< Danieli 1 >

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi.
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja Yerusalemu na kuuzunguka mji ili kuzuia mahitaji yake yote.
2 Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
Bwana alimpa Nebukadneza ushindi dhidi ya Yehoyakimu mfalme wa Yuda, na alimpatia vitu vitakatifu kutoka nyumba ya Mungu. Alivipeleka vitu hivyo mpaka katika nchi ya Babeli, kwa nyumba ya mungu wake, na aliviweka vitu vitakatifu katika hazina ya mungu wake.
3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu,
Mfalme akamwambia Ashipenazi, afisa wake mkuu, awalete baadhi ya watu wa Israeli, wa familia ya kifalme na za kiungwana -
4 vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo.
vijana wasio na hila, wenye mwonekano wa kuvutia, wenye ujuzi katika hekima yote, wenye kujawa na ufahamu na weledi, na wenye sifa za kutumika katika ikulu ya mfalme. Alitakiwa kuwafundisha maandiko na lugha ya Babeli.
5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
Mfalme aliwatengea kwa ajili yao fungu kutoka katika chakula chake kizuri kwa kila siku na katika divai aliyokunywa. Vijana hawa walitakiwa kufunzwa kwa miaka mitatu, na baada ya hapo, wangeweza kumtumikia mfalme.
6 Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria.
Miongoni mwao walikuwa ni Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria, baadhi ya watu wa Yuda.
7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.
Afisa mkuu aliwapa majina: Danieli alimwita Belteshaza, Hanania alimwita Shadraka, Mishaeli alimwita Meshaki, na Azaria alimwita Abedinego.
8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii.
Lakini Danieli alinuia katika akili yake kuwa asingejitia ujanisi mwenyewe kwa chakula kizuri cha mfalme wala kwa divai ambayo alikunywa.
9 Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli,
Basi, aliomba ruhusa kutoka kwa afisa mkuu ili kwamba asije akajitia uchafu yeye mwenyewe. Hivyo, Mungu alimpa Danieli kibali na huruma kupitia katika heshima ambayo afisa mkuu alikuwa nayo kwake.
10 lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”
Afisa mkuu alimwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme. Ameagiza aina ya chakula na vinywaji mnavyotakiwa kutumia. Kwa nini awaone ninyi mkiwa mnaonekana vibaya kuliko vijana wengine wa umri wenu? Mfalme aweza kukitwaa kichwa changu kwa sababu yenu.
11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria,
Kisha Daniel akamwambia msimamizi ambaye afisa mkuu alikuwa amemweka juu ya Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria.
12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa.
Alisema, “Tafadhari tujaribuni, sisi watumishi wako kwa siku kumi. Tupatieni tu mboga mboga za kula na maji ya kunywa.
13 Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.”
Kisha ulinganishe mwonekano wetu na mwonekano wa vijana wanaokula vyakula vya mfalme, na mtutendee, sisi watu wako kulingana na kile unachokiona.”'
14 Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.
Hivyo msimamizi alikubaliana naye kufanya hivi, na aliwajaribu kwa siku kumi.
15 Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko yeyote kati ya wale vijana waliokula chakula cha mfalme.
Katika mwisho wa siku kumi mwonekano wao ulikuwa ni wenye afya nzuri kuliko wa wale vijana waliokula vyakula vya kifalme.
16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.
Basi, msimamizi aliliondoa fungu lao la chakula na vivywaji vyao na walipewa mboga mboga tu.
17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
Na kuhusu vijana hawa nne Mungu aliwapa uelewa na ufahamu katika maandiko yote na hekima, na Danieli aliweza kupambanua aina zote za maono na ndoto.
18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza.
Katika mwisho wa muda uliokuwa umepangwa na mfalme kuwaleta ndani, afisa mkuu aliwaleta mbele ya Nebukadneza.
19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme.
Mfalme aliongea nao, na miongoni mwa kundi lote hapo hapakuwa na wa kuwalinganisha na akina Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria. Walisimama mbele ya mfalme, wakiwa tayari kumtumikia.
20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.
Katika kila swali la hekima na ufahamu ambalo mfalme aliwauliza, aliwakuta wakiwa na uwezo mara kumi kuliko waganga wote na wale waliojidai kusema na wafu, waliokuwa katika ufalme wake wote.
21 Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.
Danieli alikuwa hapo mpaka mwaka wa kwanza wa Mfalme Koreshi.

< Danieli 1 >