< Wakolosai 2 >
1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi.
Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho.
2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe,
Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe.
3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.
Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu.
4 Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi.
Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana.
5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.
Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo.
6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake,
Maadamu ninyi mmemkubali Kristo Yesu kuwa Bwana, basi, ishini katika muungano naye.
7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.
Mnapaswa kuwa na mizizi ndani yake, kujijenga juu yake na kuwa imara katika imani yenu kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele.
8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.
Angalieni basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe!
9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu,
Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu,
10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka.
nanyi mmepewa uzima kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote.
11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo,
Katika kuungana na Kristo ninyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi.
12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo, mlifufuliwa pia pamoja naye kwa imani yenu katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka wafu.
13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote,
Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote;
14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake.
alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani.
15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.
Juu ya msalaba Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.
16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato.
Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya Mwezi mpya au Sabato.
17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo.
Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo.
18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu.
Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganifu za kidunia
19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.
na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu.
20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri:
Ninyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa kutoka nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti:
21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”?
“Msishike hiki,” “Msionje kile,” “Msiguse kile!”
22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu.
Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu.
23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.
Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima katika namna ya ibada ya kujitakia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutendea mwili kwa ukali; lakini kwa kweli, haifai chochote kuzuia tamaa za mwili.