< Torati 23 >
1 Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Bwana.
2 Mtu yeyote ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Bwana, hata mpaka kizazi cha kumi.
3 Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Bwana, hata mpaka kizazi cha kumi.
4 Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mlipotoka Misri, tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyoko Aramu-Naharaimu ili kuwalaani ninyi.
5 Hata hivyo, Bwana Mungu wenu hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Bwana Mungu wenu anawapenda.
6 Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.
7 Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake.
8 Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Bwana.
9 Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi.
10 Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko.
11 Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.
12 Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia.
13 Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kile kikutokacho.
14 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu akageuka na kuwaacha.
15 Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake.
16 Mwache aishi miongoni mwenu mahali popote anapopapenda na katika mji wowote anaochagua. Usimwonee.
17 Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.
18 Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya Bwana Mungu wako kwa ajili ya nadhiri yoyote, kwa sababu Bwana Mungu wako anachukizwa na yote mawili.
19 Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho waweza kupata riba juu yake.
20 Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili kwamba Bwana Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki.
21 Ukiweka nadhiri kwa Bwana Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi.
22 Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia.
23 Chochote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za Bwana Mungu wako kwa kinywa chako mwenyewe.
24 Kama ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke chochote kwenye kikapu chako.
25 Kama ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.