< Torati 26 >

1 Mtakapokuwa mmeingia nchi ile ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake,
Utakapofika katika nchi ambayo Yahwe Mungu wako anakupatia kama urithi, na utakapoimiliki na kuishi ndani yake,
2 chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali ambapo Bwana Mungu wako atapachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake
basi unatakiwa kuchukua baadhi ya mavuno yote ya kwanza ya ardhi uliyoyaleta kutoka katika nchi ambayo Yahwe Mungu wako anakupatia. Unatakiwa kuyaweka ndani ya kikapu na kuelekea katika eneo ambalo Yahwe Mungu wako atapachagua kama mahali patakatifu.
3 na umwambie kuhani atakayekuwepo kwa wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Bwana Mungu wako kwamba nimekuja katika nchi ambayo Bwana aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.”
Unatakiwa kwenda kwa kuhani ambaye atakuwa akihudumu katika siku hizo na kumwambia, “Siku ya leo ninakiri kwa Yahwe Mungu wako ya kuwa nimekuja katika nchi ambayo Yahwe aliapa kwa mababu zetu kutupatia”.
4 Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Bwana Mungu wako.
Kuhani anatakiwa kuchukua kikapu mkononi mwako na kukiweka madhabahuni ya Yahwe Mungu wako.
5 Kisha utatangaza mbele za Bwana Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi.
Unapaswa kusema mbele ya Yahwe Mungu wako, “Babu yangu alikuwa Mwaremi mzururaji. Alikwenda chini hadi Misri na kukaa kule, na idadi ya watu wake ilikuwa chache. Kule akawa taifa kubwa, lenye nguvu na idadi kubwa.
6 Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu.
Wamisri walitutendea vibaya na kututesa. Walitulazimisha kufanya kazi za watumwa.
7 Kisha tulimlilia Bwana, Mungu wa baba zetu, naye Bwana akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu.
Tulimlilia Yahwe, Mungu wa baba zetu, naye akasikia sauti yetu na kuona mateso yetu, kazi zetu na mateso yetu.
8 Kwa hiyo Bwana akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu.
Yahwe alituondoa Misri kwa mkono wake mkuu, kwa mkono wake ulionyoshwa, kwa hofu kuu, kwa ishara na miujiza;
9 Akatuleta mahali hapa akatupa nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali;
na ametuleta katika sehemu hii na kutupatia nchi hii, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali.
10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Bwana, umenipa.” Weka kapu mbele za Bwana Mungu wako na usujudu mbele zake.
Tazama sasa, nimeleta mavuno ya kwanza kutoka katika nchi ambayo wewe, Yahwe, umenipatia.” Unapaswa kuweka chini mbele ya Yahwe Mungu wako na kuabudu mbele zake;
11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walioko miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Bwana Mungu wenu amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.
na unapaswa kufurahia katika mema yote ambayo Yahwe Mungu wako amekufanyia, kwa ajili na nyumba yako – wewe, na Mlawi, na mgeni aliye miongoni mwako.
12 Wakati utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba.
Utakapomaliza kutoa zaka yote ya mavuno katika mwaka wa tatu, yaani, mwaka wa kutoa zaka, basi unapaswa kuwapatia Mlawi, kwa mgeni, kwa yatima, na kwa mjane, ili kwamba waweze kula ndani ya malango yenu ya mji na kujazilishwa.
13 Kisha umwambie Bwana Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo.
Unatakiwa kusema mbele ya Yahwe Mungu wako, “Nimetoa kutoka nyumbani mwangu vitu ambavyo ni mali ya Yahwe, na kumpatia Mlawi, mgeni, yatima, na mjane, kulingana na amri zote ulizonipatia. Sijavunja amri yako yoyote, wala sijazisahau.
14 Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yoyote kwa wafu. Nimemtii Bwana Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru.
Sijala kati yao wakati wa maombolezo yangu, wala sijaziweka mahali pengine nilipokuwa mchafu, wala sijazitoa kati yao kwa heshima ya wafu. Nimesikiliza sauti ya Yahwe Mungu wangu; Nimetii kila kitu ulichoniamuru kukifanya.
15 Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako matakatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupa kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”
Tazama chini kutoka mahali patakatifu unapoishi, kutoka mbinguni, na ubariki watu wako Israeli, na nchi uliyotupatia, kama ulivyoapa kwa mababu zetu, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali.
16 Bwana Mungu wako anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zishike kwa bidii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
Leo Yahwe Mungu wako anawaamuru kuzitii sheria na amri hizi; basi utazishikilia na kuzitenda kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote.
17 Umetangaza leo kwamba Bwana ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii.
Umetamka leo ya kuwa Yahwe ni Mungu wako, na kwamba utatembea katika njia zake na kushikilia sheria zake, maagizo yake na amri zake, na kwamba utaisikiliza sauti yake.
18 Naye Bwana ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya thamani kama alivyoahidi, ili kwamba mpate kuyashika maagizo yake yote.
Leo Yahwe ametamka ya kwamba mu watu ambao ni mali yake, kama alivyoahidi kwenu, na kwamba mnapaswa kushikilia amri zake zote.
19 Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu, kama alivyoahidi.
Na atawaweka juu zaidi ya mataifa mengine aliyoyaumba nanyi mtapokea sifa, umaarufu na heshima. Mtakuwa watu waliowekwa kando kwa Yahwe Mungu wako, kama alivyosema.”

< Torati 26 >