< Danieli 5 >
1 Mfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kwa ajili ya maelfu ya wakuu wake na akanywa mvinyo pamoja nao.
Mfalme Belshaza alifanya sherehe kubwa kwa kwa ajili ya wakuu wake wa kuheshimiwa wapatao elfu moja, na alikunywa divai mbele yao wote watu elfu moja.
2 Wakati Belshaza alipokuwa akinywa mvinyo wake, aliamuru viletwe vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekaluni huko Yerusalemu, ili mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake waweze kuvinywea.
Wakati Belshaza alipokuwa akionja divai, alitoa agizo la kuleta vyombo vilivyotengenezwa kwa dhahabu au kwa fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka katika hekalu huko Yerusalemu, ambavyo yeye, na wakuu wake, na wake zake, na masuria waliweza kuvinywea.
3 Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea.
Watumishi walivileta vyombo ya dhahabu vilivyokuwa vimechukulia katika hekalu, nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Mfalme na wakuu wake, na wake zake na masuria walivinywea.
4 Walipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.
Walikunywa divai na kuzisifu sanamu zao zilizotengenezwa kwa dhahabu na fedha, shaba, chuma, mbao na mawe.
5 Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika.
Kwa wakati huo huo vidole vya mkono wa mtu vilionekana mbele ya kinara cha taa na kuandika katika ukuta uliopigwa lipu katika ikulu ya mfalme. Mfalme aliweza kuona sehemu ya mkono ulipokuwa unaandika.
6 Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.
Ndipo uso wa mfalme ulibadilika na mawazo yake yalimwogopesha; miguu yake haikuweza kumfanya asimame, na magoti yake yalikuwa yakigongana kwa pamoja.
7 Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waganga waletwe, naye akawaambia hawa wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.”
Mfalme alitoa agizo kwa kupiga kelele, waletwe ndani wale ambao hudai wanaweza kuzungumza na wafu, watu wenye hekima, na wataalamu wa nyota. Mfalme akawaambia wale waliojulikana kwa hekima katika Babeli, “Yeyote atakayeyaeleza maandishi haya na maana yake atavikwa nguo za zambarau na atavikwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Naye atakuwa mtawala wa tatu wa juu kwa mamlaka katika ufalme.”
8 Ndipo watu wote wa mfalme wenye hekima wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake.
Ndipo watu wote wa mfalme walikuwa wakijulikana kwa hekima yao waliingia ndani, lakini hawakuweza kuyasoma maandishi wala kueleza maana yake kwa mfalme.
9 Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.
Kisha mfalme Belshaza alishitushwa sana na mwonekano wa uso wake ulibadilika. Wakuu wake nao walishangazwa sana.
10 Malkia aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi kiasi hicho!
Ndipo sasa malkia alikuja katika nyumba ya sherehe kwasababu ya kile ambacho mfalme na wakuu wake walikuwa wamekisema. Malkia akasema, “Mfalme na aishi milele! Usiache mawazo yako yakakusumbua. Usiruhusu mwonekano wa uso wako ubadilike.
11 Yuko mtu katika ufalme wako ambaye ana roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, yaani nasema mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi.
Kuna mtu katika ufalme wako ambaye ana roho ya miungu watakatifu dani yake. Katika siku za baba yako, mwanga na weledi na hekima ya miungu ilipatikana ndani yake. Mfalme Nebukadneza, baba yako mfalme, alimfanya kuwa mkuu wa waganga, pamoja na mkuu wa wale wanazungumza na wafu, na wa wenye hekima, na wa wataalamu wa nyota.
12 Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”
Roho bora, ufahamu, weledi, kutafsiri ndoto, kufafanua mafumbo na kutatua matatizo - hizi ni sifa zilizopatikana kwa mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Sasa mwiteni Danieli naye atawaambia maana ya kile kilichoandikwa.”
13 Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamuuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Yuda?
Ndipo Danieli alipoletwa mbele ya mfalme. Mfalme akamwambia, “Wewe ni yule Danieli, mmoja kati ya watu wa mateka wa Yuda, ambao baba yangu mfalme aliwaleta kutoka Yuda.
14 Nimesikia kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee.
Nimesikia habari kukuhusu wewe, kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na ya kwamba mwanga na ufahamu na hekima bora inapatikana ndani yako.
15 Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia.
Na sasa watu wanaojulikana kwa hekima na wale wanaozungumza na wafu, wamekwisha kuletwa mbele yangu, ili kusoma maandishi haya na kunijulisha maana ya tafsiri yake, lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri yake.
