< Danieli 11 >
1 Nami katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.)
Katika mwaka wa kwanza wa Dario Mmedi, mimi mwenyewe nilikuja kumwezesha na kumlinda Mikaeli.
2 “Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme watatu zaidi watatokea Uajemi, kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Wakati atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani.
Na sasa nitakufunulia ukweli. Wafalme watatu watainuka katika Uajemi, na mfalme wa nne atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Na wakati atakapopata nguvu kupitia utajiri wake, atamwamsha kila mtu kinyume na ufalme wa Ugiriki.
3 Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, ambaye atatawala kwa nguvu nyingi na kufanya anavyopenda.
Mfalme wenye nguvu atainuka ambaye atatawala ufalme mkubwa, na ataenenda kufuatana na matakwa yake mwenyewe.
4 Baada ya kujitokeza, milki yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautakwenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizotumia, kwa sababu milki yake itangʼolewa na kupewa wengine.
Na atakapokuwa ameinuka, ufalme wake utavunjika na utagawanyika katika pepo nne za mbinguni, lakini hawatakuwa wazao wake mwenyewe, na si kwa nguvu zake kwa wakati alipokuwa akitawala. Kwa kuwa ufalme wake utang'olewa kwa ajili ya wengine tofauti na wazawa wake.
5 “Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko mfalme, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi.
Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja kati ya maamiri jeshi wake atakuwa mwenye nguvu kuliko yeye na atautawala ufalme wake kwa nguvu kubwa.
6 Baada ya miaka kadha, wataungana. Binti wa mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini huyo binti nguvu zake hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, watoto wake, na yeyote aliyemuunga mkono.
Baada ya miaka michache, wakati muda utakapokuwa sawa, watafanya mwungano. Binti wa mfalme wa Kusini atakuja kwa mfalme wa Kaskazini kuyathibitisha makubaliano yao. Lakini hataweza kuzitunza nguvu za mkono wake, wala mfalme hatasimama wala mkono wake. Ataachwa na wale waliomleta, na baba yake, na yeye aliyemwunga mkono katika nyakati hizo.
7 “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao naye atashinda.
Lakini tawi kutoka katika mizizi yake litachipuka katika nafasi yake. Atalishambulia jeshi na kuingia ngome ya mfalme wa Kaskazini. Atapigana nao, na atawashinda.
8 Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadha atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua.
Ataichukua miungu yao mpaka Misri pamoa na sanamu zao za chuma na vyombo vyao vya fedha na vya dhahabu vyenye thamani. Kwa miaka mingi atakaa mbali na mfalme wa Kaskazini.
9 Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi nyuma hadi kwenye nchi yake.
Kisha mfalme wa Kaskazini atauvamia ufalme wa mfalme wa Kusini, lakini atajitoa na kwenda katika nchi yake mwenyewe.
10 Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.
Wana wake watajiweka tayari na kuunganisha jeshi kubwa. Litaendelea kukua na litagharikisha kila kitu, litapita katikati hadi kwenye ngome yake.
11 “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye ataunda jeshi kubwa, lakini litashindwa.
Ndipo mfalme wa Kusini atakasirika, na ataenda na kupigana naye, mfalme wa Kaskazini. Mfalme wa Kaskazini atainua jeshi kubwa, bali jeshi litatiwa katika mkono wake.
12 Wakati jeshi litakapokuwa limechukuliwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi na atachinja maelfu mengi, hata hivyo hatabaki na ushindi.
Jeshi litachukuliwa, na moyo wa mfalme wa Kusini utainuliwa juu, na atawafanya makumi maelfu kuanguka, lakini hataweza kuwa mshindi.
13 Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi jingine kubwa kuliko lile la kwanza; na baada ya miaka kadha, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.
Kisha mfalme wa Kaskazini atainua jeshi jingine, kubwa kuliko la kwanza. Baada ya miaka kadhaa, mfalme wa Kaskazini atakuja na jeshi kubwa likiwa na vifaa vingi.
14 “Katika nyakati hizo wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio.
Katika siku hizo wengi watainuka kinyume na mfalmea wa Kusini. Wana wa vurugu miongoni mwa watu wake watasimama wao wenyewe ili kuyatimiliza maono, lakini watajikwaa.
15 Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzunguka mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kuyazuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu ya kuwakabili.
