< Torati 19 >
1 Wakati Bwana Mungu wenu atakapokuwa amewaangamiza mataifa ambayo nchi yao anawapa ninyi, wakati mtakapokuwa mmewafukuza na kuishi katika miji yao na nyumba zao,
2 ndipo mtenge miji mitatu iliyopo katikati ya nchi kwa ajili yenu, katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kuimiliki.
3 Jengeni barabara katika miji hiyo na kuigawa mara tatu, nchi anayowapa Bwana Mungu wenu kama urithi, ili kwamba yeyote amuuaye mtu aweze kukimbilia humo.
4 Hii ndiyo kanuni kuhusu mtu amuuaye mwingine na kukimbilia humo kuokoa maisha yake, yaani, yeye amuuaye jirani yake bila kukusudia, wala hakumchukia kabla ya hapo.
5 Kwa mfano, mtu aweza kwenda msituni na jirani yake kukata miti, naye anapozungusha shoka kuangusha mti, shoka linaweza kuchomoka kutoka kwenye mpini na kumpiga jirani yake na kumuua. Yule mtu anaweza kukimbilia katika mmojawapo ya miji hii na kuokoa maisha yake.
6 Kama sivyo, mlipiza kisasi cha damu anaweza kumfuatilia kwa hasira kali, naye akamkamata na kumuua kama umbali ni mrefu sana hata ingawa hastahili kifo, kwa sababu amemuua jirani yake bila kukusudia.
7 Hii ndiyo sababu nimewaagiza ninyi kutenga miji mitatu ya makimbilio kwa ajili yenu.
8 Kama Bwana Mungu wenu akipanua nchi yenu, kama alivyoahidi kwa kiapo kwa baba zenu na kuwapa nchi yote aliyowaahidi,
9 kwa sababu mmefuata kwa uangalifu sheria zote ninazowaamuru leo, kumpenda Bwana Mungu wenu na kuenenda siku zote katika njia zake, ndipo mtenge miji mingine, mitatu zaidi.
10 Fanyeni hivi ili damu isiyo na hatia isimwagwe katika nchi yenu, ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi wenu, ili kwamba msije mkawa na hatia ya kumwaga damu.
11 Lakini kama mtu anamchukia ndugu yake, akamvizia, akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia katika mmojawapo ya miji hii,
12 wazee wa mji wake watatuma ujumbe kwake, kumleta kutoka mji ule na kumkabidhi mlipiza kisasi cha damu kumuua.
13 Msimwonee huruma. Lazima mwondoe katika Israeli hatia ya umwagaji damu isiyo na hatia ili kwamba mpate kufanikiwa.
14 Usisogeze jiwe la mpaka wa jirani yako ambao uliwekwa na wale waliokutangulia katika urithi upokeao katika nchi Bwana Mungu wako anayowapa kuimiliki.
15 Shahidi mmoja hatoshi kumtia hatiani mtu kwa uhalifu au kosa lolote ambalo anaweza kuwa amelitenda. Lazima shauri lolote lithibitishwe kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu.
16 Kama shahidi mwenye nia ya kumdhuru mwingine akisimama kumshtaki mtu kwa uhalifu,
17 watu wawili wanaohusika katika mabishano lazima wasimame mbele za Bwana na mbele ya makuhani na waamuzi ambao wako kazini wakati huo.
18 Waamuzi lazima wafanye uchunguzi kwa makini na shahidi akionekana kuwa ni mwongo, akitoa ushuhuda wa uongo dhidi ya ndugu yake,
19 basi mtende kama alivyotaka kumtendea ndugu yake. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
20 Watu watakaosalia watasikia hili na kuogopa, uovu kama huo kamwe hautatendeka tena miongoni mwenu.
21 Msionyeshe huruma, uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.