kama si kwamba Mwamba wao amewauza, kama si kwamba Bwana amewaacha?
31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu, sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
32 Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma, na kutoka kwenye mashamba ya Gomora. Zabibu zake zimejaa sumu, na vishada vyake vimejaa uchungu.
33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka, sumu yenye kufisha ya swila.
34 “Je, hili sikuliweka akiba na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza. Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza; siku yao ya maafa ni karibu, na maangamizo yao yanawajia haraka.”
36 Bwana atawahukumu watu wake, na kuwahurumia watumishi wake atakapoona nguvu zao zimekwisha wala hakuna yeyote aliyebaki, mtumwa au aliye huru.
37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao, mwamba walioukimbilia,
38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji? Wainuke basi, wawasaidie! Wawapeni basi ulinzi!
39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye! Hakuna mungu mwingine ila Mimi. Mimi ninaua na Mimi ninafufua, Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya, wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema: Hakika kama niishivyo milele,
41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu, nitalipiza kisasi juu ya adui zangu na kuwalipiza wale wanaonichukia.
42 Nitailevya mishale yangu kwa damu, wakati upanga wangu ukitafuna nyama: damu ya waliochinjwa pamoja na mateka, vichwa vya viongozi wa adui.”
43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake, kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake, atalipiza kisasi juu ya adui zake na kufanya upatanisho kwa ajili ya nchi na watu wake.
44 Mose na Yoshua mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.
45 Mose alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote,
46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili kwamba mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii.
47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
48 Siku hiyo hiyo Bwana akamwambia Mose,
49 “Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe.
50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake.
51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli.
52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”