Mfalme wa Kaskazini atakuja, kuizingira nchi kwa kuweka vilima, na kuuteka mji wenye ngome. Majeshi ya Kusini hayataweza kusimama, hata wanajeshi wake bora. Hawatakuwa na nguvu za kusimama.
16 Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza.
Badala yake, yeye ajaye ataenenda kwa kufuata tamaa zake kinyume chake; hakuna yeyote atakayesimama katika njia yake. Atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi wake.
17 Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia.
Mfalme wa Kaskazini atauelekeza uso wake ili kuja kwa nguvu za ufalme wake wote, na kutakuwa na makubaliano atakayoyafanya na mfalme wa Kusini. Atampatia katika ndoa binti wa wanawake ili kuuharibu ufalme wa Kusini. Lakini mpango huo hautafanikiwa wala kumsaidia.
18 Ndipo atabadili nia yake kupigana na nchi za pwani na ataziteka nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake na kurudisha ufidhuli wake juu yake.
Baada ya hayo, mfalme atafuatilia nchi za pwani na ataziteka nchi nyingi. Lakini amiri jeshi atakikomesha kiburi chake na atakisababisha kiburi chake kiishe.
19 Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
Kisha atafuatilia miji yenye ngome katika nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka; na hatapatikana tena.
20 “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.
Kisha mtu mwingine atainuka katika nafasi ambaye atamfanya mtoza ushuru apite kwa ajili ya ufahari wa ufalme. Lakini katika siku zijazo atakatiliwa mbali, lakini si kwa hasira wala si katika vita.
21 “Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona wako salama, naye atautwaa kwa hila.
Katika nafasi atainuka mtu wa kudharauliwa ambaye watu hawatampa heshima ya nguvu ya kifalme; atakuja bila kukusudiwa na atautwaa ufalme kwa ulaghai.
22 Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake; jeshi pamoja na mkuu mmoja wa agano wataangamizwa.
Mbele yake, kila jeshi litafutiliwa mbali kama gharika. Jeshi na kiongozi wa agano wataangamizwa wote kwa pamoja.
23 Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, na akitumia watu wachache tu ataingia madarakani.
Tangu katika kipindi kile ambacho makubaliano yalifanywa pamoja naye, ataenenda kwa kwa hila; atakuwa mwenye nguvu akiwa na watu wachache tu.
24 Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atafanikisha kile ambacho baba zake wala babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atafanya hila ya kupindua miji yenye maboma, lakini kwa muda mfupi tu.
Kwa ghafla ataingia katika sehemu tajiri sana za jimbo, na atafanya kile ambacho si baba yake wala baba wa baba yake alishakifanya. Atagawanya mateka, nyara, na mali zake miongoni mwa wafuasi wake. Atapanga mpango wa kuiangusha ngome, lakini ni kwa muda tu.
25 “Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya kwa hila zilizofanywa dhidi yake.
Ataamsha nguvu zake na moyo wake kinyume na mfalme wa Kusini kwa jeshi kubwa. Mfalme wa Kusini atapigana vita akiwa na jeshi kubwa lenye nguvu, lakini hataweza kusimama kwa kuwa wengine watafanya njama dhidi yake.
26 Wale wanaokula kutoka kwenye ruzuku za mfalme watajaribu kumwangamiza; jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani.
Hata wale wanaokula chakula chake kizuri watajaribu kumwangamiza. Jeshi lake litakatiliwa mbali kama gharika, na wengi wao watauawa.
27 Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya, wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamriwa.
Wafalme wote hawa wawili, wakiwa na mioyo yao imejawa na uovu kinyume na mwenzake, watakaa katika meza moja na kudanganyana, lakini haitakuwa na maana yoyote. Kwa kuwa mwisho utatokea katika kipindi ambacho kimeshapangwa.
28 Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume na agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano, kisha atarudi nchi yake.
Kisha mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake akiwa na utajiri mkubwa, na moyo wake ukipinga vikali agano takatifu. Atatenda na kisha atarudi katika nchi yake mwenyewe.
29 “Wakati ulioamriwa, atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza.
Katika muda uloamriwa atarudi na kuushambulia ufalme wa Kusini. Lakini katika kipindi hiki hakitakuwa kama awali.
