< Torati 21 >

1 Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua,
Iwapo mtu amekutwa kauwawa ndani ya nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kumiliki, kalala shambani, na haijulikani aliyemshambulia;
2 wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala mpaka kwenye miji ya jirani.
basi wazee wenu pamoja na waamuzi wenu wanapaswa kutoka nje, na kupima katika miji ambayo inamzunguka yule aliyeuawa.
3 Kisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira,
Kisha wazee wa mji ulio karibu na mwili wa marehemu wanapaswa kuchukua mtamba kutoka kwenye kundi la mifugo, ambaye hajawahi kutumikishwa, wala kubebeshwa nira.
4 na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi itiririkayo. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo.
Kisha wanapaswa kumuongoza mtamba huyo mpaka chini ya bonde litiririkalo maji, bonde ambalo halijawahi kulimwa wala kupandwa, na mle bondeni wanapaswa kuvunja shingo ya mtamba huyo.
5 Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Bwana, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio.
Makuhani, uzao wa Lawi, wanapaswa kuja mbele, kwa maana Yahwe Mungu wako amewachagua wamtumikie yeye na kutoa baraka katika jina la Yahwe na kuamua kila mtafaruku na ugomvi kwa neno lao.
6 Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde,
Wazee wote wa mji ulio karibu na mtu aliyeuawa wanapaswa kunawa mikono yao juu ya mtamba aliyevunjwa shingo bondeni;
7 nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika.
na wanapaswa kutoa suhulisho juu ya jambo hilo na kusema, ‘Mikono yetu haijamwaga damu hii, wala macho yetu hayajaona suala hili.
8 Ee Bwana, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli, ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho.
Tusamehe watu wako Israeli, Yahwe, ambao umewakomboa, na usiweke hatia juu ya umwagaji damu usio na kosa miongoni mwa watu wako Israeli.’ Kisha umwagaji damu utasamehewa kwao.
9 Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Bwana.
Kwa njia hii utaweka mbali umwagaji damu usio na hatia miongoni mwenu, mtakapofanya yaliyo mema machoni pa YAHWE.
10 Mkienda vitani kupigana na adui zenu naye Bwana Mungu wenu akawatia adui mikononi mwenu, nanyi mkachukua mateka,
Utakapokwenda kupigana vita dhidi ya maadui zako na Yahwe Mungu wako atakapokupa ushindi na kuwaweka chini ya mamlaka yako, na ukawachukua mbali kuwa mateka,
11 kama ukiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri wa sura nawe wavutwa naye, waweza kumwoa akawa mke wako.
kama kati ya mateka ukamwona mwanamke mzuri, nawe ukamtamani na kutaka kujitwalia awe mke wako,
12 Mlete nyumbani mwako, anyoe nywele na kukata kucha zake,
basi utamleta nyumbani kwako; atanyoa nywele zake na kukata kucha zake.
13 avue nguo alizokuwa amevaa alipotekwa. Baada ya kuishi nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake kwa mwezi mzima, ndipo utakapoweza kumwendea na kuwa mume wake naye atakuwa mke wako.
Kisha atazivua nguo alizokuwa amezivaa wakati alipochukuliwa mateka na atabaki nyumbani kwako na kuwaomboleza baba yake na mama yake kwa mwezi mzima. Baada ya hapo unaweza kulala naye na kuwa mume wake, naye atakuwa mke wako.
14 Lakini kama hutaendelea kupendezwa naye, mwache aende popote anapotaka. Kamwe huwezi kumuuza au kumtendea kama mtumwa, kwa sababu utakuwa umemvunjia heshima.
Lakini usipofurahishwa naye, basi unatakiwa kumruhusu aondoke apendaye yeye. Lakini haupaswi kamwe kumuuza kwa fedha, pia haupaswi kumfanya kama mtumwa, kwa sababu umemdhalilisha.
15 Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda,
Iwapo mwanamume ana wake wawili na mmoja wao ampenda na mwingine kumchukia, na wote wamekwisha mzalia watoto –wote mwanamke mpendwa na mwanamke achukiwae –
16 wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi.
basi katika siku ambayo mwanamume atakapowarithisha mali zake wanawe, hapaswi kumfanya mwana wa mke ampendaye kuwa mzawa wa kwanza kabla ya mwana wa mke amchukiaye, ambaye ndiye mwana wa kwanza.
17 Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyo navyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.
Badala yake, anapaswa kumtambua mwana wa kwanza, mwana wa mke asiyempenda, kwa kumpatia mara mbili ya mali zake; kwa maana huyo mwana ni mwanzo wa nguvu zake; haki za mzawa wa kwanza ni zake.
18 Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomrudi,
Iwapo mwanamume ana mwana mkaidi na muasi ambaye hatatii sauti ya baba yake au sauti ya mama yake, ambaye, hata baada ya kurekebishwa, hatawasikia;
19 baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake.
basi baba yake na mama yake wanapaswa kumshika na kumleta mbele ya wazee wa mji na kwenye malango ya mji.
20 Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.”
Wanapaswa kuwaambia wazee wa mji, “Huyu mwanetu ni mkaidi na muasi; hataki kusikia sauti zetu; ni mwasherati na pia ni mlevi’.
21 Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe mpaka afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.
Kisha wanaume wote wa mji wanapaswa kumpiga kwa mawe hadi kufa; nanyi mtaondoa uovu miongoni mwenu. Israeli yote itasikia juu ya hili na kuogopa.
22 Kama mtu ana hatia ya kosa linalompasa kuuawa naye akauawa, mwili wake utaangikwa mtini,
Iwapo mwanamume kafanya dhambi inayostahili kifo na kisha akauwawa, kwa kunyongwa juu ya mti,
23 kamwe msiuache mwili wake mtini usiku kucha. Hakikisheni mnauzika mwili wake siku ile ile, kwa sababu kila mtu anayeangikwa mtini yupo chini ya laana ya Mungu. Msiinajisi nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi wenu.
basi mwili wake haupaswi kubaki usiku kucha juu ya mti. Badala yake, unapaswa kuhakikisha unamzika siku hiyo; kwa maana yeyote anyongwaye amekwisha laaniwa na Mungu. Tii amri hii ili kwamba usitie najisi nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kama urithi.

< Torati 21 >