< Danieli 6 >

1 Ilimpendeza Dario kuteua wakuu 120 kutawala katika ufalme wake wote,
Ilimpendeza Dario kuchagua juu ya ufalme magavana wa majimbo 120 ambao wangetawala juu ya ufalme wote.
2 pamoja na wasimamizi watatu juu yao, ambao mmoja wao alikuwa Danieli. Wakuu walitoa hesabu kwa hao wasimamizi ili mfalme asipate hasara.
Juu yao kulikuwa na watawala wakuu watatu, na Daniel alikuwa mmoja wao. Hawa watawala waliwekwa ili waweze kuwasimamia magavana wa majimbo, ili kwamba mfalme asipate hasara.
3 Basi Danieli alijidhihirisha, miongoni mwa wasimamizi na wakuu kwa sifa zake za kipekee hata mfalme akapanga kumweka juu ya ufalme wote.
Danieli alipambanuliwa juu ya watawala wakuu na juu ya magavana wa majimbo kwasababu alikuwa na roho isiyo ya kawaida. Mfalme alikuwa akipanga kumweka juu ya ufalme wote.
4 Walipofahamu hilo, wakuu na wasimamizi wakajaribu kutafuta sababu za kumshtaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu, wala hakupatikana na upotovu au uzembe.
Basi watawala wakuu wengine na magavana wa majimbo walitafuta makosa katika kazi ambazo Danieli alizifanya kwa ufalme, lakini hawakuweza kuona ufisadi au kushindwa katika majukumu yake kwasababu alikuwa mwaminifu. Hakuna kosa au uzembe uliopatikana ndani yake.
5 Mwishoni watu hawa walisema, “Kamwe hatutapata msingi wa mashtaka dhidi ya huyu Danieli isipokuwa iwe inahusiana na sheria ya Mungu wake.”
Kisha watu hawa wakasema, “Hatukuweza kupata sababu yoyote ya kumshitaki huyu Danieli isipokuwa tukitafuta kitu fulani dhidi yake kuhusiana na sheria za Mungu wake.'”
6 Basi wasimamizi na wakuu wakaingia kwa mfalme kama kikundi wakasema, “Ee Mfalme Dario, uishi milele!
Ndipo watawala hawa na magavana walileta mpango mbele ya mfalme. Walimwambia, “Mfalme Dario, uishi milele!
7 Wasimamizi wa ufalme, wasaidizi, wakuu, washauri na watawala wote wamekubaliana kwamba mfalme atoe sheria na kukazia amri kuwa yeyote atakayetoa dua kwa mungu au mwanadamu yeyote katika muda huu wa siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, ee mfalme, atupwe ndani ya tundu la simba.
Watawala wote wakuu wa ufalme, magavana wa mikoa, na magavana wa majimbo, washauri, na magavana wameshauriana kwa pamoja na kuamua kuwa wewe, mfalme, unapaswa kupitisha amri na kuitekeleza, ili kwamba mtu yeyote anayefanya dua kwa mungu yeyote au mtu kwa siku thelathini, isipokuwa wewe mfalme, mtu huyo lazima atupwe katika tundu la simba.
8 Sasa, ee mfalme, toa amri na uiandike ili isiweze kubadilishwa: kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.”
Sasa mfalme, litoe agizo na utie saini nyaraka ili kwamba isije ikabadilika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi, hivyo haiweze ikabatilishwa.
9 Hivyo Mfalme Dario akaiweka amri hiyo katika maandishi.
Basi, mfalme Dario alitia saini nyaraka kwa kuifanya amri kuwa sheria.
10 Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake kama alivyokuwa akifanya mwanzoni.
Danieli alipojua kuwa nyaraka imekwisha kusainiwa kuwa sheria, alienda ndani ya nyumba yake (madirisha yake katika chumba cha juu yalikuwa wazi kuelekea Yerusalemu), na alipiga magoti yake, kama alivyokuwa akifanya mara tatu kwa siku, na aliomba na kushukuru mbele ya Mungu wake, kama alivyofanya hapo kabla.
11 Ndipo watu hawa wakaenda kama kikundi na kumkuta Danieli akiomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada.
Kisha watu hawa walikuwa wameunda hila kwa pamoja walimwona Danieli akiomba na kutafuta msaada kutoka kwa Mungu.
12 Basi wakaenda kwa mfalme na kusema naye kuhusu amri ya mfalme: “Je, hukutangaza amri kwamba kwa muda huu wa siku thelathini zijazo mtu yeyote ambaye atamwomba mungu au mwanadamu yeyote isipokuwa wewe, ee mfalme, angetupwa ndani ya tundu la simba?” Mfalme akajibu, “Amri ndivyo ilivyo, kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.”
Ndipo walipomwendea mfalme na kuongea naye kuhusiana na amri yake: “Je haukuweka amri kwamba mtu yeyote akayefanya maombi kwa mungu mwingine au kwa binadamu ndani ya siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, mfalme, lazima mtu huyo atupwe katika tundu la simba? Mfalme akajibu, “Jambo hili ni la hakika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi; ambazo haziwezi zikabatilishwa.”
