< Torati 30 >

1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Bwana Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa,
Vitu hivi vitakavyokuja juu yako, baraka na laana nilizoziweka mbele yako, na utakapozirejea akilini miongoni mwa mataifa mengine ambapo Yahwe Mungu wako kawapeleka,
2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Bwana Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo,
na utakapomrudia Yahwe Mungu wako na kutii sauti yake, na kufuata yote ambayo nayokuamuru leo – wewe na watoto wako – kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote,
3 ndipo Bwana Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya.
kisha Yahwe Mungu wako atageuza kutekwa kwako na kukuhurumia; atawarudisha na kuwakusanya kutoka kwa watu wote ambapo Yahwe Mungu wako aliwatawanya.
4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Bwana Mungu wako atakukusanya na kukurudisha.
Iwapo yeyote ya watu walio uhamishoni wapo katika sehemu za mbali sana chini ya mbingu, kutoka huko Yawhe Mungu wako atawakusanya, na kutoka huko atawarejesha.
5 Yeye Bwana atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako.
Yahwe Mungu wako atawaleta katika nchi ambayo mababu zenu walimiliki, nanyi mtaimiliki tena; atawatendea mema na kuwazidisha zaidi ya alivyofanya kwa mababu zenu.
6 Bwana Mungu wako ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi.
Yahwe Mungu wako atatahiri moyo wako na moyo wa uzao wako, ili umpende Yahwe Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote, ili kwamba uweze kuishi.
7 Bwana Mungu wako ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa.
Yahwe Mungu wako ataweka laana hizi zote kwa maadui zako na kwa wote wakuchukiayo, wale waliokutesa.
8 Utamtii tena Bwana na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo.
Utarudi na kutii sauti ya Yahwe, nawe utatenda amri zake zote ambazo ninakuamuru leo.
9 Ndipo Bwana Mungu wako atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako. Bwana atakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako,
Yahwe Mungu wako atakufanikisha katika kazi yote ya mkono wako, katika matunda ya mwili wako, katika matunda ya mifugo yako, na katika matunda ya nchi yako, kwa mafanikio; kwa maana Yahwe atafurahia tena mafanikio yako, kama alivyofurahia kwa baba zako.
10 kama ukimtii Bwana Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Sheria, na kumgeukia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
Atafanya hivi iwapo utatii sauti ya Yahwe Mungu wako, ili kuzishika amri zake na kanuni zake zilizoandikwa katika kitabu hiki cha sheria, iwapo utamgeukia Yahwe Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote.
11 Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza.
Kwa maana amri hii nayokuamuru leo sio ngumu sana, wala haipo nje ya uwezo wako kufikia.
12 Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?”
Haipo mbinguni, ili usije ukasema, “Nani atayekwenda kwa ajili yetu mbinguni na kutuletea kwetu na kutufanya tuisikie, ili tuweze kutekeleza?”
13 Wala hakiko ngʼambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?”
Wala haipo ng’ambo ya bahari, ili usije ukasema, “Nani atakwenda ng’ambo ya pili ya bahari kwa ajili yetu na kutuletea kwetu na kutufanya tuisikie, ili tuweze kuifanya?”.
14 La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.
Lakini neno lipo karibu sana kwako, katika kinywa chako na moyo wako, ili uweze kutekeleza.
15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo.
Tazama, leo nimeweka mbele yako uzima na wema, mauti na uovu.
16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Bwana Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.
Iwapo utatii maagizo ya Yahwe Mungu wako, ambayo ninakuamuru leo kumpenda Yahwe Mungu wako, kutembea katika njia zake, na kushikilia amri zake, kanuni zake, na sheria zake, utaishi na kuongezeka, na Yahwe Mungu wako atakubariki katika nchi ambayo unaingia kumiliki.
17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu,
Lakini moyo wako ukigeuka, na usisikilize na badala yake unavutwa na kusujudia miungu mingine na kuwaabudu,
18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.
basi leo nakutangazia kwako ya kwamba hakika utaangamia; siku zako hazitaongezeka katika nchi unayoipita juu ya Yordani kuingia na kumiliki.
19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi,
Naziita mbingu na nchi kushuhudia dhidi yako ya kuwa nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; kwa hiyo chagua uzima ili kwamba uweze kuishi, wewe na uzao wako.
20 na ili upate kumpenda Bwana Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Bwana ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.
Fanya hivi ili umpende Yahwe Mungu wako, kutii sauti yake, na kung’ang’ania kwake. Kwa maana yeye ni uzima wako na urefu wa siku zako; fanya hivi ili kwamba uweze kuishi katika nchi ambayo Yahwe aliapa kwa mababu zako, kwa Abrahamu, kwa Isaka, na kwa Yakobo, kuwapatia.

< Torati 30 >