< Danieli 12 >
1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.
2 Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele.
3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.
4 Lakini wewe Danieli, yafunge na kuyatia muhuri maneno ya kitabu hiki mpaka wakati wa mwisho. Wengi watakwenda huku na huko, na maarifa yataongezeka.”
5 Ndipo mimi Danieli nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto, na mwingine ukingo wa pili wa mto.
6 Mmoja wao akasema na yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?”
7 Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.”
8 Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?”
9 Akajibu, “Danieli, enenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri mpaka wakati wa mwisho.
10 Wengi watatakaswa, na kuondolewa mawaa na kufanywa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu.
11 “Tangu wakati ule wa kukomeshwa dhabihu ya kila siku na kusimamishwa kwa chukizo la uharibifu, kutakuwako siku 1,290.
12 Amebarikiwa mtu yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku 1,335.
13 “Lakini wewe, enenda zako mpaka mwisho. Utapumzika, nawe ndipo mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekewa.”