16 Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu katika ufalme.”
Nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo. Sasa kama utaweza kusoma maandishi na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na kuwa na kuvalishwa mkufu wa dhahabu shingoni mwako, na utakuwa mtawala wa tatu mwenye mamlaka katika ufalme.”
17 Ndipo Danieli akamjibu mfalme, “Waweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine zawadi zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa mfalme na kumwambia maana yake.
Kisha Danieli akajibu mbele ya mfalme, “Zawadi yako na iwe kwa ajili yako mwenyewe, na thawabu yako na umpe mtu mwingine. Hata hivyo, mfalme, nitakusomea maandishi na nitakwaambia maana.
18 “Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari.
Na juu yako, Ewe mfalme, Mungu Aliye juu sana alimpa Nebukadneza baba yako ufalme, ukuu, heshima na enzi.
19 Kwa sababu ya nafasi ya juu aliyompa baba yako, kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua; wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai; wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha; aliotaka kuwashusha, aliwashusha.
Na kwasababu ya ukuu huo, Mungu alimpa watu wote, mataifa, na lugha walimtetemekea na kumwogopa. Aliwauwa wale aliotaka wafe na aliwaacha hai wale aliotaka waishi. Aliwainua wale aliowataka, na aliwashusha wale aliowataka.
20 Lakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwa kiti chake cha ufalme na kuvuliwa utukufu wake.
Lakini wakati moyo ulipokuwa na kiburi na roho yake ilifanywa kuwa mgumu na kwasababu hiyo alitenda kwa kiburi, alishushwa kutoka kiti chake cha enzi cha kifalme, na waliiondoa enzi yake.
21 Akafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu, akala majani kama ngʼombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, mpaka alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala juu ya falme za wanadamu na kwamba humtawaza juu yao yeyote amtakaye.
Aliondolewa katika ubinadamu, alikuwa na akili za mnyama, na aliishi na punda wa mwituni. Alikula majani kama ng'ombe. Mwili wake ulilowanishwa kwa umande wa kutoka mbinguni mpaka pale alipojifunza kwamba Mungu Aliye Juu anatawala juu ya falme za watu na ya kwamba humweka mtu yeyote amtakaye juu yake.
22 “Lakini wewe mwanawe, ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote.
Wewe mwana wake, Belshaza, haujaunyenyekeza moyo wako, ingawa aliyajua haya yote.
23 Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.
Umejiinua mwenyewe kinyume cha Bwana wa mbinguni. Katika nyumba yake walikuletea vyombo ambavyo wewe, wakuu wako, wake zako na masuria wako walivinywea, na kisha ukaisifia sana sanamu zilitengenezwa kwa fedha na dhahabu, shaba, chuma, mbao, na mawe - sanamu ambazo haziwezi kuona, kusikia wa kujua kitu chochote. Haujamheshimu Mungu ambaye anaishikilia pumzi yako katika mkono wake na ambaye anazijua njia zako zote.
24 Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.
Ndipo Mungu aliutuma mkono kutoka katika makao yake na maandishi haya yaliandikwa.
25 “Haya ndiyo maneno yaliyoandikwa: mene, mene, tekeli na peresi
Haya ndiyo maandishi ambayo yaliandikwa: 'Mene, Mene, Tekeli na Peresin.'
26 “Hii ndiyo maana ya maneno haya: “Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
Maana yake ni: 'Mene,' 'Mungu ameuhesabu ufalme wako na ameukomesha.'
27 Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua.
'Tekeli' 'umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua.'
28 Peresi: Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.”
'Peresi' 'ufalme wako umegawanyika na wamepewa Wamedi na Waajemi.'”
29 Ndipo kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu katika ufalme.
Ndipo Belshaza alitoa agizo, na walimvalisha Danieli mavazi ya zambarau. Mkufu wa dhahabu walimvisha shingoni, na mfalme alitoa tamko juu ya Danieli kuwa atakuwa mtawala mwenye mamlaka ya nafasi ya tatu katika ufalme.
30 Usiku ule ule, Belshaza mfalme wa Wakaldayo akauawa,
Usiku ule Belshaza, mfalme wa Babeli aliuawa,
31 naye Dario Mmedi akashika ufalme akiwa na miaka sitini na miwili.
na Dario Mwajemi aliuchukua ufalme alipokuwa na miaka ipatayo sitini na miwili.