< Wakolosai 4 >
1 Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua ya kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.
3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa.
4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.
5 Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
6 Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.
7 Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana.
8 Nimemtuma kwenu kwa madhumuni haya ili mpate kufahamu hali yetu, na pia awatie moyo.
9 Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.
10 Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.)
11 Yesu, yeye aitwaye Yusto, pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.
12 Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti.
13 Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.
14 Rafiki yetu mpenzi Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.
15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake.
16 Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kanisa la Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.
17 Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana.”
18 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi. Amen.