13 Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa mahamisho kutoka Yuda, hakuheshimu, ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Bado anaomba mara tatu kwa siku.”
Kisha wakamjibu mfalme, “Mtu yule Daniel, ambaye ni mmoja wa watu wa mateka kutoka Yuda, hakutii wewe, mfalme wala maagizo yako uliyoyasaini. Yeye humwomba Mungu wake mara tatu kwa siku.”
14 Wakati mfalme aliposikia hili, akahuzunika mno. Akakusudia kumwokoa Danieli, hivyo akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua.
Mfalme aliposikia haya, alisikitishwa sana, alitumia akili jinsi ya kumwokoa kutoka katika utawala huu. Alisumbuka sana mpaka wakati wa kuzama kwa jua akijaribu kumwokoa Danieli.
15 Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.”
Kisha watu hawa waliokuwa wamepanga njama walikusanyika kwa pamoja na mfalme, na wakamwambia, “Ujue mfalme kwamba ni sheria ya Wamedi na Waajemi kwamba hakuna amri au sanamu ambayo mfalme anaipitisha yaweza kubadilishwa.”
16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, na wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!”
Ndipo mfalme alitoa agizo, na walimleta ndani Danieli, na kisha wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako, ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.''
17 Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mdomo wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili hali ya Danieli isiweze kubadilishwa.
Jiwe lililetwa katika mlango wa tundu, na mfalme alilitia muhuri wa pete yake mwenyewe na pamoja na muhuri wa wakuu wake ili kwamba chochote kisiweze kubadilishwa kuhusiana na Danieli.
18 Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme, naye usiku kucha hakula chakula wala kutumia viburudisho alivyoletewa. Lakini hakuweza kulala.
Basi mfalme alienda kwenye ikulu yake na usiku ule alikuwa na mfungo. Hakuna starehe yoyote iliyoletwa mbele yake, nao usingizi ulimkimbia.
19 Asubuhi na mapema, mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba.
Kisha katika mapambazuko mfalme aliamka na kwa haraka alienda kwenye tundu la simba.
20 Wakati alipokaribia lile tundu, akamwita Danieli kwa sauti ya uchungu, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa kwa simba?”
Na alipokaribia kwenye tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya huzuni, akimwambia Danieli, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je Mungu wako ambaye anamtumkia daima ameweza kukuokoa kutoka katika simba?
21 Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele!
Ndipo Danieli akamwambia mfalme, “Mfalme, uishi milele!
22 Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lolote baya mbele yako, ee mfalme.”
Mungu wangu amemtuma mjumbe na amevifunga vinywa vya simba, na hazijaweza kunidhuru. Kwa kuwa sikuwa na hatia yoyote mbele yake na pia mbele yako, ewe mfalme, na sijakufanyia jambo lolote la kukudhuru.”
23 Mfalme akafurahi mno, naye akatoa amri Danieli atolewe kutoka kwa lile tundu. Danieli alipotolewa kutoka kwa lile tundu, hakukutwa na jeraha lolote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.
Basi mfalme alikuwa na furaha sana. Alitoa agizo kwamba wanatakiwa wamtoe Danieli nje ya tundu. Hivyo Danieli aliondolewa kutoka katika tundu. Hakuna dhara lolote lililoonekana kwake, kwa kuwa alikuwa amemtumainia Mungu wake.
24 Kwa amri ya mfalme, wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote.
Mfalme alitoa agizo, waletwe wale watu waliomshitaki Danieli na kisha akawatupa wao katika tundu la simba - wao, na watoto wao, na wake zao. Kabla hawajafika sakafuni, simba waliwararua na kuvunjavunja mifupa yao vipande vipande.
25 Kisha Mfalme Dario akawaandikia kabila zote za watu, mataifa, na watu wa kila lugha katika nchi yote: “Ninyi na mstawi sana!
Kisha mfalme Dario aliandika ujumbe kwa watu wote, mataifa na lugha ambazo ziliishi katika dunia yote: “Amani na iongezeke kwenu.
26 “Natoa amri hii, kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu, lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli. “Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai, naye hudumu milele, ufalme wake hautaangamizwa, nao utawala wake hauna mwisho.
Ninaagiza kwamba katika utawala wote wa ufalme wangu watu watetemeka na kumcha mbele ya Mungu wa Danieli, kwa kuwa ni Mungu aliye hai na huishi milele, na ufalme wake hauwezi kuharibiwa; utawala wake utakuwepo hadi mwisho.
27 Huponya na kuokoa; hufanya ishara na maajabu mbinguni na duniani. Amemwokoa Danieli kutoka nguvu za simba.”
Yeye anatuhifadhi salama na kutuokoa, na anafanya ishara na maajabu mbinguni na duniani; amemhifadhi Danieli salama dhidi ya uwezo wa simba.”
28 Hivyo Danieli akastawi wakati wa utawala wa Dario, na utawala wa Koreshi Mwajemi.
Na hivyo basi, Danieli alifanikiwa katika utawala wa Dario na katika utawala wa Koreshi Mwajemi.

< Danieli 6 >