< Danieli 7 >
1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni yake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.
Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza mfalme wa Babelli, Danieli alikuwa na ndoto na maono katika akili zake wakati alipokuwa amelala kitandani kwake. Kisha akayaandika yale aliyoyaona katika ndoto. Aliandika matukio ya muhimu sana:
2 Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwepo na upepo kutoka pande nne za mbingu, ukivuruga bahari kuu.
Danieli alieleza, “Usiku katika ndoto zangu niliona pepo nne za mbinguni zilikuwa zinaitikisa bahari kuu.
3 Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.
Wanyama wakubwa wanne, kila mmoja alikuwa tofauti na mwenzake, walitoka katika bahari.
4 “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikatazama mpaka mabawa yake yalipongʼolewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.
Mnyama wa kwanza alikuwa kama simba, lakini alikuwa na mabawa ya tai. Nilipokuwa natazama, mabawa yake yalikuwa yamepasuka na alikuwa ameinuliwa katika ardhi na alikuwa amesimama kwa miguu miwili kama mtu. Na alipewa akili za kibinadamu.
5 “Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, ambaye alionekana kama dubu. Upande wake mmoja ulikuwa umeinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama mpaka ushibe!’
Na kulikuwa na mnyama wa pili, alikuwa kama dubu, na alikuwa ameinama, alikuwa na mbavu tatu katikati ya meno yake katika mdomo wake. Aliambiwa, 'Inuka na umeze watu wangi.'
6 “Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.
Baada ya hili, niliangalia tena. Kulikuwa na mnyama mwingine ambaye alionekana kama chui. Mgongoni mwake alikuwa na mabawa manne kama mabawa ya ndege, na alikuwa na vichwa vinne. Alipewa mamlaka ya kutawala.
7 “Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.
Baada haya, niliona usiku katika ndoto yangu mnyama wa nne, mwenye kuogofya, na kutisha na mwenye nguvu. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; aliteketeza, na kuvunja vunja katika vipande, na kusaga saga katika miguuni pake kile kilichosalia. Alikuwa ni wa tofauti na wanyama wengine, na alikuwa na pembe kumi.
8 “Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni zilingʼolewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.
Na wakati nilipokuwa natafakari juu ya pembe, nilitazama na niliona pembe nyingine ndogo ilichipuka katikati ya pembe zingine. Mizizi ya pembe tatu kati ya pembe za mwanzo iling'olewa. Niliona katika pembe hii macho kama macho ya mtu na mdomo ambao ulikuwa ukijivuna kwa mambo makubwa.
9 “Nilipoendelea kutazama, “viti vya enzi vikawekwa, naye Mzee wa Siku akaketi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu. Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto, nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.
Na nilipotazama, viti vya enzi vilikuwa vimewekwa, na Mtu wa siku za kale alikaa sehemu yake. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theruji, na nywele zake katika kichwa chake zilikuwa safi kama sufu. Kiti chake cha enzi kilikuwa na miali ya moto, na magurudumu yake yalikuwa yanawaka moto.
10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka, ukipita mbele yake. Maelfu elfu wakamhudumia; kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake. Mahakama ikakaa kuhukumu, na vitabu vikafunguliwa.
Mto wa moto ulitiririka kutoka mbele yake, na mamilioni ya watu walimtumikia, na wengine mia moja milioni walikuwa wamesimama mbele yake. Na mahakama iliitishwa, na vitabu vilifunguliwa.
11 “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka.
Niliendelea kuangalia kwasababu ya maneno ya kiburi yaliyosemwa na pembe. Nilitazama wakati mnyama anauliwa, na mwili wake uliharibiwa, na ulitolewa kwa ajili ya kuchomwa moto.
12 (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda fulani.)
Na kwa wale wanyama wanne waliosalia, mamlaka yao yalitwaliwa mbali, lakini maisha yao yaliendelezea kwa kipindi fulani cha muda.
13 “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake.
