< Danieli 8 >

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Belshaza, mimi Danieli, nilipata maono, baada ya maono ambayo yalikuwa yamenitokea mbeleni.
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Belshaza, mimi Danieli niliona maono (baada ya maono ya awali yaliyonipata).
2 Katika maono yangu, nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu. Katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai.
Nilipokuwa nikiangalia katika ndoto, niliona kwamba nilikuwa katika mji wa Shushani wenye ngome katika jimbo la Elamu. Niliona katika ndoto kuwa nilikuwa karibu na mfereji wa Ulai.
3 Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye.
Nilitazama juu na nikaona mbele yangu kondoo dume lenye mapembe mawili, limesimama pembeni mwa mfereji. Pembe moja lilikuwa refu kuliko jingine, lakini pembe ndefu ilikuwa inakua pole pole kuliko ile fupi na pembe fupi ilirefuka na kuizidi nyingine.
4 Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama dhidi yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Alifanya kama atakavyo, naye akawa mkuu.
Niliona kondoo mme akiishambulia magharibi, kisha kaskazini, na baadaye kusini; hakuna mnyama mwingine aliyeweza kusimama mbele yake. Hakuna yeyote aliyeweza kumwokoa yeyote katika mkono wake. Alifanya chochote kile alichokitaka, na alikuwa mtu mkubwa sana.
5 Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa sana katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi.
Na nilipokuwa natafakari juu ya haya, niliona beberu akitoka magharibi, na kuvuka katika uso wa dunia yote, akikimbia kwa kasi kana kwamba hakuonekana kama aligusa ardhini. Mbuzi huyo alikuwa na pembe kubwa katikati ya macho yake.
6 Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi.
Alienda mpaka kwa kondoo aliyekuwa na pembe mbili, nilikuwa nimemwona kondoo dume amesimama katika ukingo wa mfereji na mbuzi alikimbia kumwelekea kondoo dume kwa hasira kali.
7 Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akimpiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu, hivyo akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu.
Niliiona mbuzi ikija karibu na kondoo. Mbuzi alikuwa na hasira na kondoo, alimpiga kondoo na alizivunja pembe zake mbili. Kondoo hakuwa na nguvu za kusimama mbele zake. Mbuzi alimgonga kondoo akaanguka chini na akamkanyaga. Hapakuwa na yeyote wa kumwokoa kutoka katika nguvu zake.
8 Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.
Ndipo mbuzi alikua akawa mkubwa, lakini alipokuwa na nguvu, pembe kubwa ilivunjwa, na katika sehemu yake zilichipuka na kukua pembe nne kubwa zilizochomoza kuelekea pepo nne za mbingu.
9 Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo ukaongezeka nguvu kuelekea kusini, na kuelekea mashariki, na kuelekea Nchi ya Kupendeza.
Kutoka katika pembe moja ilichipuka pembe nyingine, ilikuwa ndogo hapo awali, lakini baadaye ilikuwa pembe kubwa upande wa kusini, na mashariki, na katika nchi ya uzuri.
10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani, na kulikanyaga.
Pembe ilikuwa kubwa na matokeo yake iliinua vita dhidi ya jeshi la mbinguni. Baadhi ya jeshi na nyota kadhaa zilitupwa chini duniani, na zilikanyagwa.
11 Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi; ikamwondolea dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini.
Alizidi kuwa mkubwa, mkubwa kama kamanda wa jeshi la kimungu. Sadaka za kuteketezwa za kila siku ziliondolewa mbali na yeye, na sehemu yake takatifu zilitiwa unajisi.
12 Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mikononi mwake. Ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.
Kwasababu ya uasi, pembe ya mbuzi ilipewa jeshi, na sadaka za kuteketezwa zitasitishwa. Pembe itautupa ukweli chini ardhini, na itafanikiwa katika kila jambo ilifanyalo.
13 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”
Kisha nilimsikia mtakatifu mmoja akiongea na mtakatifu mwingine akamjibu, “Mambo haya yatadumu kwa muda gani, maono haya ya sadaka ya kuteketezwa, dhambi ile iletayo uharibifu, ukabidhiajia wa sehemu takatifu, na jeshi la mbinguni kukanyagwa?
14 Akaniambia, “Itachukua siku 2,300. Ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”
Aliniambia, “Itadumu kwa jioni na asubuhi zipatazo 2, 300. Baada ya hapo, mahali patakatifu patawekwa sawa.”
15 Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu.
Wakati mimi Danieli, nilipoona maono, nilijaribu kuyaelewa. na hapo mbele yangu alisimama yule aliyeoneakana kama mtu.
16 Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Gabrieli, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”
Niliisikia sauti ya mtu ikiita katikati ya kingo za mfereji wa Ulai. Alisema, “Gabrieli, msaidie mtu huyu kuelewa maono.”
17 Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”
Basi alikuja karibu na mahali niliposimama. Na alipokuja, niliogopa na nilisujudia hadi chini. Aliniambia,”Fahamu, mwana wa mtu, kwamba maono ni kwa ajili ya wakati wa mwisho.”
18 Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima.
Alipokuwa anaongea na mimi, nilipata usiingizi mzito nikiwa nimelala kifudifudi. Kisha alinishika na kunisimamisha.
19 Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa.
Akaniambia, “Tazama, nitakuonyesha kile kitachotokea baadaye katika kipindi cha ghadhabu, kwasababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho uliopangwa.
20 Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi.
Na kuhusu kondoo mme uliyemwona, yule mwenye pembe mbili - ni wafalme wawili wa Umedi na Uajemi.
21 Yule beberu mwenye nywele nyingi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.
Mbuzi dume ni mfalme wa Ugiriki. Pembe kubwa katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.
22 Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ule uliovunjika.
Na kuhusu pembe iliyovunjika, ambayo katika nafasi yake pembe zingine nne zilichipuka - hizi ni falme nne zitakazoinuka kutoka katika taifa lake, lakini hazitakuwa na nguvu kubwa.
23 “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, wakati waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila.
Katika siku zijazo za falme hizo, wakati ambapo wahalifu watakuwa wamefikia kikomo chao, mfalme mwenye uso katili, na yeye mwenye akili sana, atainuka.
24 Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu.
Nguvu zake zitakuwa kubwa, lakini si kwa nguvu zake mwenyewe. Atakuwa wa kustaajabisha kwa kile atakachokuwa anakiharibu; atafanya na kufanikiwa. Atawaangamiza watu wenye nguvu, watu miongoni wa watakatifu.
25 Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora. Wakati wajisikiapo kuwa wako salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.
Ataufanya udanganyifu usitawi chini ya mkono wake kwasababu ya ujanja wake. Atawaangamiza watu wengi bila kutegemea. Atainuka pia hata kinyume cha Mfalme wa wafalme, na atavunjwa, lakini si kwa mkono wowote wa binadamu.
26 “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu wakati mrefu ujao.”
Maono kuhusu jioni na asubuhi ulizoambiwa ni ya kweli. Lakini uyafunge maono haya, kwa kuwa yanahusu siku nyingi za wakati ujao.
27 Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaenda kwenye shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo, nami sikuweza kuyaelewa.
Ndipo mimi, Danieli nilichoka sana na nikalala nikiwa dhaifu kwa siku kadhaa. Kisha nikainuka na nikaenda kufanya kazi za mfalme. Lakini nilikuwa nimetishwa sana na maono, na hapakuwa na mtu yeyote aliyeweza kuyaelewa.

< Danieli 8 >