30 Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atarudi nyuma na kutoa wazi hasira yake dhidi ya agano takatifu. Atarudi na kuonyesha fadhili kwa wale waliachao agano takatifu.
Kwa kuwa meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye ataogopa na kurudi nyuma. Atakuwa mwenye hasira dhidi ya agano takatifu, na atawaonyesha mema wale watakaoliacha agano takatifu.
31 “Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu, na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu lisababishalo ukiwa.
Majeshi yake yatainuka na kukufuru sehemu takatifu katika ngome. Wataziondoa sadaka za kawaida za kuteketezwa, na watasimamisha chukizo la uharibifu litakalosababisha ukiwa.
32 Kwa udanganyifu atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.
Na kwa wale walioenenda kwa ouvu kinyume na agano, atawadanganya na kuwatia uovu. Bali watu wale wanaomjua Mungu wao watakuwa jasiri na watachukua hatua.
33 “Wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa au kufanywa mateka.
Watu wenye hekima miongobi mwa watu watawafanya watu waelewe. Lakini watajikwaa kwa upanga na kwa miali ya moto; watatiwa mateka na kunyang'anywa kwa siku.
34 Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi ambao si waaminifu wataungana nao.
Katika siku za kujikwaa kwao, watasaidiwa kwa msaada kidogo. Watu wengi watajiunga nao wenyewe katika unafiki.
35 Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa mpaka wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamriwa.
Baadhi ya watu wenye hekima watajikwaa ili kujisafisha kutokee kwao, na kujiosha, na kujitakasa, mpaka wakati wa mwisho. Kwa kuwa wakati ulioamriwa haujaja bado.
36 “Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajasikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitokee.
Mfalme atafanya kutokana na matakwa yake. Atajiinua mwenyewe na kujifanya mkubwa kuliko kila mungu. Kinyume cha Mungu wa miungu, atasema vitu vibaya, kwa kuwa atafanikiwa mpaka pale ghadhabu itakapokuwa imekamilika. Kwa ajili kile kilichoamriwa kitakapokuwa kimefanyika.
37 Hataonyesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote.
Hatazijali miungu ya baba zake wala mungu anayependwa na wanawake. Wala hatamjali mungu mwingine yeyote. Kwa kuwa zaidi ya mtu yeyote atajifanya mwenyewe kuwa mkuu.
38 Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani na zawadi za thamani kubwa.
Atamheshimu mungu wa ngome badala ya haya. Ni mungu ambaye baba zake hawakumkubali ambaye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa mawe ya thamani na zawadi zenye kuthaminiwa.
39 Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala juu ya watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama.
Atazishambulia ngome imara sana kwa msaada wa mungu mgeni. Atampa heshima kubwa yeyote anayemkubali. Atawafanya kuwa watawala juu ya watu wengi, na ataigawanya nchi kama thawabu.
40 “Katika wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko.
Kwa wakati wa mwisho mfalme wa Kusini atamshambulia. Mfalme wa Kaskazini atamvamia kwa ukali wa magari na wapanda farasi, na meli nyingi. Naye ataenda kinyume cha nchi, kuwagharikisha, na kupita katikati.
41 Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake.
Naye ataingia katika nchi ya uzuri, makumi elfu ya Waisraeli wataanguka. Lakini watu hawa watatoroka kutoka katika mkono wake: Waedomu, Wamoabu, na mabaki ya watu wa Amoni.
42 Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka.
Naye ataunyosha mkono katika nchi; nchi ya Misri haitaokolewa.
43 Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na utajiri wote wa Misri, pamoja na Walibia na Wakushi kwa kujisalimisha.
Atakuwa na mamlaka juu ya hazina za dhahabu na za fedha, na juu ya utajiri wote wa Misri; watu wa Libya na Ethiopia watakuwa chini katika nyayo za miguu yake.
44 Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu kabisa wengi.
Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamwogopesha, naye atatoka akiwa mwenye hasira nyingi kuwa ili kuwaharibu kabisa na kuwahifadhi kwa ajli ya uharibifu.
45 Atasimika hema zake za ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.
Naye ataisimamisha hema ya makao yake ya kifalme kati ya bahari na milima ya uzuri wa utakatifu. Ataufikia mwisho wake, na hapatakuwa na msaidizi wa kumsadia.