Katika maono yangu usiku ule, nilimwona mtu mmoja anakuja katika mawingu ya mbinguni alikuwa kama mwana wa mtu; alikuja kwa Mzee wa Siku na aliletwa mbele zake.
14 Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa kabila zote, mataifa, na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.
Naye alipewa mamlaka ya kiutawala na utukufu na mamlaka ya kifalme ili kwamba watu wote, na mataifa na lugha ziweze kumtumikia yeye. Mamlaka yake ya kutawala ni mamlaka ya milele ambayo hayatapita, na ufalme wake ni ule ambao hautaangamizwa.
15 “Mimi, Danieli, nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua.
Na kwangu mimi, Danieli, roho yangu ilihuzunishwa ndani yangu, na maono niliyoyaona katika akili zangu yalinisumbua.
16 Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale na kumuuliza maana halisi ya haya yote. “Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi:
Nilimsogelea mmoja wa hawa walikuwa wamesimama hapo na nikamwomba anioneshe maana ya mambo haya.
17 ‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani.
Hawa wanyama nne wakubwa ni wafalme wanne ambao watatoa katika nchi.
18 Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’
Lakini watu watakatifu wa Mungu aliyejuu wataupokea ufalme na wataumiliki milele na milele.'
19 “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia.
Ndipo nilipotaka kujua zaidi juu ya mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti sana na wengine na alikuwa wa kutisha pamoja na meno yake ya chuma na makucha ya shaba; alimeza, na alivunja vipande vipande, na alisaga saga kwa miguu yake kile kilichokuwa kimesalia.
20 Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno.
Nilitaka kujua juu ya pembe kumi katika kichwa chake, na kuhusu pembe nyingine iliyochomoza, na ambayo mbele yake pembe zingine tatu zilianguka chini. Nilitaka kujua kuhusu pembe yenye macho na kuhusu mdomo uliokuwa unajisifu kwa mambo makubwa na ambayo ilionekana kuwa ni kubwa kuliko zingine.
21 Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda,
Na nilipotazama, pembe hii iliinua vita dhidi ya watu watakatifu na ilikuwa inawawashinda mpaka pale
22 mpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme.
Mzee wa Siku alipokuja, na watu watakatifu wa Mungu Aliye Juu Sana. Ndipo wakati ulipowadia ambapo watu watakatifu waliupokea ufalme.
23 “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda.
Hiki ndicho mtu yule alichokisema, 'Kwa habari ya mnyama wanne, utakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia ambao utakuwa tofauti na falme zingine zote. Utaimeza dunia yote, na utaikanyaga yote chini na kuivunja vunja vipande vipande.
24 Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu.
Na kuhusu pembe kumi, kutoka katika ufalme huu, wafalme kumi watainuka, na mwingine atainuka baada yao. Atakuwa wa tofauti na wale waliomtangulia, na atawashinda wale wafalme watatu.
25 Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.
Atazungumza maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu sana na atawatesa watu watakatifu wa Mungu Aliye Juu. Atajaribu kuzibadili sikukuu na sheria. Mambo haya atapewa mikononi mwake kwa mwaka mmoja, miaka miwili na nusu mwaka.
26 “‘Lakini mahakama itakaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele.
Lakini kikao cha mahakama kitaitishwa, na watazichukua nguvu zake za kifalme ili mwisho aweza kuharibiwa na kuteketezwa.
27 Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’
Ufalme na utawala, ukubwa wa falme chini ya mbingu yote, watapewa watu walio wa watu watakatifu wa Yeye Aliye juu Sana. Ufalme wake ni ufalme wa milele, na falme zingine zote zitamtumikia na kumtii yeye.'
28 “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu.”
Na huu ndio mwisho wa mambo. Na kuhusu mimi, Danieli, mawazo yangu yanihuzunisha sana mimi na mwonekano wa uso wangu ulibadilika. Lakini mambo haya niliyahifadhi mimi mwenyewe.”